Stori kubwa zilizopewa Headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania February 20, 2015
NIPASHE
Wasomi, wanasiasa na wanaharakati
nchini, wamepokea kwa hisia tofauti uteuzi alioufanya na Rais Jakaya
Kikwete, wa wakuu wa wilaya wapya, huku baadhi wakikosoa uteuzi wa mkuu
mpya wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na wengine wakiunga mkono.
Juzi Rais Kikwete aliteua wakuu wa wilaya wapya 27, akiwamo Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Uhamasishaji na Chipukizi, Makonda, kuwang’oa 19 na kuwahamisha 64.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana,
baadhi walisema Rais Kikwete amefanya jambo la busara kuboresha utendaji
kazi serikalini, lakini wakasema kumpa Makonda wadhifa huo kunaweza
kudhoofisha utendaji wa kazi katika wilaya ya Kinondoni.
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof. Mwesiga Baregu,alisema
Makonda alituhumiwa kumfanyia fujo aliyekuwa Mwenyekiti wa tume hiyo,
Jaji Joseph Warioba, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi
yake.
“Hakuna uchunguzi wa polisi au kiusalama juu ya Makonda. Kutochukuliwa hatua kunadhihirisha mambo aliyoyafanya aliagizwa,”:- Prof. Baregu.
Alisema uteuzi huo wa wakuu wa wilaya
wapya unaweza ukawa kinga kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiimarisha
katika uchaguzi mkuu na kura ya maoni za katiba inayopendekezwa.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratia Mukoba,
alisema Rais Kikwete amefanya kitendo kizuri kuteua wakuu wa wilaya,
lakini akasema kitendo cha kumpa Makonda ukuu wa wilaya ya Kinondoni
siyo chema.
Alisema Makonda amepewa wilaya kubwa na hana uzoefu wowote wa kuongoza wilaya, kwani hajawahi hata kuongoza kata.
“Sijawahi
kumsikia akiongoza hata kata. Sana sana amewahi kuongoza Tahliso (Umoja
wa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu). Mtoto mdogo kama yule kumfanyia
fujo mzee kama yule aliyeliletea sifa taifa na leo anakuwa mkuu wa
wilaya ni jambo la kushangaza sana,”Mukoba.
NIPASHE
Wananchi wa vitongoji vya Kazunzu,
kijiji cha Nyambemba, kata ya Kazunzu, wakishirikiana na wa kitongoji
cha Lueseselo, kata ya Bulyaheke, wamempiga kwa marungu, mawe na
mapanga na kisha kumchoma moto mtu ambaye bado hajafahamika, wakimtuhumu
kuwa wakala wa kuteka watoto wakiwamo walemavu wa ngozi (albino), akishirikiana na waganga wa kienyeji wapiga ramli kwa imani za kishirikina za kupata utajiri.
Mbali ya kumuua, wananchi hao pia
wamevunja na kuchoma moto nyumba 13 zilizoezekwa kwa bati mali ya mganga
wa kienyeji mwanamke mpiga ramli mwenye umri wa miaka 40 (jina
linahifadhiwa), Hata hivyo, mganga huyo na familia yake walifanikiwa
kuwatoroka wananchi hao.
Tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana katika kijiji cha Bulyaheke, kata Bulyaheke,baada ya wananchi kumkamata mtuhumiwa huyo katika kijiji cha Kazunzu na kuwaongoza hadi kijiji cha Bulyaheke kwa mganga huyo.
Richard Mangalamu baba wa mwanafunzi aliyetekwa, Winfrida
(11) anayesoma darasa la nne Shule ya Msingi Kazunzu, alisema mtuhumiwa
alimwachia mwanafunzi huyo kutokana na kumkuta ana chale mgongoni na
kifuani akidai amepoteza ubora.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Wilaya ya Sengerema, Babu Sanare na Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Enock Mabula, kwa nyakati tofauti walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Naye Diwani wa Bulyaheke, Bagadi Nyuki,
akiwa eneo la tukio, alisema chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kudaiwa
kuwa juzi alimteka mwanafunzi wa kike anayesoma darasa la nne katika
Shule ya Msingi Kazunzu na kumvutia vichakani na kisha kumvua nguo na
kumpapasa.
NIPASHE
Mkoa wa Pwani umekumbwa na maafa
kufuatia mvua kubwa zilizoyesha mapema wiki hii zikiambatana na kimbunga
na radi katika wilaya za Kibaha na Bagamoyo, kujeruhi watu 12, kubomoa
nyumba 128 na nyingine kuezuliwa paa.
Hayo yalisemwa katikati ya wiki hii na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo wakati akitoa salamu za mkoa wake kwa Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal wakati wa hafla ya uzinduzi wa barabara ya Msoga- Msolwa yenye urefu wa kilomita 10 na ukaguzi wa mzani wa Vigwaza.
Ndikilo alisema mvua hizo zilizonyesha
kwa saa mbili mfululizo katika wilaya hizo, zimesababisha zaidi ya watu
200 kukosa mahali pa kuishi, wengi wao wakiwa ni wa Jimbo la Chalinze
lililopo wilayani Bagamoyo.
Alisema tathimini ya awali inaonyesha
katika kijiji cha Msoga, nyumba 47, Shule ya Msingi Msoga na Ofisi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kata zimeathiriwa na mvua hizo na watu 11
kujeruhiwa.
Alisema vilevile katika kijiji cha Tonga
nyumba nne zimeathirika, kijiji cha Ngeta Kibaha Vijijini nyumba 77 na
mtu mmoja kujeruhiwa.
Alisema majeruhi wawili baba na mtoto wake wamelazwa Hospitali ya Tumbi Kibaha kwa uangalizi zaidi wa madaktari.
Alisema Serikali ya Wilaya ya Bagamoyo
na Kibaha kwa ushirikiano na Serikali ya Mkoa zinaendelea kufanya
tathimini ya maafa hayo ili kuwasaidia waathirika ambao kwa sasa
wanahifadhiwa kwa ndugu, jamaa na jirani zao.
MWANANCHI
Ilikuwa ni kama marudio ya ajali ya
mwaka 2002, lakini ukubwa wa athari za tukio la jana unatofautiana baada
ya watu watatu kufariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa wakati
wakijaribu kuchota mafuta kutoka kwenye lori lililopinduka katika Kijiji
cha Idweli.
Lori hilo lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Malawi, lilipinduka kwenye milima ya Mporoto,
eneo ambalo ajali kama hiyo ilitokea mwaka 2002 na kuua watu 40 na
wengine 100 kujeruhiwa na moto uliolipuka wakati wanakijiji wakijaribu
kuiba mafuta kutoka kwenye lori hilo.
Usiku wa kuamkia jana, hali ilikuwa kama
hiyo katika Kijiji cha Idweli, Rungwe wakati lori jingine lilipolipuka
kwenye Barabara ya Mbeya-Malawi.
Katika tukio hilo, watu watatu
walifariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa kwa moto uliowafuata hadi
kwenye nyumba zao walikoficha mafuta waliyoiba kutoka kwenye lori hilo.
Ofisa Tabibu wa Hospitali ya Igogwe, Alexanda Masaru
alisema alipokea miili miwili ya watu na mmoja alifariki wakati
akipatiwa matibabu na wengine 16 walilazwa baada ya kuungua sehemu
mbalimbali.
MWANANCHI
Wakati Watanzania wakizidi ‘kutoboa’
mifuko yao kununua vifurushi vya kupiga simu na kutuma ujumbe wa mfupi,
baada ya mabadiliko ya viwango vya huduma hizo, Kampuni ya Simu za
Mkononi ya Tigo imesema mabadiliko hayo hayazuiliki kutokana na
changamoto za uwekezaji.
Mkurugenzi Mkuu mpya wa Tigo, Cecile Tiano
alisema jana kuwa Tanzania ni nchi yenye bei za chini za huduma za simu
Afrika Mashariki, huku kodi zake zikiwa juu, jambo linalowapa ugumu
kibiashara.
“Tuna mipango yetu ya kuwekeza Sh221 bilioni mwaka huu, lakini hatuwezi kuendeleza uwekezaji huo kwa mazingira magumu yaliyopo,” :- Tiano.
Tigo ambao waliongeza wateja wao kwa
asilimia 20 hadi kufikia wateja milioni tisa mwaka jana, wanatarajia
kuongeza minara 787 ya intaneti ya 3G na 4G.
Mabadiliko ya huduma za vifurushi vya
simu katika mitandao ya Tigo na Vodacom yamezua mjadala mzito nchini
hasa kwa watumiaji wa mtandao wa intaneti.
MWANANCHI
Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yohana Bahati
(1), aliyetekwa juzi katika Kijiji cha Ilelema, wilayani Chato mkoani
Geita na kuokotwa katika Hifadhi ya Biharamulo akiwa amekufa bila mikono
wala miguu, atazikwa leo saa 5 asubuhi katika Kijiji cha Ibondo, mkoani
Geita chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Yohana alitekwa nyumbani kwao saa mbili
usiku, akiwa amebebwa na mama yake. Tukio la kutekwa mtoto huyo
lilifanywa na watu wawili, ambao pia walimjeruhi mama huyo kwa kumkata
mapanga kichwani.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo alisema juzi kuwa mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye shamba la mahindi katika Kijiji cha Kimasa.
Alisema mwili huo uliokotwa juzi Februari 17, saa 12 jioni kwenye makazi yasiyo rasmi.
Ndugu wa marehemu, walisema Kamanda
Konyo ameahidi kutoa ulinzi mkali wakati wa mazishi hayo kutokana na
mazingira ya tukio lenyewe.
MTANZANIA
Mwakilishi wa Magomeni visiwani Zanzibar, Salmin Awadhi Salmin (CCM),
amefariki dunia ghafla baada ya kuanguka katika kikao cha Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kinafanyika katika ofisi kuu ya chama
hicho, Kisiwandui mjini Unguja.
Taarifa hiyo ilianza kuenea mjini Unguja
jana saa 6 mchana, na hata kuzua maswali kutoka kwa wananchi kuhusu
utata wa kifo chake.
Salmin (57) ambaye pia alikuwa ni
mnadhimu wa wawakilishi wa CCM na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho
(CC), alikuwa mmoja wa wawakilishi wanaopinga mfumo wa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa (SUK) kwa kutaka wananchi waulizwe kama bado wanahitaji muundo huo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vua
Ali Vuai, alisema kabla ya kufikwa na mauti, alianguka ghafla wakati
akitoka katika kikao hicho cha kawaida.
“Baada
ya Salmin kuanguka, baadhi ya viongozi na wafanyakazi kwa haraka
walimbeba na kumpeleka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya
matibabu na baada ya kufikishwa alipelekwa katika chumba cha wagonjwa
mahututi (ICU), ambako baada ya muda mfupi madaktari walithibitisha kuwa
amefariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu.
HABARILEO
Wanasiasa wamenyooshewa vidole,
wakihusishwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi baada ya matukio
hayo kuhusishwa na harakati za kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Vyama vya watu wenye ulemavu pamoja na
baadhi ya wadau kutoka vyama vya siasa, vimetaka Serikali kutopuuzia
dhana hiyo ya kuhusisha harakati za kisiasa na mauaji hayo.
Aidha, Chama cha Walemavu wa Ngozi
Tanzania, kimesema kiko katika maandalizi ya kufanya maandamano ya amani
hadi Ikulu kwa ajili ya kumwona Rais Jakaya Kikwetewapange mikakati ya kutokomeza mauaji hayo ya ukatili .
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa
na Shirikisho la Vyama vya Walemavu na Vyama vya Siasa nchini,
mwanachama kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Abdallahalisema
katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, alisema albino wanaishi kwa
wasiwasi kutokana na uwezekano wa mauaji hayo kuanza kuibuka tena kwa
kasi.
“Mimi mwenyewe nina tatizo la ngozi
(albino), hivi sasa tuko kwenye kipindi cha uchaguzi, na tetesi ni
kwamba wengi wanauawa kwa imani potofu za baadhi ya watu kutaka
madaraka, tusaidieni jamani ukweli ni kwamba tunaishi kwa hofu,” alisema.
Alisema ni vyema Serikali ikaacha
kupuuzia tetesi hizo za kuwahusisha baadhi ya watu wanaotaka madaraka na
kuagiza watu wenye ulemavu wauawe kwa imani za kishirikina.
Alitaka hatua madhubuti zichukuliwe kuokoa maisha ya Watanzania hao. “Jamani
tujue kuwa hii ni damu inayomwagika ni ya ndugu zetu, kama hatua
zisipochukuliwa inaweza kuwa laana kwa vizazi vyetu. Tukijipanga
Tanzania tunaweza kuwa salama,” alisisitiza.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment