HADITHI
YALIYONIKUTA TANGA (20)
ILIPOISHI TOLEO
LILILOPITA
Meja akanichagua mimi na
polisi mmoja mwenye bunduki tulinde ile nyumba hadi asubuhi ili mwizi asije akaingia
na kuiba vitu kwani mlango wake wa mbele ulikuwa umesindikwa tu kama ambavyo
tumeukuta.
Meja na polisi wengine
wakaondoka na kutuacha sisi. Saa yangu iliniambia ilikuwa saa tisa na nusu
usiku. Kulikuwa na baridi kali ambayo ilitupiga. Mimi ambaye nilivaa nguo
nyepesi ndio niliisikia vizuri sana.
Tukakaa pale barazani
kulinda ile nyumba kama tulivyoagizwa. Taa za ndani ya ile nyumba tulikuwa
tumezizima. Mara tukaona zile taa zinawashwa. Tukasikia kama sauti za mapanga
yakigongana pamoja na hatua za watu wanaopishana.
Wakati tumetega masikio
tukisikiliza, tulisikia sauti ambayo mimi niitambua kuwa ni ya yule mwanamke
ikisema.
“Chinja chinja tu
sasa…kila mtu chinja….hapana kuacha…!”
Ghafla tulisikia
kishindo kikubwa kwenye ule mlango wa mbele kama vile ulipogwa na kitu kizoto.
Mlango huo ukafunguka na kuwa wazi huku sauti ya yule mwanamke ikiendelea
kusikika.
“Chinja chinja tu
sasa…kila mtu chinja….!”
SASA ENDELEA
Tulisikia kishindo cha
watu waliokuwa wakikumbana kuwania kutoka katika mlango huo hku mlio wa mapanga
yanyoyogongana ukisikika.
Askari mwenzangu
niliyekuwa naye alikuwa wa kwanza kuinuka pale tulipokuwa tumeketi akatimua
mbio. Laiti kama ule mkanda wa buduki yake usingekuwa begani angeiacha bunduki
yake pale pale. Kwa vile alikuwa ameuvaa mkanda wa bunduki hiyo kwenye bega
aliweza kukimbia nayo.
Nilipoona mwenzangu
anatimua, na mimi nikainuka na kumuata mbio!
Tulichokikimbia hapo
ilikuwa ni kuchinjwa na majini. Tulishatia imani kuwa wale walikuwa majini na
ndio waliokuwa wamemchinja Sajenti Erick hivyo tilona kwamba na sisi
tungechinjwa kutokana na ile sauti iliyokuwa ikiashiria kuchinja.
Tuliendelea kwenda mbio
bila kutazama nyuma mpaka tukaikafika kituo cha polisi. Polisi wenzetu
walitushangaa.
“Vipi?” Polisi mmoja
akatuuliza.
Tukaeleza kilichokuwa
kimetutoa mbio. Hapo hapo ikapigwa radio Call, gari lililokuwa kwenye doria
likawasili. Mimi na mwenzangu tukapanda katika gari hilo kuelekea katika ile
nyumba.
Tulipofika tulishuka na
kwenda kwenye mlango. Tuliujaribu mlango na kukuta ulikuwa umeffungwa. Zile taa
zilizokuwa zimewashwa tulikuta zimezimwa.
Hakukuwa na dalili
yoyote iliyoonesha kuwa ndani ya nyumba hiyo mlikuwa na watu. Polisi mmoja
kampigia mkuu wa zamu wa kituo kutaka apewe ruhusa ili tuvunje mlango tuingie
ndani. Ile timu tuliyokwenda nayo ilikuwa haiamini mashetani.
Ruhusa ikatolewa kuwa
tunaweza kuvunja mlango na kuwakamata waliokuwa ndani. Polisi mmoja aliupiga
vikumbo vitatu mlango huo ukafunguka. Moyo wangu ulikuwa ukinienda mbio. Polisi
wakaingia ndani, mimi nilikuwa wa mwisho kuingia.
Niliwasha taa ya
ukumbini na na uani. Tukaanza kutafuta. Hatukukutamtu yeyote humo ndani. Nyumba
ilikuwa tupu.
“Wako wapi?” Polisi
mmoja aliyekuwa na kimbelembele akauliza kwa umori.
“Nadhani wameshaondoka”
nikamjibu.
“Wameondoka wamekwenda
wapi?”
“Hatuwezi kujua”
Nikapiga simu tena
kituoni kuwajulisha kuwa tumevunja mlango na tumeikuta nyumba iko tupu.
Amri tuliyopewa ni kuwa tubakishe
askari wawili walinde nyumba na wengine warudi kituoni. Polisi wawili
wakabakishwa kulinda nyumba na waliagizwa kumkamata mtu yeyote atakayeingia mle
ndani.
Tuliporudi kituoni, mimi
niliruhusiwa kurudi nyumbani. Ile gari ya doria ikanipeleka nyumbani. Asubuhi
kulipokucha nikaenda tena kituoni. Nikaambiwa ninaitwa kwa aisa upelelezi wa
mkoa.
Nilipofika akaniambia
ameshapata taarifa zote za matukio yaliyotokea usiku uliopita.
“Miujiza imekuwa mingi.
Utaanza likizo yako kesho isipokuwa tufahamishe utakuwa wapi ili
tutakapokuhitaji tuweze kukupata”
“Nitakuwa nyumbani
Kagera”
“Sawa. Leo kamilisha
taratibu za kuanza likizo, kesho utaondoka”
“Nashukuru aande”
Nikamuaga na kutoka.
Siku ya pili yake
nikaanza likizo yangu. Na siku ya tatu nikaondoka kwenda Dar nikiwa
nimekichukua kile kisanduku cha dhahabu. Nilikitia kwenye begi langu.
Nilipofika Dar siku
iliyofuata nikatafuta usafiri wa kuelekea Kagera. Mpaka ninafika kijijini kwetu
ilinichukua siku mbili. Japo nilikuwa nimekutwa na madhila huko Tanga, nilipata
furaha kukutana tena na wazazi wangu pamoja na ndugu zangu ambao tuliachana kwa
karibu miaka mitatu iliyopita.
ITAENDELEA
Kwa mengi mazuri na habari kemkem tembelea blog hii kila wakati kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment