Thursday, February 19, 2015

WANANCHI KATA YA MAWENI WAJA JUU

Tangakumechablogspot.com

Tanga,WANANCHI wa kata ya Maweni Tanga wamepinga tangazo la ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Tanga la kutaka viwanja walivyopima havitambuli kisheria na hivyo kuvirejesha na kupimwa upya.

Wakizungumza katika mkutano wa wananchi jana, wananchi hao, walisema viwanja walivyopewa ni halali na kupimwa kisheria kwa mujibu wa mamlaka ya Serikali ya kijiji na hivyo kuitaka ofisi hiyo kutambua vyenginevyo wataacha kulipa kodi za viwanja vyao.

Wameitaka ofisi hiyo kuacha kuingia katika mgogoro   kwani wananchi hao wameteseka kwa muda mrefu na hadi kufikia hapo wamechoka baada ya viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali  kuingilia kati na kufikia mufaka wa kuwepo maeneo hayo.

Viwanja  ambavyo vimetajwa kuwa yanahitaji kupimwa upya ni Maweni, Kichangani, Kasera na Kange na wananchi kuja juu kwa madai baadhi yao wameanza kujenga na baadhi yao kuhamia na familia zao.

“Tunasema kuwa viwanja ambavyo Serikali ya kijiji imepima na kugawa kwa wananchi hakuna tena mabadiliko kwani kila mmoja ameshamilikishwa kiwanja chake-----huko ni kuanzisha mgogoro ambao haupo” alisema Salim Juma Ricco

“Kwa sauti moja tunaiomba ofisi ya mkurugenzi kuacha kuanzisha mgogoro na wananchi kwani wamechoka na maisha na wakilingiza suala hili ambalo liko nyuma ya pazia ambalo hatujui lengo lake nini linaweza kuibua mengi” alisema

Kwa upande wake mkazi wa Kasera, Magreth Kashanga, amewataka wananchi wote ambao wanamiliki viwanja kihalali kuanza kujenga na kuwasiliana na viongozi wao wa Serikali za mitaa na kijiji.

Alisema Tanga imekithiri migogoro ya ardhi na kudai mingi inasababishwa na baadhi ya maofisa na hivyo kuitaka ofisi ya mkurugenzi wa jiji kuacha kuibua mgogoro ambao haupo.

Alisema toka viongozi wa Serikali za mitaa  minne kugawa viwanja ambavyo baadhi yao wamo wakazi wa Saru Magaoni ambao kwa jitihada za Mkuu wa Wilaya aliepita, Halima Dendego alifanya suluhu ya kuwapatia viwanja baada ya kutakiwa kuondoka maeneo yao kupisha ujenzi wa bandari mpya.

“Hatukubaliani na tangazo la ofisi ya jiji kutaka kupora viwanja vyetu sisi tunamiliki kisheria na tuko na karatasi tulizopewa na viongozi wetu wa Serikali za vijiji” alisema Kashanga

Aliwataka viongozi na wananchi kushikamana ili kuepusha na mgogoro wa kupandikizwa na kudai kama kutaendelea na chokochoko wananchi kwa pamoja watafanya safari ya kuonana na Waziri mwenye dhamana.

                                            Mwisho

No comments:

Post a Comment