Nimekurahishia kwa kukuwekea hizi stori kubwa nane kutoka MAGAZETINI FEB24
MWANANCHI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimeishinda CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika juzi
katika kata tatu za Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambazo
hazikufanya uchaguzi Desemba 14, mwaka jana.
Uchaguzi katika kata hizo uliahirishwa
kutokana na kasoro mbalimbali jambo lililosababisha mkurugenzi wa
halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, William Shimwela kusimamishwa kazi.
Msimamizi wa uchaguzi huo uliofanyika katika kata za Msua, Chanji na Kizwite na mitaa mingine miwili iliyorudia uchaguzi, Hamid Njovu alisema Chadema ilinyakua jumla ya mitaa 37 kati ya 44 na kuiacha CCM ikiambulia mitaa mitano.
Matokeo hayo mapya yanaibuka sasa wakati
Ofisi ya Waziri Mkuu ilishahitimisha kutangaza matokeo ya jumla ya
mitaa katika uchaguzi huo ikisema ulikuwa umekamilika kwa asilimia 100.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tamisemi,
Kalist Luanda alisema Desemba 24, mwaka jana kuwa mitaa yote 3,875
nchini ilifanya uchaguzi na kukamilika kwa asilimia 100 huku CCM ikipata
asilimia 66.66 baada ya kuzoa mitaa 2,583, ikifuatiwa na Chadema
iliyopata mitaa 980 (25.3%), CUF mitaa 266 ( 6.9%), NCCR Mageuzi mitaa
28 (0.7%), TLP mtaa mmoja (0.03%), ACT mitaa 12 (0.31%), UDP mitaa
mitatu (0.08%), NRA mtaa mmoja (0.03%) na UMD mtaa mmoja (0.03%).
Akitangaza matokeo hayo jana, Njovu
alisema katika Kata ya Kizwite kati ya mitaa 15 iliyofanya uchaguzi
Chadema ilishinda mitaa 13 dhidi ya CCM iliyoambulia mitaa miwili, Kata
ya Msua mitaa yote 13 iliyofanya uchaguzi ilikwenda kwa Chadema na CCM
kuambulia patupu.
Alisema kwa Kata ya Chanji ambayo
ilikuwa na mitaa 14 iliyofanya uchaguzi, Chadema ilishinda mitaa 10 na
CCM mitatu huku mtaa mmoja wa Nankasi kura ziligongana katika nafasi ya
uenyekiti, hivyo kuamuliwa uchaguzi utarudiwa Jumapili.
MWANANCHI
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu
amesema hivi sasa sekta ya Utalii ndiyo inayoongoza kwa kuliingizia
taifa mapato ya kigeni baada ya kuipita sekta ya dhahabu iliyoshuka
kutokana na kuporomoka kwa bei kwenye soko la dunia.
Akizungumza leo kwenye mkutano
uliojadili mabadiliko ya kiuchumi Tanzania, Profesa Ndulu amesema sekta
ya utalii inaliingizia taifa dola 2bilioni, dhahabu (dola 1.7bilioni),
bidhaa za viwandani (dola 1.3bilioni) na huduma za usafirishaji mizigo ni dola 800milioni.
Sekta ya utalii inaingiza Dola za
Marekani 2 bilioni kwa mwaka ikifuatiwa na dhahabu inayoipatia nchi Dola
za Marekani 1.7 bilioni, bidhaa za viwanda vinazouzwa katika nchi
mbalimbali barani Afrika inaingiza Dola za Marekani 1.3bilioni
ikifuatiwa na usafirishaji wa huduma za mizigo katika nchi jirani ambapo
zinaingiza Dola za Marekani 800milioni.
Profesa Ndulu amesema ongezeko la mapato
kwenye viwanda ni sawa na fedha zote za kigeni zinazotokana na mazao
sita makubwa ya kilimo nchini kwa pamoja.
“Mfumo
wa kuingiza mapato ya fedha za kigeni nchini umebadilika sana, mimi na
imani kuwa nafasi yetu kijiografia inatupa fursa kubwa sana ya kuhudumia
wengine walioko mbali na bahari,”:- Prof.Ndulu.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amemkabidhi Kiongozi wa Madhehebu ya Isimailia ulimwenguni, Mtukufu Aga Khan hati ya usajili wa Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) ikiwa ni hatua muhimu kwa taasisi hiyo kuendeleza utoaji wa elimu nchini.
Mara baada ya kukabidhi hati hiyo, Rais Kikwete alisema ni mara ya
kwanza kwa Chuo Kikuu cha kigeni kusajiliwa nchini na kwamba Aku
itatimiza matarajio ya wengi katika utoaji wa elimu bora.
Alisema Serikali imekuwa na uhusiano wa karibu na Mfuko wa Maendeleo
wa Aga Khan na umekuwa ukisaidia masuala mbalimbali yanayochochea
maendeleo nchini.
“Utoaji wa hati hii leo ni sehemu
tu ya hatua ya maendeleo hayo. Tunayo imani kuwa Chuo Kikuu hiki
kitasaidia kupunguza tatizo la upungufu wa rasilimali watu katika fani
za udaktari, sayansi na teknolojia,” alisema Rais Kikwete katika hafla iliyofanyika Ikulu.
Mtukufu Aga Khan alisema upatikanaji wa hati hiyo ni mwanzo wa safari
ya utoaji wa huduma za elimu nchini ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa
kukipanua chuo hicho kutoka nje ya Asia na kuimarisha mizizi barani
Afrika ili kupunguza umaskini.
Kiongozi huyo, ambaye pia ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa Mtandao wa
Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), alisema katika kipindi cha maendeleo ya
kasi, suala la elimu ni la msingi ili kukuza ugunduzi na uzalishaji.
“Chuo
kitakuwa na kozi tisa tofauti maalumu kwa ajili ya masuala ya Afrika
ambazo zitakuwa na umuhimu mkubwa na matokeo ya haraka kwa jumuiya ya
Tanzania.
NIPASHE
Wanafunzi sita, mwalimu wao, wamekufa
papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa kwa kupigwa na radi darasani wakati
mvua kubwa zilizoambatana na kimbunga zikinyesha.
Tukio hilo lilitokea saa 2:30 asubuhi katika Shule ya Msingi Nyakasanda iliyopo kijiji cha Nyaphenda wilaya ya Kasuru mkoani Kigoma wakati mwalimu huyo na wanafunzi hao wakiwa darasani.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, John Ndunguru, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati mvua hizo zikinyesha.
Alisema mazishi ya mwalimu huyo na
wanafunzi hao, yatafanyika leo mchana katika kijiji hicho chini ya
usimamizi wa kamati ya ulinzi ya mkoa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Jafari Mohamed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Hata hivyo Mohamed, alisema majina ya waliokufa yatafahamika leo wakati wa mazishi yao.
Vilevile alisema wanafunzi wengine 10 na
mwalimu wao waliojeruhiwa katika tukio hilo, wamelazwa katika Hospitali
ya Mkoa huo ya Maweni kwa matibabu.
NIPASHE
Zoezi la uandikishaji wapigakura katika
Daftari la Kudumu la Wapigakura limeanza katika Mkoa wa Njombe, huku
likikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo mashine za Biometric Voter Registration (BVR) kushindwa kutambua watu wenye vidole vyenye michilizi.
Kujitokeza kwa kasoro hizo kumekuja siku tatu tangu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alipoeleza kuwa amenasa nyaraka zinazoonyesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ilishauriwa na mtaalam kutoka Marekani kwamba Tanzania haijawa tayari kwa teknolojia ya BVR.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian
Lubuva, alisema zoezi la uandikishaji limeanza katika mkoa wa Njombe na
kwamba viongozi wa tume hiyo wapo kwa ajili ya kusimamia kuhakikisha
kunakuwa na mafanikio.
Jaji Lubuva alipoulizwa kama tume
imeanza na BVR ngapi, alisema suala hilo hawezi kulijibu. Hivi karibuni
kuriripotiwa kuwa Nec imepata BVR 250 tu kati ya 8,000 zinazotakiwa.
“Nipo
Njombe ndiyo tumeanza zoezi la kuandikisha, suala la kwamba tumeanza na
BVR ngapi sina jibu, kwanza nipo kwenye kikao,”alisema Lubuva na kukata
simu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nec, Julius Malaba, alisema uzinduzi rasmi wa uandikishaji katika mkoa wa Njombe utafanyika leo.
Kasoro nyingine zilizojitokeza ni
uchache wa vifaa,watoa huduma waliopewa jukumu hilo kushindwa kutumia
mashine na kulazimika kutumia muda mwingi kumwandikisha mtu mmoja hali
inayotia wasiwasi kwamba huenda siku saba zilizopagwa kufanyika kwa kila
mkoa kushindwa kufikia malengo.
NIPASHE
Mbivu au mbichi za vigogo 99 wa Tanzania
waliotajwa kuficha mabilioni ya fedha kwenye akaunti za siri nchini
Uswiss zitajulikana hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema.
Kwa mujibu wa Zitto, PAC imewaita Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu; Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk. Rished Bade, ili kuhojiwa na kamati yake Machi 9, mwaka huu.
Zitto alisema majina ya watu au kampuni
zinazohusika na mabilioni hayo vitajulikana kwa kuwa serikali
imeshachunguza na ripoti iko tayari.
“Tumewaita
BoT, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna Mkuu wa TRA Machi 9 waje
kwenye kamati kujieleza…tunategemea serikali ina taarifa zote kwa sababu
sehemu kubwa ya fedha zinazotoroshwa nje ni kwa nia ya kukwepa kodi.
Kwa hiyo, TRA watakuwa wanawajua,”:-Zitto.
Aliongeza: “Siwezi kumtaja mtu yeyote kwa sasa. Lakini bila shaka wahusika wakuu watakuwa wafanyabiashara wakubwa.”
Kwa upande wake, Prof. Ndulu alisema
ameitwa na PAC, lakini hawezi kuueleza umma taarifa zozote kwa sasa kwa
kuwa atajieleza kwenye kamati.
“Subirini, mimi nimeshaitwa kwenye kamati. Nitajieleza huko…unataka niseme nini sasa hivi wakati nitahojiwa huko?” Alihoji Prof. Ndulu.
Tuhuma za vigogo wa Tanzania kuficha
mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi ziliibuliwa upya hivi
karibuni baada ya ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa
Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ), kutaja vigogo 99 wenye akaunti
za siri nchini humo.
HABARILEO
VIONGOZI wa madhehebu ya dini jijini
Mwanza, wakiwamo Maaskofu na Mashehe jana walijikuta wakibubujikwa na
machozi baada ya kumtembelea Ester John, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Ester amelazwa baada ya kujeruhiwa
vibaya na watu wasiofahamika, ambao walimteka mwanawe mwenye ulemavu wa
ngozi (albino), Yohana Bahati na kutokomea naye kusikojulikana.
Viongozi hao wakiwemo maaskofu 10 na
mashehe 10 walimtembelea Ester hospitalini hapo jana, ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya kongamano kubwa la amani linalotarajiwa kufanyika
Februari 28 mwaka huu kuiombea nchi amani na kulaani mauaji ya albino.
Mashehe na maaskofu hao walimuombea dua
na sala Ester aweze kupona haraka na walilaani kitendo cha kinyama,
alichofanyiwa na wauaji hao. Waliiomba Serikali ichukue hatua za haraka
kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
Akizungumza hospitalini hapo huku
akitokwa na machozi katika Wadi Namba 9 alikolazwa Ester, Mwenyekiti
Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa ya Viongozi wa Dini, Shekhe Hassan Kabeke
alisema wanaungana kwa pamoja kulaani matukio mawili ya kinyama ya
kuuawa kwa mtoto Yohana na kujeruhiwa vibaya mama yake mzazi.
“Maneno
ya kusema yananiishia baada ya kumuona Ester, mimi nadhani hakuna
sababu ya kuremba maneno dhidi ya ukatili huu wa kinyama, nasikia
maumivu makali sana ndani ya moyo wangu kama kiongozi wa kiroho,
tunaitaka serikali katika hili isiondoe adhafu ya kifo kwa kisingizio
cha haki za binadamu”, alisema.
HABARILEO
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia vijana watano wa kundi la wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa tuhuma za kufanya uchochezi na kufanya mikusanyiko isiyo halali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alisema vijana hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti kwa makosa ya kuunda
kikundi kisicho halali kwa mujibu wa sheria za nchi na kuwahamasisha
wenzao, kuandamana hadi Ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete kudai ajira za kudumu.
“Tunawashikilia
vijana watano ambao ndio viongozi wa kikundi kinachojiita umoja wa
wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa. Mwenyekiti ndio alikuwa wa kwanza
kukamatwa na wengine tuliwakamata juzi mara baada ya kukusanyika eneo la
Msimbazi Centre na Muhimbili,”:-Kova.
Akieleza chanzo cha vijana hao kutaka
kuandamana kuelekea Ikulu, alidai wahitimu hao wanadai kuahidiwa ajira
za kudumu walipomaliza mafunzo yao na hivyo baada ya kukaa kwa muda
mrefu bila kuajiriwa, ndipo wakaamua kuanzisha kikundi hicho ili kwenda
kumwona Rais Kikwete kumweleza tatizo la ajira linalowakabili.
“Vijana
hawa wanadai kuwa waliahidiwa kupewa ajira za kudumu mara baada ya
kumaliza mafunzo yao ya JKT. Jambo hili sio la kweli, kwani tumefanya
uchunguzi na kubaini hakuna mkataba wowote unaosema wakimaliza mafunzo
lazima waajiriwe, bali kila mtu anatakiwa kutumia ujuzi alioupata
kujiajiri.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot/com
No comments:
Post a Comment