Tangakumekuchablog
Korogwe, WAKAZI wa vijiji vya Kwamsisi, Kwakombo na Maili kumi
Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, wamelitaka Shirika la umeme Tanzania (Tanesco)
kutoa elimu ya matumizi ya umeme ili kuepusha hatari kabla ya kuanza kuwafungia
mita majumbani.
Wakizungumza kwa vyakati
tofauti wakati wa utoaji elimu mradi wa usambazaji umeme vijijini (Rea)
uliofanywa na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa
Tanga, wakazi wengi wamedai hawana elimu ya matumizi ya umeme.
Wamelitaka shirika hilo
kuwahamasisha wateja wake kujenga nyumba bora na imara ili kuwa rahisi
kuunganishiwa umeme jambo ambalo litapunguza idadi ya nyumba za nyasi na
makuti.
Walisema mradi huo wa
usambazaji umeme vijijini utakuwa msaada mkubwa kwa shughuli
za maendeleo hasa kwa wakulima wa matunda na mbogamboga jambo ambalo
litawakomboa na kuongeza kipato.
“Mradi huu wa usambazaji umeme
vijijini kwa kweli ni mapinduzi makubwa si kwa viburudisho tu majumbani bali
hata sisi wakulima tutaweza kuhifadhi matunda yetu na kuepuka vitisho vya
kutuozea majumbani” alisema Hamis Shomari
“Mara nyingi kama mchicha na
matembele usipouza kwa wakati unajikutaka unauza majani makavu ambayo hata
mnyama hawezi kula tena kwani itakuwa imekauka----umeme vijijini utakomesha pia
biashara ya ulanguzi” alisema
Shomari amelitaka shirika hilo
kuwapunguzia gharama za matumizi na kuwa tofauti na watu wanaoishi mjini kwani
kufanya hivyo watashindwa kulipa Ankara za matumiz yao.
Alisema ni lazima kuwepo na
utofauti ya Ankara za watu wa vijijini na wa mjini kwani wengi hawana vipato
vya kuwawezesha kulipa sawa na watu wanaokaa mjini ambao wako na nyenzo nyingi
za kuwaingizia vipato na kumudu gharama za maisha.
Akizungumza wakati wa uhamasishaji
wa wananchi kuupokea mradi huo wa umeme vijijini, Afisa habari na huduma kwa
wateja, Monica Mabada, amewataka wananchi kuilinda miundombinu ya umeme na
kuwafichua mafundi vishoka.
Alisema ujio wa mradi wa usambazaji
umeme vijijini kunaweza kujitokeza wafanyakazi feki wa shirika la umeme Tanesco
na hivyo kuwataka kuwafichua na kuepuka njama za kulipa Ankara mikononi.
Alisema zipo taarifa za kuwepo kwa
vishoka wanaopita majumbani kuwadai wananchi kutaka kuwafungia umeme kwa
gharama za juu ikiwa lengo ni kujipatia pesa kwa udanganyifu na hivyo
kuwakumbusha taratibu zote zinafanyika ofisi za shirika hilo.
“Ndugu zangu wananchi wa Kwamsisi
nawapa tahadhari na mafundi vishoka kwani ujio wa umeme vijijini kunaweza
kuzuka matapeli na kuwahadaa ili kujipatia pesa kwa udanganyifu” alisema Mabada
“Taratibu zote zihusuzo umeme
zinafanyika ofisi za shirika la umeme Mkoani au Wilayani----epukeni kulanguliwa
kwani taarifa tulizonazo ni kuwa wameanza kujingiza maeneo yenu” alisema
Aliwataka kuitumia fursa ya ujio wa
umeme katika maeneo yao kwa kuanzisha fursa mbalimbali za kuingiza kipato
ikiwemo viwanda vidogovidogo vya kusindika matunda na ufundi mhuzi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment