Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu ChaCandle Education Centre Tanga, kituo kinapokea wanafunzi wa kidato cha pili hadi cha sita kwa kujiandaa na mitihani, Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Watu 42 wamepoteza maisha na wengine 23
kujeruhiwa baada ya lori la mizigo kugongana na basi na kontena
lililokuwa limebebwa kuangukia gari hilo la abiria, katika ajali ya aina
yake iliyotokea eneo la Mafinga Changalawe mkoani Iringa.
Watu 37 waliokuwa kwenye basi hilo la kampuni ya Majinjah Express
lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam, walifariki papo hapo
na wengine watano kufariki wakiwa Hospitali ya Mafinga. Dereva wa basi
na wa lori hilo la kampuni ya Cipex, pia wamefariki.
Shuhuda mmoja wa ajali hiyo, Nyasio Pascal,
aliyekuwa akiendesha basi la Saibaba, alisema aliliona lori hilo
likijaribu kukwepa mashimo kwenye barabara hiyo ambayo ni nyembamba, na
mara likaanza kuyumba kulia na kushoto baada ya kukanyaga shimo na ndipo
lilipolifuata basi na kugongana nalo.
Alisema kontena lililokuwa limebebwa na
lori hilo, liliangukia juu ya basi na kulikandamiza, jambo ambalo
lilisababisha vifo vya watu wengi na pia kuzuia watu waliokuwa karibu na
ajali kuokoa watu waliojeruhiwa hadi tingatinga lilipowasili. Hata
hivyo, alisema mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja, alinusurika
kwenye ajali hiyo bila ya kudhurika.
Miili ya waliokufa imehifadhiwa kwenye
Hospitali ya Mafinga, ambayo ina chumba cha kuhifadhia miili ya watu
saba tu, na mingine imepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa.
“Hii ni ajali mbaya ambayo haijawahi kutokea mkoani hapa,” alisema mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyefika eneo hilo la ajali.
NIPASHE
Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, Zitto amesema hajapewa taarifa rasmi, hivyo ataendelea kuwa mbunge.
Pamoja na kauli hiyo ya Zitto, viongozi
wa Chadema wamesema hawatahangaika kumwandikia barua kumjulisha hatua
zilizochukuliwa na chama hicho dhidi yake.
Zitto akizungumza na waandishi wa habari
jana katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, alisema
ataendelea na kazi yake ya ubunge kwasababu hajapewa taarifa rasmi na
Chadema kuhusu uamuzi uliochukuliwa wa kumvua uanachama.
“Sina
taarifa rasmi kilichotokea na kama mnavyoona naendelea na vikao vya
kamati kama kawaida na leo (jana) nitakuwa na watu wa Benki Kuu (BoT),
TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali),
Ijumaa nitakwenda Kigoma jimboni kwangu kwa ajili ya kazi zangu,
niliwahidi wananchi wangu nitakwenda kabla ya kwenda bungeni, kimsingi
mimi bado ni mbunge,” Zitto.
Licha ya Chadema kutangaza kumvua uanachama, Zitto jana aliendesha vikao vya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kama kawaida.
Zitto alisema hawezi kujibishana na
chama chake kwani hajalelewa katika maadili kama hayo na kwamba kitu
muhimu kwake ni kazi ya kuwatumikia Watanzania.
“Mimi
huwezi ukanilinganisha na mbunge yeyote katika kazi ambazo nimekuwa
nikizifanya, siasa kwangu ni ‘issues’ tofauti na watu wengine ambao
siasa zao ni kugombana na watu, kwangu hizi ni changamoto, nakomazwa,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu,
alisema chama hicho hakitahangaika kumwandikia barua Zitto kumjulisha
uamuzi wake kwa kuwa anajua alishakiuka Katiba ya chama kwa kushtaki
hivyo uanachama wake unakoma mara moja.
NIPASHE
Kundi jipya la kihalifu linalojulikana
kwa jina la Libya limeibuka jijini la Dar es Salaam na kuvamia eneo la
kituo cha daladala cha Tabata Mawenzi na kufanya uharibifu mkubwa
uliosababisha magari kadhaa kuvunjwa vioo na kuzua taharuki kubwa
miongoni mwa wakazi, wafanyabiashara na wapita njia katika eneo hilo.
Kundi hilo limeibuka ikiwa ni miezi chache baada ya kundi la vijana wa kihalifu, maarufu kama ‘Panya Road’ kufanya vurugu na kuzusha hofu kubwa jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea jana na vijana
wawili wametiwa mbaroni na hadi tunakwenda mitamboni walikuwa
wakiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala, Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Mary Nzuki, alithibitisha kutokea vurugu hizo.
Vurugu hizo zilizuka juzi majira ya saa 8
mchana baada ya vijana hao kutoka kwenye mazishi ya mwenzao anayedaiwa
kuuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira.
Kijana huyo, Amiri Shabani
(14-15), maarufu kwa jina la “Ega”, ambaye ni mkazi wa maeneo ya mtaa
wa Twiga, kata ya Kimanga, anadaiwa kuuawa usiku wa kuamkia juzi.
Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa,
kijana huyo aliuawa kwa kupigwa na wananchi hao baada ya kumvamia njiani
mwanamke aliyekuwa akipita eneo la Mawenzi na kujaribu kumpora mkoba
wake, ambao ndani yake kulikuwa na fedha.
NIPASHE
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi kubaini zilikopotelea Sh. milioni 699 zilizotolewa na Wizara ya Fedha kwenda Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambazo hazijulikani ziliko sasa.
Aidha, PAC imeagiza Tanesco kuwasilisha
katika ofisi ya Bunge mikataba yote ya kampuni zinazozalisha umeme
nchini ambazo zimeingia nayo mikataba ili kupitiwa upya na kuwa
kumbukumbu kwa Bunge.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe,
alitoa maelekezo hayo jana katika kikao baina ya kamati hiyo na
menejimenti ya Tanesco na kusema kumekuwa na mvutano kuhusu Sh. milioni
699 zilizotolewa na Hazina kwenda Tanesco.
Zitto alisema inawezekana fedha hizo
zimetolewa kwa Tanesco, lakini zimetumika vibaya au Hazina wamezitoa kwa
mtu tofauti, hali ambayo imekuwa ikileta mkanganyiko ambao unahitaji
kufanyiwa uchunguzi.
Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha Tanesco, Anetha Chegula,
alisema fedha hizo zinadaiwa kutolewa na Hazina tangu mwaka 2012 kwenda
Tanesco kwa ajili ya kusaidia miradi ya umeme, lakini hazijafika katika
shirika hilo licha ya Hazina kuonyesha kuwa zilishatolewa.
Chengula alisema wamekuwa wakiitaka
Hazina kuonyesha vielelezo vinavyoonyesha kuwa fedha hizo zimepelekwa
Tanesco, lakini hadi mwaka jana Hazina haikufanya hivyo huku Tanesco
ikifanya uchunguzi katika akaunti zake bila kuziona fedha hizo.
Akizungumzia mikataba ya makampuni ya
Agrecco, Symbion, Songas na IPTL , alisema ipelekwe haraka ofisi za
Katibu wa Bunge ili iwe kumbukumbu kwa Bunge.
Wabunge walisema tozo ya uendeshaji wa
mitambo (capacity charge) iangaliwe upya kwa sababu inaingiza gharama
kubwa kwa Tanesco, hivyo kushindwa kufikia malengo ya kujiendesha badala
yake kuendelea kutegemea serikali kulisaidia.
Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy,
alisema ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini ni kwa Tanesco kuchukua
hatua ya kuinunua mitambo ya umeme inayomilikiwa na kampuni
zinazozalisha umeme na kuiuzia Tanesco kwa bei ya juu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema
Songas inalipwa Sh. bilioni 8.562 za tozo ya uendeshaji, IPTL Sh.
bilioni 4.302 na Aggrecco Sh. bilioni 1.600 kwa mwezi. Mramba alisema
Aggreco imekuwa ikiiuzia Tanesco umeme kwa Dola za Marekani senti 40 na
IPTL senti 23 huku Tanesco ikiuza umeme huo kwa senti Dola za Marekani
26.
NIPASHE
Serikali imesema asilimia tano kati ya
17 inayochangiwa na wahisani wa maendeleo katika bajeti ya mwaka huu
imeathirika kutokana na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300
kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum,
alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam, baada ya mkutano kati ya serikali, wadau na wahisani wa
maendeleo kwa nchi zinazoendelea.
Lengo la mkutano huo ni kufanya
majadiliano ili kufahamu mwenendo mzima wa bajeti ya serikali ulipofikia
na maeneo yanayohitaji kurekebishwa.
Mkuya alisema kutokana na sakata la
Escrow lililojitokeza baada ya bajeti kupitishwa, wameona ipo haja ya
kuangalia upya mfumo mzima na mikakati yao ya utekelezaji wa bajeti hiyo
ili kujua kama bado itaendelea kuwa hai katika utekelezaji wake.
“Katika
hili tumeona upo umuhimu wa kutazama upya makubalianao na misingi yetu
kama imepoteza uhalisia kiutendaji au la ili kujua tutaendeleaje nayo
hata baada ya kujitokeza kwa jambo hili,” Mkuya.
Aliongeza kuwa kutokana na hatua stahiki
na za wazi zilizochukuliwa na serikali, wahisani wameridhika na
wataendelea na utekelezaji wa kuchangia bajeti hiyo kama
walivyokubaliana.
“Si
vyema bajeti ya serikali iathirike kutokana na mambo yanayojitokeza, na
hivi sasa fedha tutakazopata tutazielekeza katika maeneo ya barabara,
maji na nishati kama ilivyopendekezwa,” alisema.
Alisema wiki mbili kuanzia sasa
takribani Dola milioni 44 (zaidi ya Sh. bilioni 50) huku Benki ya Dunia
na Benki ya Maendeleo ya Afrika wakijipanga kutoa Dola millioni 227 (Sh.
bilioni 409).
Alisema nchi zinazoendelea zinakabiliwa
na masharti magumu katika kupewa misaada, hivyo uwapo utaratibu maalum
wa upokeaji wa misaada ili kuepusha kukwama pindi matatizo
yanapojitokeza baada ya makubalinao na wahisani.
NIPASHE
Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kimekanusha tuhuma za kuwahusisha baadhi ya viongozi wake waandamizi
kuwa wanapanga njama za kumdhuru Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, kikisema ni za uongo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema tuhuma hizo ni za kipuuzi na uongo, lakini zisipojibiwa zinaweza kugeuka ajenda.
Alisema ni vizuri Watanzania wakakumbuka
historia ya tuhuma lukuki zilizowahi kutolewa na Dk. Slaa tangu aanze
siasa na zote zilithibitika baadaye kuwa ni za uongo. “Kupanga kumdhuru Dk. Slaa, ili CCM ipate nini kwa kudhurika kwake.
“Kwa
nini CCM ipange kumdhuru, huu ni mwendelezo wa tabia yake ya kuzusha
mambo ya uongo kila anapoona anachuja kisiasa, ni busara kwa umri wake
akatumia muda mwingi kumrudia Mwenyezi Mungu,” Nape.
Alitaja mambo ambayo Dk. Slaa amewahi
kuzusha kuwa ni pamoja na kuwatangazia wananchi wakati wa kampeni za
mwaka 2010, akiwa mkoani Singida kuwa wananchi kwamba lilikamatwa lori
la mizigo lililojazwa karatasi za kura za urais zilizokuwa tayari
amepigiwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
“Katika kuonyesha kwamba alikuwa na
uhakika wa jambo hilo, alisoma hadi namba za lori hilo na tela lake
kutoka kwenye karatasi aliyokuwa ameshika mkononi, kisha akasema kuwa
lori hilo lilikamatwa katika mji mdogo wa Tunduma, mkoa wa Mbeya wakati
likiingia nchini kutoka Lusaka, Zambia, Lakini baada ya polisi kuchukua
hatua za haraka kulikamata, kisha wakalipekua hadharani huku wananchi
wakishuhudia pale pale Tunduma, kilichokutwa ndani ya lori ni shehena ya
vipodozi vya kinamama na sabuni za manukato,” alisema Nape.
Nape aliongeza kuwa, siku chache
baadaye, Dk. Slaa akatangaza kuwa Rais Kikwete alikesha katika hoteli ya
Lakairo, Mwanza akiweka mikakati ya kuiba kura siku ya uchaguzi huo ili
ashinde.
Alitoa mfano mwingine kuwa ni mwaka
2011, akisema Dk. Slaa alimzushia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Yohana Balele, lakini baadaye iligundulika alikuwa mzima.
MTANZANIA
Tuhuma za mauaji ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, zimeendelea kutikisa pembe za nchi huku mlinzi wake binafsi, Khalid Kagenzi, akitoboa siri za mkasa huo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, kudai mlinzi huyo alikuwa akitumiwa na vyombo vya usalama kwa lengo la kumuua Dk. Slaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam, Kagenzi alisema hausiki na mpango huo ila kuna
watu ndani ya Chadema wamekuwa wakimtuhumu bila kutoa uthibitisho wa
madai hayo.
Akiwa amefuatana na mtoto wake wa kiume
katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, alisema taarifa iliyotolewa
Machi 8, mwaka huu kwa waandishi aliiandika yeye kwa kushinikizwa baada
ya kupigwa na kuteswa, huku akitishiwa kuuawa na walinzi wenzake wa
Chadema.
Alisema Machi 7, mwaka huu aliitwa
katika ofisi ya Makao Makuu Chadema ambako aliingizwa katika chumba
kilichokuwa na watu watano aliowatambua kwa majina ambao ni Boniface Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo, Hemedi Sambura, Benson Mramba, na watu wengine wawili aliowataja kwa majina moja moja ya Jumanne na Mamba.
Kagenzi alisema baada ya kuingizwa ndani
ya chumba hicho, aliona begi lililokuwa limehifadhiwa bisibisi, kisu,
bikari na ‘plies’ ambazo walizitumia kumpiga na kumtesa.
“Ndani
ya chumba hicho waliniweka kwenye kona na sikuwa na wasiwasi na
kuniamuru ‘weka vitu vyako hapo’, nikawajibu hawana sheria ya kuniambia
hivyo kama kuna tatizo waniambie.
“Beni
alinyanyuka na kunipiga teke la ubavuni, tena teke la nguvu, sijakaa
sawa akanipiga teke jingine na kunibamiza na mbao alizokuwa amezifunga
mikononi, nikaanguka chini.
MTANZANIA
Wakazi wa Endarasha nchini Kenya
wanaishi kwa shaka kubwa kutokana na nyani na tumbili waliopo katika
hifadhi ya Taifa iliyo jirani na makazi yao kuwanyanyasa wanawake pekee
huku mmoja akivuliwa nguo wakati alipokuwa shambani.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Ester Wangui
ameeleza alichoshuhudia juzi baada ya makundi ya nyani na tumbili
wanakadiriwa kuwa 50 kutoka katika hifadhi hiyo kuvamia katika mashamba
yao kwa wakato mmoja.
Katika tukio hilo mwanamke huyo
alishambuliwa na nyani hao wa kiume ambao walikuwa 10 ambao walikuwa
wakinguruma kwa sauti kubwa huku wakiwa wameshika sehemu zao za siri
huku wakimtisha.
Mwanamke mwingine alishambuliwa na kuvuliwa nguo wakati alipojaribu kuwazuia nyani hao wasivamie shamba lake.
Walisema nyani hao wamekuwa wakiongezeka
katika makazi ya watu kutokana na kupata chakula kingi tofauti na
wakiwa ndani ya hifadhi hiyo.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment