Wednesday, March 11, 2015

YALIYONIKUTA TANGA SEHEMU YA (23)

HADITHI
 
YALIYONIKUTA TANGA (23)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Hata hivyo nilikuwa nikijiuliza bangi ilikuwa inatumikaje katika uganga wakati kilikuwa kilevi kisichokubalika? Sikupata jibu la swali hilo.
 
Yule mtu aliyetumwa bangi hakuchelewa sana akarudi akiwa na bangi yake mkononi. Nikahisi kwamba bangi ilikuwa ikiuzwa sana pale kijijini.
 
Nikakumbuka zamani nilishuhudia kesi ya mvuta bangi mmoja aliyedai kuwa akivuta bangi huwa anapata nguvu ya kulima. Nikajiambia  huenda zilitumika pale kijijini kwa sababu hiyo.
 
Ile bangi ilipoletwa ilichanganywa na vile vitu vingine vilivyoletwa kwanza, yaani ule mchanga wa kaburini na kile kinyesi cha nguruwe.
 
Baada ya vitu hivyo kuchanganywa vilitiwa kwenye chungu na kuwekwa kwenye jiko. Baada ya sekunde chache vilianza kuungua na kutoa moshi. Yule mganga alikuwa ameshika mwiko akivigeuza huku na huku.
 
Vilikuwa vikitoa harufu mbaya iliyokuwa inaumiza kichwa. Mama yangu alipiga chafya mara mbili.
 
“Kama unasikia vibaya toka nje” Mganga huyo akamwambia mama.
 
Mama akatoka nje. Mganga aliendelea kuvichoma vile vitu mpaka vikaungua na kuwa vyeusi. Aliepua kile chungu na kukiweka kando ya jiko.
 
SASA ENDELEA
 
Alisubiri chungu hicho kilipopoa akaanza kuvisaga vile vitu alivyokuwa amevichoma kwa kutumia aina fulani ya jiwe lililokuwa na rangi ya kahawia.
 
Vitu hivyo vilisagwa na kuwa unga unga mweusi ambao aliutoa kwenye chungu hicho na kuutia kwenye karatasi nyeupe. Akaanza kuutabania maneno ya kiganga huku akiugeuza geuza kwa kidole chake.
 
Alipomaliza kuutabania aliuchota kidogo akautia kwenye kile kisanduku akauchnganya changanya na yale mapambo ya dhahabu. Ule unga uliobaki aliufunga kwenye ile karatasi akanipa.
 
“Utakuwa unachota kisdogo na kutia kwenye maji ya kuoga kama ulivyofanya jana. Utaoga asubuhi na jioni kwa siku saba” akaniambia.
 
Ili nipate uhakika wa alichoniagiza nikamuuliza.
 
“Umeniambia niioge hii dawa kidogo dogo kwa siku saba asubuhi na jioni?”
 
“Ndio. Usipitishe hata siku moja”
 
Nikabaki kumtazama yule mganga wakati akiniambia hivyo. Sikumtazama kwa sababu nilikuwa namsikiliza. Nilimtazama kutokana na mawazo yaliyokuwa yakipita akilini mwangu.
 
Nilikuwa nikijiambia, yaani niende nikaoge bangi na mavi ya nguruwe kwa siku saba!
 
Uganga wa kienyeji unahusisha mambo mengi machafu!
 
Licha ya kuona kinyaa, niliona sikuwa na budi kutekeleza vile nilivyoambiwa ili kusalimisha maisha yangu na pia nipate zile dhahabu ambazo nazo zilitiwa ile dawa.
 
“Ukioga dawa hiyo shetani hatakufuata hata siku moja. Atakupitia mbali sana na hizo dhahabu hatazitaka tena kwa sababu zimeshanajisika na wewe mwenyewe pia unapata najisi ukioga dawa hiyo” Mganga aliniambia.
 
“Hata zikipita hizo siku saba hao majini hawatanifuata?” nikamuuliza ili nipate ufafanuzi.
 
“Ukishaioga kwa siku saba, inakuwa ni basi. Hawatakufuata tena”
 
“Sawa, nimekuelewa”
 
Kule kwetu ni mwiko kwa mganga kukwambia nataka kiasi fulani cha pesa isipokuwa mteja mwenyewe ndio unamkadiria kutokana na kazi aliyokufanyia.
 
Nilitoa shilingi elfu ishirini nikampa. Akatuambia kwamba tunaweza kwenda zetu.
 
Tukaondoka.
 
Tuliporudi nyumbani nilikitia kile kisanduku kwenye begi langu kisha nikampa mama begi hilo ili alihifadhi chumbani kwake.
 
Nikaanza kutumia ile dawa. Kila siku nikawa ninaioga mara mbili asubuhi na jioni. Mpaka siku saba zikaisha. Nikakaa kwa mwezi mzima, sikuona tatizo lolote. Nikaamini kwamba ile dawa ilikuwa inafanya kazi.
 
Udadisi ukanifanya nipige simu kwa mpelelezi mwenzangu aliyekuwa Tanga ili anieleze hali ilivyo.
 
“Tuko shwari tu” akaniambia.
 
“Vipi kuhusu wale majini wa barabara nane, polisi bado wanawafuatilia?’
 
“Ule upelelezi ulishaachwa waka hakuna afisa yeyote anayehoji kuhusu kesi ile”
 
“Huenda wameingia uoga”
 
“Sio huenda, wameingia uoga kweli”
 
Baada ya kuelezwa hivyo na kupata picha kamili ya hali iliyokuwa huko Tanga nikapata matumaini kuwa yale matatizo yalikuwa yamekwisha na kwamba ningefaidi zile dhahabu.
 
Siku moja mama yangu alinifuata chumbani na kuniambia kuwa kuna msichana ambaye alitaka nimuoe ili niende naye Tanga. Nikataka kumjua huyo msichana.
 
“Nitatuma mtu jioni amuite, utakuja kumuona” Mama aliniambia.
 
“Sawa”
 
ILipofika jioni mama akaja chumbani mwangu akiwa na msichana mmoja mzuri wa kihaya.
 
Akaniambia kwa kinyumbani.
 
“Nimekuletea mchumba mwanangu”
 
“Ndiye huyu?” nikamuuliza nikiwa nimemtumbulia macho.
 
“Ndiye yeye niliyekwambia asubuhi, ni msichana mpole sana na ana tabia nzuri anafaa kuwa mke wako”
 
Msichana akanipigia goti kisha akanisalimia. Nikafurahi kupewa heshima za kinyumbani. Baada ya kusalimiana naye nilimwambia aketi kwenye kiti, akakaa.
 
“Unaitwa nani?”  nikamuuliza.
 
“Naitwa Mage”
 
“Haya zungumzeni, mimi niko hapa ukumbini” Mama akaniambia na kutoka mle chumbani.
 
“Unaishi na wazazi wako?” nikamuuliza.
 
“Ndiyo naishi na wazazi wangu”
 
“Umesoma hadi darasa la ngapi”
 
“Nimekomea kidato cha nne”
 
“Mwaka gani?”
 
“Mwaka juzi”
 
“Mama yangu amekupenda, kwa hiyo uko tayari tufunge uchumba?”
 
“Kama na wewe umenipenda”
 
“Kusema ukweli alichokipenda mama yangu na mimi nitakipenda tu”
 
“Wewe unafanya kazi gani?”
 
“Mimi ni polisi upande wa upelelezi”
 
“Unafanya kazi mkoa gani”
 
“Kwa sasa nimehamishiwa Tanga”
 
“Kwa hiyo ukishanioa tutakwenda kuishi Tanga?”
 
“Ndiyo”
 
“Sawa. Sasa uje ujitokeze kwa wazazi wangu”
 
“Nitafanya hivyo katika siku chache zijazo”
 
Baada ya kuzungumza na Mage, msichana niliyechaguliwa na mama yangu na ambaye mimi mwenyewe pia nilimpenda nilimuita mama nikamwambia kuwa nimeshazungumza naye.
 
“Mmeshakubaliana”
 
“Ndiyo, tumekubaliana”
 
“Basi ngoja nimsindikize arudi kwao”
 
Mama akatoka na yule msichana.
 
Je nini kitaendelea? Usikose kuendelea na hadithi hii katika toleo lijalo kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment