Saturday, March 14, 2015

YALIYONIKUTA TANGA SEHEMU YA (25)

HADITHI
 
YALIYONIKUTA TANGA (25)
 
ILIPOISHIA
 
Usiku ule ulikuwa balaa! Hatukulala. Mke wangu alikuwa akipiga kelele usiku kucha akidai kuwa kila alipofumba macho alikuwa akiona msichana anampiga bakora akimwambia avue zile dhahabu alizovaa.
 
Mwisho wake ilibidi mke wangu atii na kavua zile dhahabu nilizokuwa nimempa na hapo ndipo alipopata usingizi.
 
Kulipokucha asubuhi nilikichukua kile kisanduku nikakitia kwenye begi na kumpa polisi aliyekuwa jirani yangu.
 
“Tafadhali nihifadhie hili begi langu nitalichukua kesho” nikamwambia.
 
Kwa vile yule polisi alikuwa rafiki yangu akalichukua begi hilo na kunihifadhia chumbani kwake. Nikaenda zangu kazini.
 
Niliporudi kutoka kazini mke wangu akaniuliza maswali mengi kuhusu zile dhahabu nilizokuwa nimempa ambazo zilikuwa zimemtia wasiwasi mkubwa.
 
Nikamdanganya kwamba dhahabu hizo nilizinunua kwa sonara na kwamba nilishazirudisha.
 
“Sasa kwanini nilikuwa naota ile ndoto ya kuchapwa?” akaniuliza.
 
“Sijajua lakini nimemueleza sonara huyo ameniambia alikosea akaniuzia dhahabu za majini lakini kwa vile nimezirudisha hakutakuwa na tatizo.” Nikaendelea kumdanganya ili kumtoa wasiwasi.
 
SASA ENDELEA
 
Nilidhani kwa kuhamisha kile kisanduku kwa mwenzangu ndio ningemaliza yale matatizo ya majini lakini nilikuwa nimejidanganya.
 
Yapata saa nane usiku wakati nimelala, yule polisi niliyempa lile begi lenye kisanduku anihifadhie alinibishia mlango.
 
Nilipofungua mlango nilimuona amesimama mbele ya mlango akiwa na lile begi mkononi.
 
“Chukua hili begi lako, linaniletea miujiza chumbani kwangu” akaniambia huku uso wake ukiwa umetaharuki.
 
“Miujiza gani tena?”
 
“Kuna joka linatoka ndani ya hili begi halafu linazunguka chumbani kwangu”
 
Nikajifanya nashangaa.
 
“Joka?”
 
“Ndio joka. Tena joka kubwa sana. Linazunguka chummbani kisha linarudi kwenye hili begi linapotea”
 
“Mh! Unanieleza habari ya ajabu sana”
 
“Kwani umeweka nini humu ndani”
 
“Sijui kilichomo humo ndani. Hilo begi alilisahau mtu mmoja aliyekuja hapa nyumba kuomba maji ya kunywa” nikamdanganya.
 
“Mh! Basi lichukue. Siwezi kuliweka kwangu”
 
Nikalichukua lile begi. Yule polisi akarudi nyumbani kwake. Na mimi nikapatwa na kizungumkuti. Nilikuwa sijui nikaliweke wapi. Yale maelezo ya polisi mwenzangu yalinitisha.
 
Nilipoona nimekosa pa kuliweka nililiweka chini ya meza pale sebuleni. Nikafunga mlango wa chumbani ili kama kuna joka linalotoka lisiingie chumbani mwetu.
 
Wakati ule mke wangu alikuwa amelala. Hakuwa akijua kilichokuwa kinaendelea. Nilishukuru kwa hilo. Laiti angekuwa macho akasikia yale niliyokuwa nikiyazungumza na yule polisi, ingekuwa taabu.
 
Wakati nimejilaza kitandani nikiwaza, nilijiambia kuwa ule uganga niliofanyiwa na yule mganga wa kijijini kwetu haukufaa kitu, sasa vituko vilikuwa vinanijia nyumbani kiasi kwamba mimi mwenyewe nilikuwa nimeshapata uoga na nilikuwa sijui la kufanya.
 
Nikajiambia tamaa yangu ya kumiliki zile dhahabu sasa inaniponza.
 
Wakati niko kwenye lindi la mawazo nikapitiwa na usingizi ghafla, nikaota nimeamka saa kumi na mbili asubuhi, nikatoka na lile begi na kwenda kule magomeni kwenye yale mkaburi. Nilipofika nikakitoa kile kisanduku na kukiweka juu ya kaburi mojawapo. Hapo hapo nikaona kinatitia chini na kupotea kabisa.
 
Baada ya hapo nilizinduka usingizini nikatazama saa na kuona ilikuwa saa kumi na mbili kasorobo, nikavaa nguo na kutoka chumbani. Nilikwenda kuosha uso na kusukutua maji. Nikalichukua lile begi na kutoka nalo bila hata kumuaga mke wangu.
 
Nilikwenda kupanda daladala nikaenda Magomeni. Nilifika kule makaburini nikakitoa kile kisanduku na kukiweka juu ya kaburi kama vile nilivyoota usiku. Hapo hapo nikaona kile kisanduku kinazama chini.
 
Kilizama hadi kikapotea kabisa.
 
Nilitishika sana lakini kwa vile tukio lenyewe nilishaliota nilijikaza.
 
Kile kisanduku kilipopotea, nikajua kimerudi kwa wenyewe. Nikaondoka na kurudi nyumbani. Nilipofika nilimkuta mke wangu bado amelala. Nikaenda kuoga. Wakati narudi kutoka kuoga nikamkuta ameshaamka. Sikumwambia chochote.
 
Baada ya siku ile sikuona tena vile vituko vya majini. Tukio hilo licha ya kunitesa lilinipa fundisho ambalo sitalisahau. Nikawa polisi muadilifu sana niliyefanya kazi yangu kwa misingi ya haki na sheria na sio kama nilivyokuwa hapo mwanzo.
 
Hayo ndiyo yaliyonikuta tanga’ usiache kunitumia maoni yako juu ya hadithi kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
 
 

No comments:

Post a Comment