TAARIFA YA ZADIA KUHUSU KUFUTWA KWA MATOKEO YA UCHAGUZI ZANZIBAR.
Jumuiya ya Wazanzibari Waishio
Nchini Marekani (ZADIA), imekuwa ikifuatilia kwa karibu na makini zaidi
zoezi zima la Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kwa kiasi kikubwa mchakato wa uchaguzi ulifanyika kwa njia za amani na
utulivu. Hata hivyo ZADIA imeshtushwa mno na tamko la Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Mh. Jecha Salim Jecha la kutangaza kuufuta
Uchaguzi Mkuu Zanzibar na matokeo yake.
Ama kwa hakika kitendo hicho
hakikuwa cha busara na kinapelekea kurudisha nyuma maendeleao ya
demokrasia Zanzibar, na vilevile hakiashirii mustakbali mwema kwa nchi
yetu tuipendayo. Wazanzibari wameelezea maoni na matakwa yao kwenye
visanduku vya kupigia kura, na maoni na matakwa yao hayo yanapaswa
kusikilizwa na kuheshimiwa.
Kwa hivyo, ZADIA inatoa wito
kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar, kumalizia mchakato mzima wa
kuhesabu kura kwa majimbo yaliyobakia na kutoa matokeo ya mwisho ya
Uchaguzi na kumtangaza mshindi ili kuiepusha Zanzibar yetu tuipendayo
kuingia katika hali ya mtafaruku na mifarakano isiyokuwa na tija bali
kuleta hasara.
ZADIA pia inaungana na jumuiya
zote za kimataifa ambazo zimetoa msimamo wao juu ya uchaguzi wa
Zanzibar, hasa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, ambao ni kiungo
madhubuti kati ya Wazanzibari walioko Zanzibar na wenzao wanaoishi
nchini Marekani.
Chanzo Full Shangwe
No comments:
Post a Comment