HADITHI
YALIYONIKUTA
TANGA (11)
ILIPOISHIA
TOLEO LILILOPITA
Maimuna
alikuwa ameshika ule upanga wake akiangaza macho yake huku na huku. Sikuweza
tena kusubiri, nikatoka mbio. Nilielekea upande ule lilikoelekea gari la
polisi.
Wakaniona!
“Si yule!”
niliisikia sauti ya Maimuna.
“Twende
tumfuate” Sauti ya kiume nayo ikasikika.
Niliendelea
kukimbia. Kila nilipopiga hatua tatu nilitazama nyuma. Niliwaona wananifuata.
Hawakuwa wakikimbia lakini walikuwa wanakuja kwa haraka.
Kwa mbali
nikaona mwanga wa gari linalokuja. Nikazidi kukimbia. Niliona nikimbie nikiwa
katikati ya barabara ili watu waliomo ndani ya gari hilo waweze kuniona.
Nikajitokeza katikati ya barabara huku taa za gari zikinimulika.
Haikutosha
kujitokeza katikati ya barabara. Niliinua mikono yangu miwili nikawa nalipungia
gari hilo ili kulisimamisha. Niliomba gari hilo liwe la polisi lililonipita.
Kama halitakuwa gari la polisi halitasimama. Litanikwepa na kuendelea na safari
yake.
“Jamani
simameni, nakufa.. jamani simameni nakufa!” nilikuwa nikipiga kelele.
Nyuma yangu
Maimuna na mwenzake walikuwa wakiendelea kunifuata bila kujali kama kulikuwa na
gari linakuja.
Sikuwa na
hakika kama gari hilo lilikuwa la polisi. Na kama lilikuwa na polisi sikuwa na hakika
kama wangeweza kupambana na majini hao waliokuwa na hasira na mimi.
SASA ENDELEA
Gari hilo
lilipunguza mwendo na kusimama katikati ya barabara. Kama lingeendelea kuja
lingenigonga kwa vile na mimi nilikuwa katikati ya barabara.
Taa za gari
hilo zilikuwa zikinimulika. Mpaka muda huo sikujua gari hilo lilikuwa la nani.
Mara tu liliposimama, niliona polisi wakishuka haraka haraka. Walikuwa polisi
sita waliokuwa na bunduki. Hapo nikajua kuwa lilikuwa gari la polisi ambalo
lilinipita mara ya kwanza.
Walikuwa
wameshanitambua wakanifuata haraka haraka.
“Kitu gani
Martin?” Polisi mmoja aliyekuwa na cheo cha Koplo akaniuliza.
“Nikageuka
nyuma ili niwaoneshe wale majini. Nilishaanza kuwambia.
“Wale majini
bado wananifuata…”
Lakini
nilisita nilipoona wale majini hawapo. Walitoweka ghfla nyuma yangu.
“Kitu gani
Martin?” Polisi huyo aliniuliza tena baada ya kutonielewa.
Sasa
nikawaeleza kwa utulivu mkasa mzima.
“Sasa wako
wapi hao majini?” Polisi mwingine akaniuliza.
“Wametoweka
sasa hivi”
“Una hakika
kwamba Sajenti Erick amechinjwa na umekiona kichwa chake kiko mbali na mwili
wake?” yule koplo wa polisi akaniuliza.
“Nimekiona
kichwa chake kiko ndani ya boksi na mwili wake unaning’inia juu”
“Ni sehemu
gani?”
“Sehemu
yenyewe mmeipita, ni pale mbele kwenye mbuyu”
Niliwaonesha
kwa kidole.
“Ingia
kwenye gari twende”
Nilikuwa wa
kwanza kujipakia kwenye gari. Nilikaa kwenye siti iliyokuwa kando ya dereva.
Mwili wote ulikuwa umenijaa baridi ya hofu. Baada ya polisi hao kujipakia, gari
likaondoka. Tulipokuwa tunaukaribia ule mbuyu, polisi aliyekuwa akiendesha
aliniuliza.
“Ni mbuyu
ule pale?”
“Ndio ule
pale. Kuna njia upande wa kushoto”
Tulipofika
katika eneo lililokuwa na mbuyu huo, dereva alikata kushoto. Tukaingia kwenye
vichaka.
“Ni kwa
upande gani?”
“Twende tu.
Huko mbele kuna njia inaelekea kulia”
Tulipoifikia
njia hiyo inayoelekea kulia, dereva akaniuliza.
“Njia
yenyewe ndio hii?”
“Ndiyo hii,
sasa kata kulia. Tutaiona hiyo nyumba”
Dereva
akakata kulia.
“Huku
ulifikaje wewe?” Dereva huyo akaniuliza.
“Ni
ushawishi tu wa yule msichana” nikamjibu.
“Huoni kama
kunatisha?”
Nikaguna na
kunyamaza kimya. Muda ule ndio niliona kunatisha. Wakati ule namfuata yule
msichana sikuona kama kunatisha kiasi kile.
“Yaani
sajenti Erick ni marehemu?” polisi aliyekuwa akiendesha gari hilo alikuwa bado
haamini niliyowaeleza.
“We twende,
utakwenda ona mwenyewe”
Baada ya
mwendo mfupi tukaiona ile nyumba mbele yetu.
“Nyumba
yenyewe ni ile pale” nikamwambia polisi aliyekuwa akiendesha.
Akalisimamisha
gari mbele ya nyumba hiyo. Tukashuka. Koplo wa polisi aliishika vyema bunduki
yake akaenda kubisha mlango. LIcha ya kubisha kwa sekunde kadhaa hakukuwa na
majibu. Akaupiga teke mlango huo ambao ulifunguka.
Mlango
ulipofunguka aliwaashiria polisi wengine wamfuate. Sote tukaingia ndani. Kila
polisi alikuwa ameielekeza mbele bunduki yake tayari kukabiliana na tukio
lolote litakalotokea.
Kwa kutumia
mwanga ule wa fanusi ambayo bado ilikuwa inawaka tuliangaza macho kila upande.
Ile sebule ilikuwa tupu. Tukaingia ndani zaidi.
Nilimuonesha
koplo wa polisi kile chumba kilichokuwa na kichwa cha Sajenti Erick pamoja na
mwili wake. Kabla ya kuingia koplo huyo aliwaashiria polisi wawili kwenda uani
na kumuweka chini ya ulinzi yeyote watakayemuona.
Aliwambia
polisi wengine waingie katika vumba vingine kwa wakati mmoja. Ndipo mimi na
yeye tulipoingia katika kile chumba. Polisi mmoja alikuwa amebaki ukumbini kmwa
ajili ya kuweka ulinzi.
Tulipoingia
humo chumbani niliutazama ule mwili uliokuwa ukining’inia, haukuwepo.
Nikalisogelea lile boksi lililokuwa nyuma ya mlango na kulitazama ndani. Kile
kichwa hakikuwemo isipokuwa damu iliyokuwa ikivuja kutoka kwenye kichwa hicho ndio
iliyosambaa ndani ya boksi.
“Kichwa
chenyewe kilikuwa humu lakini kimeondolewa” nikamwambia koplo huyo.
“Una maana
hii damu ilitoka kwenye kichwa hicho”
“Ndiyo.
Kilikuwa kinavuja damu”
“Na ule
mwili uliosema ulikuwa unaning’inia uko wapi?”
“Ulikuwa
uking’inia hapa”
Nikamuonesha
pale mahali ambapo chini yake palikuwa na matone ya damu.
“Ulikuwa
unadoda damu, hii hapa chini”
“Ina maana
wameuondoa?” Koplo akaniuliza. Uso wake ulikuwa umeshabadilika rangi kwa
taharuki.
“Wameuondoa
au wameuzika, kwa sababu yule bibi alikuwa akichimba kaburi uani”
“Hebu twende
na huko”
Koplo
alitangulia kutoka. Mimi niliyachukua yale magazeti yaliyokuwa yamewekwa
pembeni mwa chumba kisha nikatoka.
Polisi wote
tukakutana tena hapo ukumbini.
“Mmekuta
nini?” Polisi mmoja aktuuliza.
“Kuna damu
tu” Koplo alimjibu.
Je nini
kitatokea? Endelea kufuatilia hapo kesho
Toa maoni yako kupitia blog hii
No comments:
Post a Comment