Friday, February 6, 2015

YALIYONIKUTA TANGA (12)

HADITHI
 
YALIYONIKUTA TANGA (12)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
“Mwili na kichwa vimeondolewa. Nafikiri vimezikwa uani” nikaongezea maelezo.
 
“Tumekuta makaburi uani!” Polisi mwingine akasema.
 
“”Kwenye hivi vyumba vingine hamkukuta watu?” Koplo akauliza.
 
“Hakuna mtu humu ndani. Hii nyumba iko tupu”
 
“Hebu twendeni tukayaone hayo makaburi”
 
Tukaenda uani. Lile kaburi nililoliona likichimbwa na yule mwanamke lilikuwa limefukiwa. Pembeni yake kulichimbwa kaburi jingine lililokuwa wazi. Shepe lilikuwa limeachwa kwenye chuguu ya mchanga.
 
“Hili kaburi lililofukiwa ndilo nililokuta linachimbwa. Bila shaka mwili wa Sajenti Erick umezikwa hapa” nikawambia wenzangu.
 
“Tulifukue tuone ndani” Koplo akasema.
 
Lilikuwa wazo zuri.
 
“Lakini tusitumie hili shepe. Tutaharibu alama za vidole za aliyekuwa amelishika” Koplo akatukumbusha.
 
“Tunaweza kulifukua hata kwa mikono. Mchanga wenyewe bado uko laini” nikawambia.
 
Bila kujua hatari ambayo ilikuwa inatukabili, tulianza kulifukua kaburi hilo kwa mikono.
 
SASA ENDELEA
 
Polisi watano nikiwemo na mimi tuliendelea kulifukua kaburi hilo kwa mikono. Koplo wetu alikuwa amesimama na bunduki kuweka ulinzi. Tulilifukua kaburi hilo hadi likawa shimo, tukaingia ndani na kuendelea kufukua.
 
Wakati tukiendelea kufukua huku tukimwaga mchanga kwa juu niliona kiatu cheusi, nikakishika na kukivuta. Nikaona nimevuta mguu.
 
“Jamani nimeshika mguu!” nikawambia wenzangu.
 
“Ni kweli hapa pamezikwa mtu, hebu tufukue zaidi” Polisi mmoja akatuambia.
 
Tukaendelea kufukua na hatimaye kuupata mwili kamili usio na kichwa. Mara moja niligundua kuwa mwili huo ulikuwa wa Sajenti Erick na ndio ule uliokuwa ukining’inia kule chumbani..
 
“Huu hapa mwili wa Sajenti Erick” nikawambia wenzangu ambao walikuwa wameshituka na kushikwa na mshangao.
 
“Kichwa chake kiko wapi?” Koplo akauliza.
 
“Kichwa hakipo, nadhani hawakukizika lakini nilikiona kwenye lile boksi” nikasema.
 
“Sasa tutauthibitishaje kuwa ni mwili wa Erick?” Koplo akauliza.
 
“Lakini unaonekana ni mwili wake kweli, hili shati ndilo alilokuwa amevaa jana” Polisi mmoja akasema.
 
“Utoeni, tuuangalie vizuri” Koplo akatuambia.
 
Tukaubeba na kuuweka juu ya kaburi.
 
Koplo akautazama na kutuambia.
 
“Hata mimi naona ni Sajenti Erick, hivi viatu ni vya kipolisi. Ngoja nimfahamishe Inspekta aliyeko kwenye zamu”
 
Kiplo alitoa simu akampigia Inspekta aliyekuwa ameshika zamu ya usiku ya kuongoza kituo.
 
“Afande tumefika hapa mahali, tumeonana na Martin na tumeukuta mwili wa Sajenti Erick umezikwa lakini hauna kichwa” Koplo huyo akazungumza kwenye simu baada ya simu yake kupokelewa.
 
“Hilo kaburi alilozikiwa liko wapi?” Sauti kutoka upande wa pili wa simu ikamuuliza.
 
“Liko uani mwa hii nyumba tulioingia”
 
“Mmekamata watu wangapi humo ndani?”
 
“Hatukukuta mtu yeyote”
 
Wakati Koplo huyo akisema hivyo tulisikia mlango wa mbele wa nyumba hiyo ukifunguliwa. Tukamuona yule mwanamke na binti yake Maimuna pamoja na yule jini mwanaume wakiingia. Maimuna na yule jini mwanaume walikuwa wameshika mapanga.
 
Polisi wote waliokuwa hapo walishituka. Walishituka si kwa sababu tu ya kuwaona viumbe hao, bali walishituka kwa kuona maumbile waliyokuwa nayo. Walikuwa na maumbile ya kijini huku miguu yao ikiwa na kwato nyeusi kama kwato za punda!
 
Koplo aliyekuwa akiongea kwenye simu alikatiza mazungumzo yake akaitia simu mfukoni na kuinua bunduki. Polisi wengine pia waliinua bunduki zao kuwaelekezea majini hao.
 
“Majini wenyewe ndio hao wanaokuja” nikawambia polisi hao kwa mshituko. Kwa vile nilikuwa nyuma nilisimama pale pale nilipokuwa ili nijikinge kwa wenzangu waliokuwa na bunduki.
 
“Simameni hapo hapo!” Koplo aliwambia majini hao kwa sauti ya amri.
 
Moyo ulikuwa ukinienda mbio. Kwanza sikuziamini bunduki hizo za polisi kama zingeweza kuwatiisha majini hao lakini kwa vile tulikuwa wengi nilipata matumaini kidogo.
 
Majini hao hawakusimama, waliendelea kuja uani kama vile hawakusikia walichoambiwa.
 
“Nimewambia simameni hapo hapo!” Koplo aliwaamuru tena akiwa amewaelekezea bunduki.
 
“Afande tuwababue risasi kama hawasikii” Polisi mmoja akamwambia koplo huyo kama kuwatisha majini hao.
 
“Nyinyi ni kina nani?” Maimuna akauliza kwa sauti ya ukali huku akiwatangulia wenzake.
 
“Sisi ni polisi” Koplo alimjibu.
 
Walikuwa wameshafika kwenye mlango wa uani. Sasa walikuwa wanavuka kizingiti ili watoke uani. Koplo akafyatua risasi juu.
 
“Mtakufa nyote, simameni na tupeni mapanga yenu!” akawambia kwa sauti kali.
 
Yule mwanamke aliinua mkono na kufanya kama anampiga kibao koplo huyo lakini akiwa yuko mbali naye. Hapo hapo koplo aliachia bunduki akaanguka chini. Hakuinuka tena. Mwanamke huyo akageukia upande wetu akafanya vile vile kwa polisi mwingine ambaye naye alianguka.
 
Akaendelea kufanya hivyo hivyo kwa kila polisi. Wote walianguka na kila aliyeanguka hakuinuka tena. Mimi nilikuwa wa mwisho. Alinipitishia mkono kama ananipiga kibao nikaona kama dunia inazunguka. Macho yangu yakafunga kiza. Nikaanguka hapo hapo na kupoteza fahamu.
 
Nilipokuja kuzinduka kulikuwa kumekucha. Kwanza nilianza kuona miale ya jua ikipiga kwenye macho yangu. Nikayafumba kisha nikayafumbua tena. Nilikuwa nikijiuliza niko wapi. Sikuweza kuelewa mara moja. Pia macho yangu hayakuweza kuona sawa sawa kutokana na miale ya jua iliyokuwa ikinipiga usoni.
 
Nikatulia na kuwaza. Nikakumbuka kilichotokea. Nikainuka kwa haraka na kuketi. Nilikuwa nimelala kwenye tuta la mchanga wa kaburi mahali palepale nilipoanguka. Niliwaona polisi wenzangu waliokuwa wamelala kama nilivyokuwa nimelala mimi. Kila mmoja alikuwa sehemu yake, bunduki yake ikiwa pembeni.
 
Wakati ule nainuka, polisi hao nao walianza kuinuka mmoja mmoja. Walikuwa wamezinduka kama mimi baada ya kupotewa na fahamu kwa muda ambao hatukuujua.
 
Jambo la ajabu tuliloliona ni kuwa ile nyumba ya Maimuna haikuwepo tena. Eneo lote lilikuwa makaburi matupu. Lile kaburi la Sajenti Erick ambalo tulilifukua lilikuwepo na mwili wake ulikuwa juu ya kaburi hilo kama tulivyouweka.
 
Gari la polisi tulilokwenda nalo mahali hapo lilikuwepo. Pia kulikuwa na gari jingine lililokwenda na polisi wengine. Polisi hao tuliwaona wamesimama wakitutazama.
 
Kila mmoja wetu aliyeinuka alikuwa akishangaa. Alishangaa kwa jinsi tulivyokuwa tumepotewa na fahamu na alishangaa kuona ile nyumba haikuwepo tena na badala yake kulikuwa na makaburi matupu.
 
“Vipi?” Inspekta Amour ambaye alikuwa mmoja wa polisi waliofika alituuliza kwa mshangao.
 
Je nini kitatokea? Usikose kuendelea na hadithi hii hapo kesho.

No comments:

Post a Comment