HADITHI
YALIYONIKUTA
TANGA (9)
ILIPOISHIA
TOLEO LILILOPITA
“Leo
nimekwisha!” nikajiambia. Nilikuwa sina pa kukimbilia. Lakini nilikwishatambua
kila kitu.
Sikujua
niliwezaje kuwasiliana na yule msichana hadi nikafika katika nyumba ile ya
mauti! Kusema kweli nilijipeleka mwenyewe!
Kwa vyovyote
vile, nilijiambia, nyumba ile haikuwa ya binaadamu wa kawaida. Yule bibi
alikuwa jini! Na kama alikuwa jini, niliendelea kujiambia, sitaweza kunusurika
mle ndani.
Licha ya
kutoka pale uani, yule bibi hakushituka. Aliendelea kuchimba lile shimo kwa
bidii.
Hakuna
binaadamu yeyote anayekubali kufa kirahisi, nikageuka haraka na kurudi
nilikotoka. Wakati nafika kwenye mlango wa mbele, mlango huo ulikuwa
unafunguliwa. Nilijificha nyuma ya mlango. Akaingia yule msichana.
Na yeye
alikuwa uchi na alikuwa na umbile sawa na lile la mama yake. Alikuwa amejaa
manyoya mwili mzima na miguu yake ilikuwa ya kwato nyeusi. Mkononi alikuwa
ameshika upanga.
Mwenzake
alikuwa mwanaume. Na yeye alikuwa kama walivyokuwa wenzake. Hapo nikagundua
kuwa yule mama na binti yake waliokuwa wakiuza vitu vya dhahabu, walikuwa ni
majini lakini watu hawakuwa wakijua.
SASA ENDELEA
Ule upanga
aliokuwa ameushika Maimuna ulikuwa wa nini? Nikajiuliza.
Lakini jibu
lilikuwa wazi kuwa upanga huo ulikuwa ni kwa ajili ya kuchinja kichwa changu.
Bila shaka ndio uliotumika kumchinja Sajenti Erick.
Usiku huo
ulikuwa wa balaa kwangu. Nilijuta kulaimisha mawasiliano na yule msichana hadi
yakanikuta yaliyonikuta. Lakini nilihisi kukutana tena na majini hao ilikuwa ni
mipango yao ya kutukomoa kama walivyomkomoa Sajenti Erick kutokana na ile
dhambi tuliyowafanyia.
Kosa langu
ni kuwa nilijiingiza kichwa kichwa mara tu Maimuna aliponitumia meseji
aliyodai kuwa haikuwa yangu bali alikosea namba. Ilikuwa tamaa yangu ya
wasichana iliyopelekea nifike mahali hapo pa mauti.
Maimuna na
mwenzake walipoingia hawakuufunga ule mlango wa nje. Kama wangeufunga
wangeniona.
“Yuko wapi?”
Maimuna akauliza alipoona sikuwepo mahali ambapo nilikuwa nimelala. Akakimbilia
uani. Mwenzake aliyekuwa naye akamfuata.
Hapo ndipo
nilipopata upenyo wa kutoka. Nilipotoka nje nilianza kukimbia. Jambo
lililonishangaza ni kuwa nilijiona niko kwenye msitu wa kutisha. Nilikuwa
najikimbilia ovyo bila kujua nilikuwa ninakwenda wapi.
Nikatoa simu
yangu mfukoni na kuwapigia polisi wenzangu ili nipate msaada. Wakati napiga
simu nilikuwa nakimbia. Simu ilipokelewa. Aliyepokea alikuwa mwanamke.
Nikamwambia.
“Mimi ni
Martin Lazaro wa CID nimepatwa na matatizo, naomba msaada wenu”
“Mimi ni
Maimuna. Uko wapi Martin, nakutafuta?” Sauti ikaniuliza kutoka simu ya upande
wa pili. Mara moja niliitambua sauti ya Maimuna.
Nikaikata
simu haraka kwa kuona nilikuwa nimekosea namba na kumpigia yule msichana muuaji
niliyekuwa namkimbia.
Nikasimama
na kuiangalia kwa makini namba ya polisi kisha nikaipiga. Nilikuwa nimesimama.
Moyo ulikuwa ukinienda mbio na nilikuwa nahema kama niliyekuwa nafukuzwa.
Simu
ikapokelewa tena. Kabla ya kusema chochote nikaisikia tena sauti ya Maimuna
ikiniuliza.
“Uko wapi?”
Moyo
ukanilipuka kwa hofu. Nikaitazama ile namba. Nikaona ni namba ya polisi lakini
aliyepokea alikuwa Maimuna. Nikaamini kuwa wale walikuwa majini kweli.
Nikakata
simu na kuendelea kukimbia. Simu ikawa inapigwa. Nikasimama na kutazama namba
iliyokuwa inapiga, nikaona namba ya polisi.
Nikaipokea
haraka.
“Jamani nina
matatizo, nikipiga simu inakwenda kwingine…”
“Inakwenda
wapi?” Sauti iliyoniuliza ilikuwa ya Maimuna.
“Wewe nani?”
nikamuuliza kwa kutaharuki.
“Mimi
Maimuna umenisahau mara moja hii, wakati tulikuwa wote hapa nyumbani…”
Nikakata ile
simu na kuendelea kukimbia. Kutahamaki nikajiona nimetokea mbele ya ile nyumba
ya Maimuna.
Nilikuwa
nakimbia lakini nilipiga breki ya ghafla, nikaitazama ile nyumba iliyokuwa
mbele yangu. Nilihakikisha kuwa ilikuwa ndio ile ile nyumba ya Maimuna na
mahali palikuwa pale pale. Kwa maneno mengine ni kwamba nilikuwa nimerudi hapo
hapo.
Mlango
ulikuwa umefungwa, nikaona unafunguliwa. Sikujua nani angetoka, nikageuka na
kuanza tena kukimbia. Sasa nilikuwa kama mwendawazimu niliyekuwa nikijikimbilia
ovyo.
Wakati
ninakuja katika eneo lile hakukuwa na msitu. Kulikuwa na vichaka tu na miti
michache ya mikoroshi. Sasa niliona ajabu kuona msitu wa kutisha. Sikuweza
kujua jinsi msitu huo ulivyotokea.
Simu yangu
ilkuwa inaita lakini sikushughulika nayo tena, niliendelea kukimbia tu. Nia
yangu ilkuwa kutokea katika barabara au njia ya watembea kwa miguu lakini
sikuona njia wala barabara.
Ghafla
niliona nyumba kwa mbali. Ilikuwa inawaka taa kwa nje, nikakimbilia kwenye
nyumba hiyo ili kuomba msaada. Nilipofika niligonga mlango.
“Jamani
naomba msaada…jamani naomba msaada” nikasema huku nikiendelea kugonga.
Baada ya
muda kidogo mlango ukafunguliwa.
“Karibu”
Bibi mmoja aliyekuwa amejitanda shuka nyeupe akanikaribisha.
Nikamueleza
ule mkasa ulionifika. Nilipomaliza kumueleza akapandisha juu gauni lake na
kuniuliza.
“Hao watu
unaosema wana kwato, kwato zao ni kama hizi?” alinionesha miguu yake.
Nilipoitazama
nikaiona ina kwato kama zile za kina Maimuna! Nikashituka na kumtazama yule
bibi usoni. Sasa nikamuona vizuri. Alikuwa ndiye yule aliyekuwa akichimba
kaburi kule uani kwa Maimuna.
“Eh!
Amefikaje huku!” nikajiuliza kabla ya kugeuka nyuma na kuanza tena kukimbia.
“Mbona unakimbia?”
akaniuliza.
Sikumjibu,
niliendelea kukimbia.
“We kijana
hebu njoo…” Yule bibi alinipigia kelele.
Nikageka na
kumtazama. Alikuwa ametoka nje akiniangalia. Nikajipoteza kwenye msitu.
Nilikuwa nimechoka na moyo ulikuwa ukinienda mbio sana. Nilijua kuwa wakati
wowote ningeweza kuanguka na kuzimia.
Kitisho
nilichokipata kilikuwa kikubwa na kiliutikisa moyo wangu hasa. Sikuwa mtu wa
kuamini mashetani lakini siku ile niliamini kuwa mashetani wapo na wanatisha.
Licha ya kujitahidi kukimbia muda wote nilijua kuwa nitakufa kwani sikuwa na
ujanja wa kutoka kwenye msitu huo. Ile hofu peke yake ingweza kuniua.
Hapo
nikaanza kumlaumu Sajenti Erick kwani yeye ndiye aliuleta mpango ule wa kwenda
kumkamata yule bibi na kumbambikia kesi ya madawa ya kulevya.
Usiache kutembelea blog hii kila wakati kwa mambo mazuri na matamu kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment