Thursday, March 12, 2015

HADITHI YALIYONIKUTA TANGA SEHEMU (24)

HADITHI
 
YALIYONIKUTA TANGA (24)
 
ILIPOISHIA
 
“Wewe unafanya kazi gani?”
 
“Mimi ni polisi upande wa upelelezi”
 
“Unafanya kazi mkoa gani”
 
“Kwa sasa nimehamishiwa Tanga”
 
“Kwa hiyo ukishanioa tutakwenda kuishi Tanga?”
 
“Ndiyo”
 
“Sawa. Sasa uje ujitokeze kwa wazazi wangu”
 
“Nitafanya hivyo katika siku chache zijazo”
 
Baada ya kuzungumza na Mage, msichana niliyechaguliwa na mama yangu na ambaye mimi mwenyewe pia nilimpenda nilimuita mama nikamwambia kuwa nimeshazungumza naye.
 
“Mmeshakubaliana”
 
“Ndiyo, tumekubaliana”
 
“Basi ngoja nimsindikize arudi kwao”
 
Mama akatoka na yule msichana.
 
SASA ENDELEA
 
Aliporudi aliniuliza kama nimempenda yule msichana.
 
“Nimempenda” nikamjibu.
 
“Sasa una mawazo gani ya kumuoa?”
 
“Nilikuwa sijapanga kuoa kwa sasa…”
 
“Nimekuonesha yule msichana ili kukutia mawazo ya kuoa. Umeshafikia umri wa kuwa na mke”
 
“Ni kweli, kwa hiyo mama unanishauri nimuoe yule msichana”
 
“Tena tuwaozeshe haraka iwezekanavyo, ukimaliza likizo yako uondoke na mke wako”
 
“Itawezekana mama?”
 
“Kwanini isiwezekane. Harusi za vijijini usizifananishe na harusi za mijini”
 
“Sasa la muhimu ni kupeleke barua ya uchumba kwa wazazi wake tusikie watatujibu nini”
 
“Kama msichana mwenyewe amekubali na wazazi wake watakubali tu. Hilo halina tatizo.
 
Niliandika barua ya uchumba siku ile ile baada ya mama kunitia mawazo ya kuoa. Barua ilipelekwa na siku ya pili yake majibu  yakarudishwa.
 
Nilifurahi kwa kukubaliwa uchumba wangu na Mage. Nilitajiwa mahari iliyokuwa inatakiwa pamoja na ada nyinginezo kwa mujibu wa mila zetu.
 
Siku ile tulikaa kikao cha ndugu tukaijadili ile barua na kukubaliana na kila kilichoandikwa. Baada ya siku tatu nilipeleka mahari pamoja na ada zote.Tukatakiwa tutoe siku ya kwenda kuoa.
 
Tulikaa tena kikao cha ndugu tukapanga siku ya kwenda kuoa. Tulipokubaliana juu ya siku hiyo tukatoa taarifa upande wa pili. Mipango ya harusi ikafanyika kwa pande zote mbili na siku ilipowadia nikaoana na Mage.
 
Nilikaa na Mage nyumbani kwetu kwa wiki mbili tu kabla ya kuondoka kurudi Tanga, kwani likizo yangu ilikuwa ikikaribia kwisha.
 
Nilipoondoka nilikichukua kile kisanduku changu cha dhahabu na kuondoka nacho. Nilipofika Tanga nilimtambulisha mke wangu kwa polisi wenzangu tuliokuwa tunakaa kambini.
 
Polisi wenzangu walitupongeza kwa uamuzi wetu wa kufunga ndoa lakini pia walinilaumu kwa kutowaarifu kuwa ninaoa.
 
Siku mbili baada ya kufika, Tanga nilitoa mkufu wa dhahabu, bangili mbili na vipuli na kumpa mke wangu avae.
 
Usiku wa siku ile nilikwenda kutembea mjini na mke wangu ili kumuonesha mji. Tulirudi nyumbani karibu saa sita usiku. Tukafikia kulala.
 
Usiku ule ulikuwa balaa! Hatukulala. Mke wangu alikuwa akipiga kelele usiku kucha akidai kuwa kila alipofumba macho alikuwa akiona msichana anampiga bakora akimwambia avue zile dhahabu alizovaa.
 
Mwisho wake ilibidi mke wangu atii na kavua zile dhahabu nilizokuwa nimempa na hapo ndipo alipopata usingizi.
 
Kulipokucha asubuhi nilikichukua kile kisanduku nikakitia kwenye begi na kumpa polisi aliyekuwa jirani yangu.
 
“Tafadhali nihifadhie hili begi langu nitalichukua kesho” nikamwambia.
 
Kwa vile yule polisi alikuwa rafiki yangu akalichukua begi hilo na kunihifadhia chumbani kwake. Nikaenda zangu kazini.
 
Niliporudi kutoka kazini mke wangu akaniuliza maswali mengi kuhusu zile dhahabu nilizokuwa nimempa ambazo zilikuwa zimemtia wasiwasi mkubwa.
 
Nikamdanganya kwamba dhahabu hizo nilizinunua kwa sonara na kwamba nilishazirudisha.
 
“Sasa kwanini nilikuwa naota ile ndoto ya kuchapwa?” akaniuliza.
 
“Sijajua lakini nimemueleza sonara huyo ameniambia alikosea akaniuzia dhahabu za majini lakini kwa vile nimezirudisha hakutakuwa na tatizo.” Nikaendelea kumdanganya ili kumtoa wasiwasi.
 
ITAENDELEA KESHO, peruzi www.tangakumekucha.blogspot.com kila wakati kwa habari na matuiko ya papo kwa papo na motomoto.

No comments:

Post a Comment