Tangakumekuchablog
Tanga,MWENYEKITI wa Taifa baraza la Wanawake wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) , Halima Mdee, anatarajiwa kuwaongoza
wanawake siku ya wanawake Duniani mjini hapa pamoja na kuzindua matawi
mapya ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Tanga, Gress Joseph, alisema siku
hiyo pamoja na mambo mengine Mdee atazindua matawi na kutoa kadi kwa wanachama
wapya.
Alisema siku hiyo Chadema itaitumia
kwa kuwaelimisha wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za
kuongoza na kuacha woga na kuwa mstari wa mbele kuweza kutetea
maslahi yao.
Alisema kuna baadhi ya wanawake wako
na uwezo wa kuongoza lakini bado hawajawa na utayari wa kufanya hivyo jambo
ambalo limechangia kwa kiwango kikubwa wanawake kuwa nyuma katika sekta
mbalimbali za maendeleo.
“Siku ya wanawake Duniani Tanga
itazidi kunogeshwa na wabunge wengi wanawake akiwemo Halima Mdee----atatoa
misaada katika vituo vya watoto wanaoishi mazingira hatarishi” alisema na
kuongeza
“Haitoshi pia atazindua matawi
mapya ya Chadema na kutoa kadi kwa wanachama wapya katika mkutano wa hadhara
ambao utafanyika kata ya Nguvumali” alisema Gress
Alisema kwa sasa taratibu zote
zikiwemo za kibali cha mkutano zimeshafanyika na hivyo kuwataka wakazi wa
jiji la Tanga kukiunga mkono chama hicho ili kuweza kushika nafasi za kuongoza
katika uchaguzi wa Wabunge na Urais.
Kwa upande wake, Katibu wa Bawacha
Wilaya, Amina Mahmood, aliwataka vijana kujiunga na chama hicho kwani ndicho ambacho
kitaweza kuwakomboa katika dimbwi la umasikini uliowajaa.
Alisema hali ya maisha ya
Mtanzania imekuwa ngumu huku Serikali ikiwabana katika nyanja mbalimbali
za kujikwamua kiuchumi na hivyo kuwataka kukiunga mkono ili kukiweka kando
chama kilicho madarakani..
Alisema utitiri wa kodi zimekuwa
kikwazo cha maendeleo na kusema kuwa hakuna chama chochote ambacho kitaweza
kuzikomesha zaidi ya Chadema kwani kiko na dhamira ya kweli ya kumkomboa
Mtanzania.
“Chadema kila siku kimekuwa kikipiga
kelele za kuwaelisha wananchi kukiunga mkono kwani ndicho
kinachoweza kuwapunguzia mzigo wa kodi na makali ya maisha” alisema
Amina
Alisema mwaka huu Chadema
imedhamiria kuchukua viti vya Udiwani na Ubunge jimbo la Tanga kwa kufanya
mikutano ya uhamasishaji mjini na vijijini ikiwemo kufungua matawi na kuunda
timu moja ya ushindi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment