Wednesday, March 4, 2015

POLISI TANGA KUFANYA MSAKO MAJUMBA YA MADANGURO



TANGAKUMEKUCHABLOG

Tanga,JESHI la Polisi Tanga limesema litafanya msako katika kumbi na madanguro  ambayo yanatajwa kuendesha biashara ya kujiuza  na kuwataka wananchi kutoa taarifa za majumba yanayoendesha biashara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Juma Ndaki, alisema polisi itafanya msako huo baada ya taarifa kutoka kwa wananchi juu ya kuwepo kwa tabia hiyo.

Alisema polisi itafanya msako katika kumbi na majengo ambayo yanadhaniwa kuweko kwa biashara  hiyo haramu ambayo awali waliweza kuitokomeza na sasa kuibuka tena.

“Kama kweli biashara hiyo ipo katika maeneo hayo ambayo yanatajwa basi niwahakikishie wakazi wa Tanga kuwa polisi itaitokomeza-----msako huo utaenda sambamba na kuwachukulia hatua watu wanaojihusisha nayo” alisema Ndaki na kuongeza

“Tanga haiko na utamaduni huo kwani kama kweli tetesi zinazotajwa kuwepo na zikiachiwa zinaweza kuleta athari kwani hata watoto wadogo wanaweza kujitumbukiza katika mkumbo huo” alisema

Akizungumzia kuhusu watu wanaofanya biashara haramu ya mihadarati na upitishaji wa wahamiaji haramu, kamanda Ndaki alisema polisi itazidisha doria usiku na mchana katika mpaka wa Horohoro.

Alisema kwa sasa wameweza kuzuia mianya ya upitishaji wa mihadarati na wahamiaji haramu ila kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiibuka na kuwataka wakazi wanaoishi mpakani kuacha kushirikiana na watu wa aina hiyo.

“Natoa agizo kwa wakazi wanaoishi mipakani kuacha kushirikiana na watu wanaofanya biashara za magendo na upitishaji wahamiaji haramu-----tutaendesha msako na tutakaemgundua mahakamani” alisema Ndaki

Alisema msako huo utahusisha askari polisi na polisi jamii ambao watakuwa wakifanya kazi usiku na mchana na hivyo kuwataka wakazi wa maeneo hayo kuacha kujihusisha na watu wenye tabia hiyo.

                                              Mwisho

No comments:

Post a Comment