Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Kituo kinasajili wanafunzi wa kidato cha nne wapo Tanga mkabala na benki ya CRDB, simu , 0715 772746
NIPASHE
Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serilali (PAC) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, amejibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, kwamba naye amekuwa akipokea misaada mbalimbali kwa matumizi binafsi kuwa ni upuuzi.
Zitto alijibu tuhuma hizo jana kupitia ukurasa wake wa Facebook,
ikiwa ni siku moja baada ya Ngeleja kumtuhumu na kueleza kuwa tuhuma
hizo ni za kipuuzi na kwamba ameshawahi kuzijibu huko nyuma na kuziita
ni siasa za majitaka.
“Tuhuma
zote hizo zimeshawahi kutolewa huko nyuma, hazina msingi wowote na
zilikuwa siasa za majitaka, hata hivyo zimekuwa zikijirudia rudia kwa
malengo maalumu wanayoyajua wanaotoa tuhuma hizo”.
“Watuhumiwa
wa ufisadi wa Escrow hawajazoea kuona taasisi za maadili zikifanya kazi
kwa namna ilivyo sasa, hivyo wanajaribu na wataendelea kubwabwaja na
kuhangaika ikiwamo kutaka kila mtu aonekane ni mtuhumiwa kama wao.”
“Ndiyo
maana Ngeleja ametaja msururu wa watu akiwamo mfanyabiashara kwamba
huwapa fedha wabunge bila kuwapo chembe ya ushahidi, hivyo narudia
kutamka kwamba ninataka uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ufanyike mara
moja, wenye ushahidi wapeleke katika vyombo vya uchunguzi na niitwe
mbele ya Baraza la Maadili kujieleza,” Zitto.
Aidha, Zitto aliunga mkono kazi
iliyofanywa na Baraza la Maadili, alieleza kazi hiyo ilipaswa kuwa
imefanywa kwa muda mrefu sasa kwa kashfa mbalimbali zilizowahi kuwapata
viongozi, kama vile rada, rushwa katika manunuzi ya mafuta mazito ya
kuendeshea mitambo ya umeme, kujipatia mikopo katika taasisi za umma
bila kulipa na kujilimbilikizia mali tofauti na kipato.
Zitto aliiomba Sekretarieti ya Maadili
izichukulie kwa uzito tuhuma za Ngeleje dhidi yake, kwani kwa mujibu wa
sheria na kanuni za utumishi wa umma yanapaswa yafanyiwe uchunguzi.
Akijitetea juzi kwenye Baraza la Maadili, Ngeleja alikiri kupata mgawo wa Sh. bilioni 40.2 kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemalila wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd
na kudai kuwa wabunge wamekuwa wakifadhiliwa na wafanyabiashara na
mmoja wa wabunge walionufaika na misaada ya fedha za wafadhili, ni
Zitto, ambaye kisheria ni mtumishi wa umma.
NIPASHE
Taifa limekumbwa na msiba mkubwa, baada
ya watu 38 kufa na wengine zaidi ya 82 kujeruhiwa vibaya, baada ya
kuangukiwa na nyumba zilizobomolewa na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha
usiku wa kuamkia jana ikiambatana na kimbunga, katika kijiji cha
Mwakata, kata ya Isaka, wilayani hapa, mkoa wa Shinyanga.
Kufuatia maafa hayo, Rais Jakaya Kikwete,
amemtumia salamu za rambirambi na pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,
Ali Nasoro Rufunga, kuomboleza vifo vya watu 38 na pole kwa wengine 82
waliojeruhiwa.
“Nimepokea
kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 38
waliopoteza maisha na wengine 82 waliojeruhiwa na kukimbizwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu baada ya nyumba zao kusombwa
kabisa na maji kutokana na mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo
mkali kunyesha,”.
Rais Kikwete katika salamu zake kupitia
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, alisema msiba huo siyo wa
wananchi wa Shinyanga pekee, bali ni wa Taifa zima ambalo limepoteza
nguvukazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii.
Aliwaomba wafiwa wote wawe na moyo wa
uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao
wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao na wasisahau ukweli kwamba
kazi ya Mungu haina makosa.
Aidha, aliwahakikishia wafiwa wote kuwa
binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huo
mkubwa kwao na kwa Taifa.
Maafa hayo yalitokana na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali na hivyo kuathiri watu 3,500.
Alivitaja vijiji vilivyoathirika kuwa
ni, Makata ambako kaya 350 zimeathiriwa, kijiji cha Ngumbi, kaya 100
zimeathirika na katika kijiji cha Magung’hwa, kaya 50 zimeathiriwa.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha,
akizungumzia tukio hilo, alisema idadi ya watu waliokufa wengi wao ni
watoto ambao walisombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua hizo baada
ya maji kujaa ndani ya nyumba na kubomoa nyingine.
Kamugisha alisema idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na waokoaji kuendelea kufukua vifusi vya nyumba zilizobomoka.
Alisema hadi sasa majina ya waliokufa hayajafahamika kutokana na kuendelea kwa kazi ya uokoaji.
“Tunaendelea
na uokoaji na kufukua miili ya watu pamoja na madhara mengine yaliyopo,
idadi ya watu waliokufa inaweza kuongezeka… Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Mkoa wa Shinyanga itakutana baadaye ili kutathmini maafa hayo pamoja
na kujua msaada upi unahitajika kwa waathirika,” Kamugisha.
Alisema mvua hiyo ilianza kunyesha saa 4:00 usiku wa kuamkia jana na kudumu kwa saa kadhaa na kusababisha maafa hayo.
NIPASHE
Meneja Miradi ya umeme ya Kinyerezi, Simon Jilima, amesema mtambo wa Kinyerezi 1 unaojengwa na kampuni ya Yakobsen Elektro ya Norway unatarajia kukamilika mapema Juni mwaka huu.
Jilima aliyasema hayo mbele ya Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanya ziara katika mtambo
huo ili kujionea maendeleo ya ujenzi wake. Kamati hiyo imeanza ziara
ya kutembelea miradi ya umeme iliyopo katika mikoa ya Dar es Salaam,
Dodoma, Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa
madini aina ya tanzanite katika mkoa wa Manyara.
Jilima alisema kwa sasa mradi huo
umekamilika kwa asilimia 80 na kufafanua kuwa kazi inayofanyika kwa sasa
ni kumalizia utandazaji wa nyaya, ufungaji wa mabomba ya maji na gesi
pamoja na ujenzi wa barabara za ndani.
Alisema ofisi kwa ajili ya watumishi pamoja na karakana kwa ajili ya kuhifadhia mitambo imekamilika.
Jilima alisema mpaka sasa serikali
imelipa kiasi cha Dola za Marekani milioni 167.2 na kuongeza kuwa
kiasi cha Dola za Marekani milioni 15 kinatarajiwa kumaliziwa kabla ya
kukamilika kwa mradi.
Jilima alieleza kuwa awali changamoto
kubwa ilikuwa ni ukamilishwaji wa mradi wa bomba la gesi ili waanze
kutumia gesi hiyo katika kuzalisha umeme, lakini kutokana na kasi ya
mradi huo kuwa ya kuridhisha, wana imani kuwa gesi itaanza kuzalishwa
mapema kabla ya kukamilika kwa mtambo wa Kinyerezi 1
“Ndugu
wajumbe, awali tulikuwa na wasiwasi wa kupatikana kwa gesi kwa ajili ya
kuzalisha umeme kupitia mradi wa Kinyerezi 1 kutokana na mradi wa
bomba la gesi kuwa na changamoto nyingi, lakini baada ya kuona mradi
wa bomba la gesi uko katika hatua nzuri yaani zaidi ya asilimia 90,
tunaamini kuwa mara mtambo utapokamilika, gesi itakuwa imekwishaanza
kuzalishwa na hapo ndipo tutaanza kuzalisha umeme mara moja,” Jilima.
JAMBOLEO
Askari wa Jeshi la Polisi kikosi cha kutuliza Ghasia FFU Mkoani Mwanza PC Magesa ameuawa baada ya kunyongwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Kamanda wa Polisi Mwanza,kamishna msaidizi mwandamizi ‘SACP’ Valentino Mlowola alithibitisha jana ni kweli askari huyo ameuawa.
Askari huyo akiongozwa na polisi jamii
walikwenda eneo la tukio usiku kwa nia ya kuwakamata watu hao wanaodaiwa
kuwa ni wezi wa mafuta,lakini baada ya kupata taarifa walijipanga ili
kutelekeza unyama huo.
“Inaonyesha
askari polisi akisaidiwa na polisi jamii walikwenda kutekeleza jukumu
hilo kinyemela na walipofika eneo la tukio ambapo uhalifu ulitokea
walifanikiwa kuwakamata baadhi ya wahalifu”:-Mlowola.
“Lakini gafla walijitokeza wengine kasha kuwazingira na wakamuua askari wa FFU kwa kumnyonga shingo”.
HABARILEO
Mnikulu Shaban Gurumo
amekiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kwamba alipokea
Sh milioni 80.8 kutoka kwa James Rugemalira na kuzitumia kwa matumizi
yake binafsi, ingawa amekanusha kuomba fedha hizo.
Gurumo alitoa utetezi huo jana Dar es
Salaam mbele ya baraza baada ya kusomewa mashitaka ya kutumia cheo chake
cha uongozi wa umma vibaya na kujipatia fedha hizo, jambo ambalo ni
kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alikiri kumfahamu Rugemalira, akisema ni rafiki yake kwa zaidi ya miaka 10. Alisema daktari wake, Fred Limbanga ndiye aliyemtambulisha kwa Rugemalira.
“Kama Mnikulu sijawahi kupokea fedha za
kiuchumi kwa Rugemalira wala kuwa na mahusiano naye ya kiuchumi,
naitambua akaunti ya Mkombozi kuwa ni ya kwangu na niliifungua baada ya
James kunishauri,”:- Gurumo.
Alisema awali hakufahamu nani aliyemwekea kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti hadi hapo baadaye alipotambua kuwa ni Rugemalira.
Alidai hadi sasa hajafahamu sababu za
kupewa kiasi hicho cha fedha na wala hakuhangaika kumuuliza Rugemalira.
Pia, alisisitiza kuwa pamoja na kutofahamu fedha hizo alipewa za
matumizi gani, ana uhakika si zawadi kama inavyodaiwa.
“Ila
nahisi baada ya kuitwa na Kamati ya Uchunguzi ya Sekretarieti ya Maadili
ya Viongozi wa Umma kujibu tuhuma zinazonikabili, huenda Rugemalira
alinitumia fedha hizo baada ya kusikia kuwa nina mgonjwa anayeumwa
saratani ya mfuko wa uzazi,” alisema.
Alisisitiza kuwa hajawahi kuzungumza
wala kuomba fedha si kwa barua, simu wala kwa mazungumzo ya ana kwa ana
na Rugemalira, ila amekuwa akizitumia kwa shughuli zake binafsi kwa kuwa
alizikuta kwenye akaunti yake.
“Sijawahi kuomba fedha yoyote kwa Rugemalira wala VIP,”
alisema. Alisema pia hata katika tamko la mali na madeni,
aliloliwasilisha Desemba 29, mwaka jana kwa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, akiwa kama kiongozi wa umma, aliziorodhesha fedha hizo
kuwa ni mali yake iliyopo katika akaunti yake ya Benki ya Mkombozi
alizopewa na Rugemalira.
Alikiri kuwa alikuwa na matatizo ya kuwa
na mgonjwa huyo, aliyempeleka India kwa matibabu na hadi sasa
ameshatumia dola za Marekani 40,000 ambayo ni sawa na Sh milioni 73.2,
hivyo hakuwa na shida yoyote ya fedha. “Mimi nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira ndio maana sikuomba.”
“Nakiri
kupokea fedha hizo Sh milioni 80.8, lakini nilishangaa kwa mara ya
kwanza niliposikia kwenye redio iliyokuwa ikirusha hewani kipindi cha
Bunge, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alikuwa akisisitiza
nilipewa Sh milioni 800 na kampuni ya VIP Engineering and Marketing
Limited, jambo ambalo si la kweli,”.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment