Uchambuzi huu kutoka magazetini uneletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinapokea wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita. Kituo kiko na walimu waliobobea na kufaulisha. Kituo kimesajiliwa na NECTA. Wapo Tanga mkabala na bank ya CRDB, simu, 0715 772746
MWANANCHI
Machungu ya Watanzania yakiwa hayajapoa
kutokana na kashfa ya Sh306 bilioni kutoka katika Akaunti ya Tegeta
Escrow, ufisadi mwingine wa zaidi ya Sh252 bilioni umeibuliwa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa
Assad ndani ya wizara ya ujenzi.
Ukaguzi maalumu uliofanywa na ofisi ya
CAG katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 na 2011/12 umebaini kuwa
taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, bungeni
Novemba 2013 kuwa fedha hizo zilitumika kwa miradi ya ujenzi wa
barabara, haikuwa sahihi.
Kutokana na ufisadi huo, habari
zilizolifikia Mwananchi zinasema CAG amependekeza hatua stahiki
zichukuliwe kwa wahusika wa wizara ya ujenzi na wakala wa barabara ili
kuleta imani na uwazi katika bajeti kwa jamii na wahisani.
“Wizara (ya ujenzi) ililidanganya Bunge
kuwa kuna ujenzi wa barabara hizo wakati wakijua kwamba walikusudia
kulipa madeni ya wakandarasi na washauri wa ujenzi wa barabara…mpango
mkakati wa wakala wa barabara wa mwaka wa fedha 2011/12 pamoja na
manunuzi ulioidhinishwa havikuonyesha utekelezaji wa mradi huo,” chanzo
cha habari kilikariri ripoti ya CAG.
Matumizi hayo yasiyo sahihi yaliibuliwa
na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Novemba 22, 2013 baada ya kutilia
shaka kiasi hicho cha fedha na ofisi ya CAG kuagizwa kufanya ukaguzi.
Katika kikao hicho ambacho wizara ya
ujenzi iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake wa wakati huo, Balozi Herbert
Mrango alihojiwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe kuhusu hati ya
mashaka waliyoipata kutoka kwa CAG mwaka 2011/12.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti
ya mwaka huo Sh348.1 bilioni zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu
lililokuwa limetajwa kuwa ni la mradi maalumu hazikutumiwa kwa malengo
yaliyoelezwa bungeni.
“Ni vizuri leo (ilikuwa Novemba 22 mwaka
2013) uiambie kamati fedha hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika
kwa jambo gani. Tunajua kwamba fedha hizi zilipunguzwa Sh95 bilioni na
kupelekwa Wizara ya Uchukuzi, zilibakia Sh252.975 bilioni katika kifungu
hicho lakini kuna bilioni 100 zimetumika visivyo,” alisema Zitto.
Alisema katika majumuisho ya bajeti
wizara hiyo, Dk Magufuli na Dk Harrison Makyembe aliyekuwa Naibu waziri
wa wakati huo aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi
walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha hizo.
MWANANCHI
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa amesema analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua
mpango wa mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili
kumwekea sumu katika chakula au maji.
Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa
sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha
Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri
za chama hicho.
Tayari polisi imeanza kuchunguza taarifa
hizo na jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura
aliliambia gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ana haki kama watuhumiwa
wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za jinai na kusisitiza
kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na tunazichunguza.”
Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk
Slaa alisema, “Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema
sisi huwa tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi
na hili ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”
Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa na
mlinzi wake ameyaona kwa macho na kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na
wanaomtumia haziwezi kukiondoa chama hicho katika harakati zake za kila
siku.
“Tupo makini ndiyo maana tumebaini yote.
Tunawajua waliohusika na tupo makini katika kuwafuatilia. Kama Mungu
yupo upande wetu tumuogope nani zaidi,” alisema.
Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo
ni lazima wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa
kila aina, akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.
Tuhuma dhidi ya mlinzi huyo zilitolewa
juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando kuwa wamebaini
nyendo za mlinzi huyo na kuzifuatilia kwa ukaribu hadi kupata taarifa
hizo alizosema ni ukweli mtupu.
Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai
kuna mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari
2009 alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati
uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
MWANANCHI
Daktari bingwa wa zamani wa upasuaji
katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Fulgence Mosha anasotea mafao yake
ya kiinua mgongo na pensheni kwa miaka 10 mfululizo bila mafanikio.
Akizungumza juzi, Dk Mosha alisema licha
ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo husika, ikiwamo Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, bado mafao yake ni kitendawili.
Dk Mosha aliajiriwa na Serikali mwaka
1983 kabla ya Januari 1,1995 kupelekwa KCMC kwa barua ya Desemba 29,
1994 yenye kumb HE/MP ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Desemba 11, 2004, Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii ikauandikia barua uongozi wa KCMC kutoa kibali cha Dk
Mosha kustaafu rasmi baada ya kufikisha umri wa miaka 60 wa kustaafu
kisheria.
Alisema baada ya kustaafu, alilipwa Sh10
milioni na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF), ikiwa ni michango yake
na ya mwajiri ambaye ni Shirika la Msamaria Mwema (GSF) linalomiliki
KCMC.
“Katika utumishi wangu nimefanya
operesheni kubwa zaidi ya 7,000 zikiwamo za viongozi wakuu wa nchi hii
lakini leo baada ya kustaafu napigwa danadana sina thamani tena kwa
Serikali,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Mosha, utata wa mafao
yake ikiwamo kulipwa pensheni kila mwezi, unatokana na Hazina kutopeleka
mchango wowote katika Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Dk Mosha alisema baada ya kustaafu,
alichukua malipo yake ya NSSF na kuyapeleka PSPF ili yajumlishwe na
michango ya Serikali katika kipindi alichokuwa mtumishi wa Umma
(1983-1994).
“Zile fedha zilikaa kule, PSPF wakaamua
kunirudishia maana Serikali haikupeleka ile michango yake ambayo
walitakiwa wailipe kati ya 1983 na 1994 nilipokuwa serikalini,” alisema.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu malalamiko ya Dk Mosha
alionyesha kushtushwa na kusema, huenda daktari huyo hakutumia njia
sahihi kudai haki yake.
“Simfahamu huyo daktari lakini ni jambo
linaloshtua. Naomba mwelekeze aje ofisini na nyaraka zake zote nimpeleke
SSRA (Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii),” alisema
Kabaka.
Kwa mujibu wa Kabaka, kwa sasa zipo
kanuni zinazounganisha mafao kama mfanyakazi alifanya kazi katika maeneo
mawili yanayohudumiwa na mifuko miwili tofauti ya hifadhi ya jamii.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi wilayani hapa, limedai
kuwa watoto waliokutwa ndani ya nyumba katika eneo la Pasua, Manispaa ya
Moshi siyo wakazi wa Kilimanjaro na walikuwa wakiishi kwenye mateso
makubwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela imeeleza kuwa hayo
yalibainika katika mahojiano baina ya watoto na askari wa dawati la
jinsia.
Alisema watoto hao wanatoka mikoa mbalimbali ikiwamo Tanga, Mara, Kagera, Mbeya na Dodoma.
Kamanda Kamwela alisema pia wamegundua
kuwa watoto walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu ikiwamo kulala
chini katika chumba kidogo.
Alisema polisi linawashikilia watu wawili (mume na mke) ambao wanatuhumiwa kuwahifadhi watoto hao.
Kamanda huyo alisema watoto hao wana umri wa kwenda shule, lakini walikuwa hawasomi.
Alisema polisi wanachunguza aina ya masomo ya dini waliyokuwa wakifundishwa.
“Lazima tuchunguze uhalali wa masomo ya
dini waliyokuwa wakisoma ili tujue kama kweli watoto hawa walipelekwa na
wazazi wao au la, kwa kuwa watoto hao walipaswa kuwa shuleni” alisema
Kamanda Kamwela.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga
alisema watoto hao walikuwa wakiishi kwenye mazingira magumu, huku
wakipewa adhabu kali ikiwamo kubeba matofali mgongoni pindi wanapokosea.
“Maelezo ya watoto yanaonyesha walikuwa
wakiteswa, adhabu hizi kwa watoto ni kubwa, bado tunawachunguza ili
tujue kila kitu na walichukuliwaje huko majumbani kwao,” alisema
Makunga.
Alisema kwa wazazi watakaowatambua
watoto wao, wanapaswa kwenda na uthibitisho ikiwamo cheti cha kuzaliwa
au uthibitisho mwingine utakaoonyesha ni mzazi halisi.
NIPASHE
Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi wa Mamlaka ya
Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dk. James Benedict Diu, amekiri
kupokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 80.8 kutoka kwa mmiliki wa kampuni
ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira, huku akitoa
maelezo yanayokinzana kuhusu sababu za kupewa fedha hizo pamoja na
matumizi yake.
Fedha hizo, ambazo anadaiwa kuingiziwa
na Rugemalira katika akaunti yake iliyofunguliwa katika Benki ya
Biashara ya Mkombozi tawi la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, zinadaiwa
kuwa ni sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizochotwa kifisadi katika
akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Dk. Diu, ambaye amewahi kuwa Meneja
Udhibiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura)
mwaka 2006-2011, alitoa maelezo hayo kwa nyakati tofauti wakati akijibu
tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma zinazomkabili mbele
ya Baraza la Maadili jana na kudai kuwa hazijui kazi za Ewura.
Awali, akimhoji shahidi wa upande wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambao ni walalamikaji
katika shauri hilo, Zahara Guga, Dk. Diu alidai fedha alizopokea kutoka
kwa Rugemalira, hazikuwa zawadi, bali zilikuwa ni msaada zilizotolewa
kuchangia gharama za matibabu ya mkewe, Beatrice, ambaye kwa sasa ni
marehemu.
“Sijapokea zawadi, bali ni mchango kama
msaada wa matibabu ya mke wangu. Nasisitiza tena hii haikuwa zawadi.
Natambua kwamba iwapo ningepokea zawadi ningetamka kwa afisa mas-uul
(bosi wake) kwa kuwa ile haikuwa zawadi sikuona umuhimu wa kuitamka,”
alidai Dk. Diu.
Wakati awali akieleza fedha hizo
zikiluwa ni msaada kwa ajili ya kumuuguza mkewe. baadaye wakati akitoa
maelezo ya kujitetea mbele ya baraza hilo jana, Dk. Diu alidai fedha
alizopewa na Rugemalira zilikuwa ni mkopo wenye masharti nafuu, ambao
walikubaliana kwa mdomo aulipe siku yoyote atakapofanikiwa.
Hata hivyo, alipotakiwa na Wakili wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus,
alithibitishie baraza kuhusu makubaliano hayo kati yake na Rugemalira,
Dk. Diu alidai suala hilo ni kati yake na Rugemalira aliyempa mkopo huo
na kwamba, haliwahusu watu wengine.
Wakili Getrude alimhoji kama hakuona
haja na umuhimu wa kwenda na Rugemalira katika baraza kuthibitisha dai
hilo, Dk. Diu alidai alitegemea Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma wangemwita.
Alipohojiwa na Wakili Getrude sababu za
kutoenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuomba kibali ili kutimiza
matakwa ya sera kuhusu matibabu ya viongozi wa umma nje ya nchi, Dk. Diu
alijibu alishindwa kufanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho mgonjwa wake
alikuwa katika hali mbaya, hivyo hakukuwa na muda, kwani ilihitajika
haraka ya kumpeleka nchini India kwa matibabu.
Pia Wakili Getrude akimhoji, Dk. Diu
alikiri katika maelezo aliyoyatoa chini ya kiapo mbele ya kamati ya
uchunguzi ya sekretarieti hiyo kuwa fedha alizopokea kutoka kwa
Rugemalira zilikuwa ni kwa ajili ya kulipia deni la nyumba, iliyoko eneo
la Mbezi la mwaka 2012.
Hata hivyo, alidai alizitamka fedha hizo
kwenye fomu yake ya rasilimali za madeni kwa Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma.
Alidai matibabu ya mkewe yaliratibiwa na
Rugemalira, kutekeleza ahadi aliyoitoa baada ya kwenda kumuona katika
Hospitali ya TMJ na Sanitas, zilizoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam
alikokuwa amelazwa kwa nyakati tofauti wakati akiugua.
Alidai Rugemalira ni rafiki wa karibu na
wa siku nyingi yeye na familia yake na kwamba, alihitimu naye Shahada
ya Kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1982-1985.
NIPASHE
Baadhi ya wanazuoni, viongozi wa dini,
wanasiasa na wanaharakati wamesema hakuna muujiza wowote unaoweza
kufanyika hivi sasa kufanikisha kura ya maoni Aprili 30, mwaka huu.
Wamesema kulazimisha kura ya maoni kama ilivyotangazwa ni sawa na ‘kuchochea fujo’, jambo linaloweza kuepukika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana,
walisema nchi imegawanyika vipande vipande, huku wengine wakipinga
mchakato wote, hivyo kulazimisha kura ni kuendelea kuligawa taifa.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Semboja Hajji, alisema kulazimisha kura ya
maoni ni sawa na kuleta fujo.
“Hii iko very clear (wazi kabisa),
kwamba muda unapingana na jambo hili. Rasilimali muda ni jambo adimu na
mimi sizungumzi siasa, ni hali halisi kwamba, muda hauko na sisi kwa
sasa. Kwa ushauri wangu, tusilete fujo kulazimisha jambo hili. Unaweza
kulazimisha kufanya jambo zuri, lakini mwisho likaonekana halina maana
kabisa,” alisema.
Alisema hata kama kura ya maoni
haitafanyika sasa hivi, Watanzania wapo na Katiba ni yao, hivyo hakuna
mtu au chama chochote kinachoweza kufanikisha jambo hilo kwa sasa.
Dk. Semboja alisema hakuna sababu ya
kufanya haraka kwenye jambo kubwa na zito kwa mustakabali wa nchi kwa
miaka mingi ijayo na kusema Watanzania watamkumbuka Rais Jakaya Kikwete
kwa uamuzi wake wa busara wa kuanzisha mchakato huo na hivyo ni busara
sasa ikaachwa ili ipate muda wa kutosha kujiandaa kabla ya kura ya
maoni.
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole, alisema serikali haijajiandaa
kufanikisha kura ya maoni kwa kuwa nchi imegawanyika na wananchi hawana
uelewa wowote kuhusu Katiba inayopendekezwa.
Alisema kabla ya kura ya maoni, taifa
linahitaji muda zaidi kujenga muafaka na kuelimishana kuhusu maudhui
yaliyomo kwenye Katiba inayopendekezwa na namna ilivyopatikana.
Alisema siyo busara kwa nchi kuendelea
na mchakato huo na hata kufika kwenye kura ya maoni ikiwa vipande
vipande kama ilivyo sasa na kwamba, muda huo kwa sasa haupo.
“Tangu Katiba inayopendekezwa itolewe,
Watanzania hawajaelimishwa vya kutosha juu ya maudhui, wala iliyopelekea
kupatikana kwa rasimu hiyo kwamba, ni zao la kitu gani…Katiba hii
inapaswa ipimwe na iliyokuwa rasimu ya tume ya Warioba siyo kwa katiba
ya mwaka 1977 kama baadhi ya watu wanavyoeleza. Hatuwezi kwenda kwenye
kura Aprili 30,” alisema.
Alisema hata elimu kwa umma iliyopaswa
kutolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa mujibu wa sheria ya kura
ya maoni, bado haijatolewa na kwamba, hata asasi za kiraia, ambazo
zilitakiwa kushiriki kutoa elimu hiyo, nazo bado hazijaanza kazi.
MTANZANIA
Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu wakidaiwa kutoa mafunzo ya ugaidi kwa vijana wa
Tanzania mkoani Tanga.
Mmoja wao anaelezwa kuwa alikuwa pia
akitoa mafunzo ya jeshi kwa kundi la Hizbul al lililotaka kuipindua
serikali ya Somalia mwaka 2010.
Washtakiwa hao, Ally Nassoro au Dk. Sule
na Juma Zuberi au Kitambi, walifikishwa jana katika mahakama hiyo mbele
ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter
Njike akisoma mashtaka ya washtakiwa, alidai kati ya Oktoba Mosi, 2010
na Januari 30, 2001, katika eneo la Doblen Kisimayu, Somalia, Nassoro
aliwezesha watu kushiriki mazoezi ya jeshi ya kundi la Hizbul al, lengo
likiwa ni kuipindua Serikali ya Somalia.
Nassoro pia anadaiwa kati ya Mei Mosi,
2013 na Agosti 31, mwaka jana, katika Msitu wa Nguu ulioko eneo la Gombe
wilayani Muheza, Tanga, aliwapa mafunzo ya matumizi ya silaha watu
ambao hawakuwapo mahakamani hapo, lengo likiwa ni kufanya ugaidi nchini.
“Shtaka la tatu linamkabili Zuberi.
Anadaiwa kati ya Mei Mosi, 2013 na Agosti 23, mwaka jana katika Msikiti
wa Kichangani, Magomeni, Dar es Salaam, alimsaidia Ally Nassoro
kutekeleza vitendo vya ugaidi kwa kumpa sehemu ya kukaa na kutekeleza
mipango yake.
“Zuberi unadaiwa katika kipindi hicho
ukiwa na eneo la biashara katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni,
ulimruhusu Ally Nassoro kukaa na wenzake kupanga na kujadili mipango ya
mafunzo kwenye Msitu wa Nguu kutekeleza vitendo vya ugaidi,” alidai
Wakili Njike.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Hakimu Riwa alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 23, mwaka huu itakapotajwa tena na washtakiwa walirudishwa rumande.
MTANZANIA
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) imetoa miezi mitatu kwa Msajili wa Hazina kuratibu na kusimamia
uanzishwaji wa shirika jipya la ndege litakaloendeshwa na mamlaka za
hifadhi za taifa ili kutoa huduma kwa abiria na watalii
Mamlaka hizo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Akizungumza na wadau katika kikao cha
majadiliano kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa PAC,
Zitto Kabwe, alisema mamlaka hizo zitashirikiana moja kwa moja na
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kuangalia namna ambayo shirika hilo
linaweza kufanya kazi zake, hivyo kusaidia Serikali kuongeza mapato.
“Lengo letu ni kuhakikisha Serikali inamiliki ndege zake binafsi ambazo zitaweza kubeba abiria na watalii wanaokuja nchini, hivyo kusaidia kuongeza mapato,” alisema Zitto.
“Lengo letu ni kuhakikisha Serikali inamiliki ndege zake binafsi ambazo zitaweza kubeba abiria na watalii wanaokuja nchini, hivyo kusaidia kuongeza mapato,” alisema Zitto.
Mwenyekiti huyo wa PAC alisema mchakato
wa uanzishwaji wa shirika hilo ulianza mwaka 2011 ambapo wabunge kwa
pamoja waliangalia namna ya kulishughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja
na kuzitaka mamlaka hizo kuanzisha mashirika ya ndege ili yaweze kufanya
kazi hiyo.
Alisema ilipofika Novemba 2012, wabunge
hao walifikia maazimio ya kuitaka Serikali kutekeleza maagizo
yaliyotolewa na wabunge ili kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo,
Serikali iliziandikia barua mamlaka hizo na kuwataka kuchangia
uanzishwaji wa shirika hilo jipya bila ya kumiliki jambo ambalo ni
kinyume na maazimio ya wabunge.
“TANAPA na Ngorongoro walikuja kwenye
kamati na kulalamikia uamuzi wa kuchangia kwa madai kuwa wametwishwa
mzigo kwa kuwa wanakatwa kodi nyingi.
“Kwa mwaka wanatoa wastani wa Sh bilioni
15 za pato ghafi kwenda hazina, halafu wanatoa asilimia 3 ya mapato yao
kwa ajili ya kupeleka Wizara ya Maliasili na Utalii na asilimia 30 kwa
ajili ya kodi,” alisema Zitto.
Alisema ikiwa watapunguziwa kodi na makato mbalimbali, wataweza kutoa Sh bilioni 30 kwa ajili ya uanzishwaji wa shirika hilo.
Alisema ikiwa watapunguziwa kodi na makato mbalimbali, wataweza kutoa Sh bilioni 30 kwa ajili ya uanzishwaji wa shirika hilo.
Alibainisha wakati wanaangalia namna ya
kulishughulikia suala hilo kamati hiyo ilikaa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuangalia namna ambayo wanaweza
kulishughulikia suala hili.
Alifafanua kutokana na hali hiyo, kamati
imeamua kuwaita wadau wote hao ili kukaa kwenye kikao cha majadiliano
na kufikia uamuzi wa kuanzishwa kwa shirika hilo hadi ifikapo Juni mwaka
huu.
HABARILEO
Wakazi 10 wa jijini hapa, akiwemo
mwanafunzi wa sekondari wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
wakikabiliwa na makosa matano tofauti kuhusu tukio la kuwanyang’anya
polisi silaha pamoja na kumuua askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Sajenti Mohamed Rashid Kajembe.
Mwanafunzi aliyefikishwa mahakamani ni Rajab Bakari (19) wa shule ya sekondari na mkazi wa Makorora jijini hapa.
Watuhumiwa tisa wameelezwa kuwa ni
wafanyabiashara, nao ni Mbega Seif (25) maarufu ‘Abuu Rajab’ mkazi wa
Kiomoni, Amboni, Ayubu Ramadhani (27) maarufu ‘Chiti’ ambaye ni fundi
umeme na mkazi wa Kona Z Kiomoni, Hassani Mbogo (20) maarufu
‘Mpalestina’ mkazi wa Makorora, Mohamed Ramadhani (19) mfanyabiashara na
mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25) maarufu ‘Kizota au Kisaka’ mkazi
Magaoni. Washtakiwa wengine ni Saidi Omari (26) mkazi wa Magaoni Tairi
Tatu, Nurdin Mbogo (27) Makorora, Ramadhan Mohamed (18) mkazi wa Donge
pamoja na Omari Harubu Abdala (55) maarufu ‘Ami’ mkazi wa Dunia Hoteli
Makorora.
Wakisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu
Mkazi Aziza Rutala, Wakili wa Serikali, George Barasa akisaidiana na
MariaClara Mtengule, walidai kuwa kosa la kwanza hadi la tatu
linawahusisha washitakiwa namba moja mpaka nane (1 8) ambao
wanatuhumiwa kushiriki kula njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria.
Barasa alidai kuwa katika maeneo tofauti
ya jijini Tanga kati ya Septemba mosi 2014 hadi Januari 26 mwaka huu,
washitakiwa wote wanane kwa pamoja walitenda kosa la kula njama na
kufanya kosa la unyang’anyi wa silaha.
Katika kosa la pili, Barasa alidai
mahakamani hapo kwamba mnamo Januari 26 mwaka huu, katika mgahawa wa
Jamali ulipo kati ya barabara ya Nne na ya Tano jijini Tanga,
washitakiwa wote wanane waliiba silaha moja aina ya SMG namba za usajili
14303545 mali ya Polisi na muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo
walitumia visu kumchoma askari H 501 Mwalimu ili kupata silaha hiyo.
Kosa la tatu la washitakiwa hao ni
unyang’anyi wa kutumia silaha, na washitakiwa wote wanane wanadaiwa kuwa
katika mgahawa wa Jamali uliopo kati ya barabara ya nne na ya tano
waliiba silaha nyingine yenye namba za usajili 14301230 SMG mali ya
polisi na kwamba muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walimtishia.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete amesema alipoingia
madarakani, serikali ilikuwa ikikusanya mapato ya Sh bilioni 170 kwa
mwezi, lakini sasa inakusanya Sh bilioni 900 kwa mwezi.
Rais alisema hayo Dar es Salaam jana
wakati akifungua Mkutano wa 22 wa Wahasibu Wakuu wa Ukanda wa Afrika
Mashariki na kusini mwa Bara la Afrika (ESAAG), ulioshirikisha nchi 14.
“Nilipoingia madarakani, serikali
ilikuwa ikikusanya mapato ya Sh bilioni 170 kwa mwezi, lakini sasa
serikali inakusanya Sh bilioni 900 kwa mwezi, lakini kutokana na utawala
bora na uwajibikaji, sasa serikali inakusanya Sh bilioni 900 kwa mwezi
na hiyo inachangiwa pia na sheria nzuri za usimamizi wa fedha na
manunuzi,” alisema Rais ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka
2005.
Rais aliwataka wahasibu na wakaguzi wa
fedha, kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha na kukagua miradi ili
iendane na thamani halisi ya fedha zilizotolewa kwa manufaa ya umma.
Pia, aliwataka wahasibu na wakaguzi hao
kuzingatia elimu waliyonayo kwa kutoa hati safi, kulingana na ubora,
badala ya kutoa hati hizo kwa kujuana au bila kujiridhisha.
Akitoa mfano, alisema kijijini kwake
iliwahi kutolewa hatisafi na ilielezwa kuna miradi miwili imetekelezwa,
lakini kiuhalisia hapakuwa na miradi hiyo, hali inayoonesha kwamba
ukaguzi haukufanyika kwa usahihi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment