Saturday, February 14, 2015

CHAGONJA AILAUMU MITANDAO YA KIJAMII KUPOTOSHA TUKIO LA TANGA



Tangakumekuchablog
KAMISHNA wa Polisi Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi Taifa, Poul Chagonja, ameilaumu mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kusambaza taarifa za tukio la mapambano kati ya Majambazi na polisi na kulibadilisha kuwa la Kigaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishana huyo alisema tukio lililotokea Tanga ni la majambazi kurushiana risasi na polisi baada ya kufanya uvamizi eneo ambalo lilisadikika kuwa walijificha.
Alisema wakati wa uvamizi huo majambazi hayo yalikuwa yamejificha katika mapango ambayo yanatumika kama kivutio cha utalii na kuweza kuwashambulia askari kwa ushirikiano  na wanajeshi.
Katika kulizungumzia hilo, Chagonja alisema kuna baadhi ya mitandao imekuwa ikipotosha taarifa na  kuwapa vitisho wananchi kuwa tukio hilo ni la Kigaidi.
Aliitaka mitandao hiyo ya kijamii kuacha kusambaza  taarifa za upotoshaji na kuutumia vyema uhuru wao wa habari kwa kuisaidia jamii katika mambo mbali mbali yakiwemo ya kimaendeleo.
“Tukio la Amboni ni la Majambazi na sio la kigaidi kama baadhi ya mitandao ilivyoripoti kuwa Alshaabaab wameingia Tanga-----taarifa hizi sio za kweli na uongo” alisema Chagonja
“Hakuna kitisho cha Kigaidi si cha Al Shaabab wala Alqaida na lolote linalojitokeza tutawataarifu wananchi na kwa sasa wafanye shughuli zao kama kawaida” alisema
Taarifa za kuwepo kwa kundi la Al Shaabab eneo la Amboni liliishutua jiji la Tanga na nchi nzima baada ya mitandao ya kijamii kusambaza  uwepo huo na hivyo kuzusha taharuki.
Baada ya ufafanuzi wa jeshi la polisi juu ya tukio hilo wananchi wamekuwa wakifanya shughuli zao za kujiletea maendeleo na kazi za mashambani kama kawaida.
                                                       Mwisho

No comments:

Post a Comment