Hadithi
YALIYONIKUTA TANGA (18)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
“Mwenye nyumba alikwishakufa”
Mwanamke huyo alituambia.
“Sawa. Nani anayemiliki kwa
sasa?”
“Ndiyo haijulikani”
“Sasa hicho ndicho
tunachotaka kujua. Na hatuwezi kujua bila kuwapata wahusika’
“Kama
mngeweza kuja usiku mwingi mnaweza kuwapata. Mchana hawapo”
“Tutajaribu kufanya hivyo, Asante”
Meja akamuaga yule mwanamke,
tukaondoka na kurudi kwenye gari.
Tulipofika kituoni tulianza
kufanya uchambuzi. Katika uchambuzi wetu tulipata mashaka kuwa jinsi
tulivyolala fofofo usiku ule na kuamka asubuhi ilitokana na hao majini. Meja
mwenyewe aliamini kuwa majini hao ndio waliotutia usingizi.
“Sasa leo tutakwenda kukaa
barazani kabisa. Gari la doria liwe linatupitia mara kwa mara ili tusilale”
Meja akatuambia.
Tukapanga tena kukutana saa
sita usiku. Kwa upande wangu mawazo yangu yalikuwa kwenye likizo yangu. Siku
zilikuwa zimeshawadia. Nilibakisha siku moja tu nianze likizo, nikaona niende
kwa bosi wangu, afisa upelelezi wa wilaya nikamueleze suala hilo.
Nilipokwenda kwa afisa
upelelezi akaniambia nimuone afisa upelelezi wa mkoa. Nikaenda kwake. Baada ya
kumueleza kuhusu likizo yangu nilimuona akiuma midomo yake.
SASA ENDELEA
”Itawezekanaje kwa sasa?”
akaniuliza lakini kama aliyekuwa akijiuliza
mwenyewe kisha akaongeza.
“Subiri kidogo”
“Hadi lini?” nikamuuliza.
“Kwani ulitakiwa uanze lini
likizo yako?”
“Nilitakiwa kuanza kesho”
“Subiri hadi utakapoambiwa”
Afisa upelelezi wa mkoa
aliponiona nimenywea aliniambia.
“Si unajua kuna huu upelelezi
wa mauaji ya Sajenti Erick ambao unakuhusu sana wewe”
“Sasa sijui upelelezi huu
utaisha lini. Nadhani utachukua muda mrefu”
“Hauwezi kuchukua muda mrefu,
kuna mambo tu tunataka tuyaelewe vizuri”
Afisa upelelezi akainua mkono
wa simu iliyokuwa juu ya meza yake akampigia afisa upelelezi wa wilaya.
“Hivi huu upelelezi wa mauaji
ya Sajenti Erick umefikia wapi?” akamuuliza.
“Kuna timu ya polisi
inaendelea na uchunguzi, niliambiwa jana usiku walikwenda kwenye nyumba ya yule
mwanamke aliyekufa mahabusi pale barabara ya nane, kuwavizia watu wanaofika
hapo wakati wa usiku lakini polisi wote walipitiwa na usingizi hadi asubuhi…”
nikaisikia sauti ya afisa upelelezi wa wilaya akimueleza ule mkasa uliotutokea
usiku uliopita. Alimuelezea mwanzo hadi mwisho.
“Sasa leo wamepanga kwenda
tena lakini watakuwa barazani mwa ile nyumba. Na gari letu la doria litakuwa
linawapitia mara kwa mara” Afisa upelelezi aliendlea kumueleza.
“Lakini wana uhakika kwamba
hao watu wanafika usiku?”
“Majirani waliwaeleza kuwa
wanafika kuanzia saa nane usiku. Hata jana walipoamka asubuhi waliuliza,
wakaambiwa walifika”
“Martin anataka kwenda likizo
unadhani kuondoka kwake kutaathiri uchunguzi huo?”
“Nafikiri hadi kesho ninaweza
kuwa na jibu”
“Sawa”
Afisa upelelezi wa mkoa
akakata simu.
“Basi wewe nenda, njoo
uniulize keshokutwa” akaniambia.
Nikatoka hapo ofisini na
kurudi kituoni.
Wakati wote nilionekana kuwa
na fadhaa na kwa kweli sikuweza kufanya kazi kama
ilivyo kawaida yangu. Nilikuwa nawaza mengi. Japokuwa kwa upande wa ile kesi
sikuwa na wasiwasi sana,
nilikuwa na wasiwasi na wale majini.
Niliamini kuendelea kuwa na
kile kisanduku cha dhahabu kungewafanya majini hao waendelee kuniandama na
mwisho wake waitoe roho yangu. Sikuwa na pa kukipeleka. Ningeweza kukitupa
lakini nilijiambia, nikikitupa kinaweza kuokotwa na mtu mwingine na hivyo
kunisababushia matatizo zaidi.
Na akama ni kukirudisha kwa
wenyewe, sikujua ningekirudisha wapi. Sikuwa na haja nacho tena kwa kujua kingeniangamiza.
Pia ningeweza kukisalimisha polisi lakini ndio ningeumbuka kwa kuonekana
nilimdhulumu yule mwanamke.
Yale mawazo ya kupata utajiri
baada ya kuuza ile dhahabu yalikwishafutika akilini mwangu.
Kama ningefanikiwa kupata ile likizo yangu, niliendelea
kuwaza, ningekwenda na hicho kisanduku hadi kwetu Kagera. Huko ningepata
ushauri kutoka kwa wazazi na ndugu zangu na ningejua nini cha kufanya.
Pia kule kwetu kuna waganga
wa kienyeji wanaojua mambo ya majini ambao nilitarajia kuwa wangenisaidia baada
ya kuwaeleza ukweli wote. Lakini kwa jinsi mambo yalivyokuwa yanakwenda
nilipata wasiwasi sana.
Nilikuwa sijui nifanye nini.
Akili yangu ilikuwa ikiwaza kila kitu. Ile juhudi yetu ya kumtafuta mwenye ile
nyumba haikuwa na maana yoyote kwangu kwani hata akifahamika bado tatizo lingeendelea
kuniamdma, nilijiambia.
Lakini kwa vile lilikuwa
zoezi lililopangwa na viongozi wangu wa kazi ilibidi nilitekeleze ili niweze
kujinasua na tuhuma za mauaji ya Erick. Kwa kanuni za kipolisi ninaweza kuwa
mshukiwa namba moja kutokana na uhusika wangu katika mauaji ya polisi huyo.
Usiku haukuchelewa. Saa sita
usiku polisi watano nikiwemo mimi na meja wetu, tukaenda barabara ya nane
kwenye ile nyumba.
Kwanza tulimgongea na kumfahamisha yule mwenyeji wetu wa
nyumba ya jirani kuwa tumekuja kuwasubiri hao watu ambao kelele zao wanazisikia
kuanzia saa nane usiku.
“Kama
mtazisikia, tunaomba mtufahamishe. Sisi tutaendelea kuwepo hadi watakapokuja
hao watu” Meja Elias alimwambia yule mwanamke.
“Sawa. Kma tutawasikia
tutawafahamisha”
Mwanamke akarudi ndani na
kufunga mlango. Tukapata wazo kuwa tukae katika nyumba ile ile ili
tusiwagutushe hao watu.
Wakati tumekaa mazungumzo
yakaanza. Meja Elias ndiye aliyeanza kusimulia visa vya majini ambavyo alidai
kuwa alikutana navyo akiwa katika kazi yake ya upolisi.
Alituambia kwamba kulikuwa na
siku alitongoza mwanamke alipokuwa mkoa wa Pwani. Kumbe mwanamke yule alikuwa
ni jini. Yule mwanamke alimwambia kuwa alikuwa na chumba chake akamtaka Meja
waende katika chumba hicho.
Meja akakubali na wakaenda katika
chumba cha mwanamke huyo ambacho kilikuwa kimepambwa vizuri. Walipofika Meja
hakukumbuka nini kilitokea. Alishitukia kumeshakucha.
“Nilijikuta nimelala juu ya
mti wa mbuyu nikiwa peke yangu na nikiwa na nguo zangu vile vile. Kwa kweli
nilishituka sana”
Meja akatuambia na kuongeza.
“Nilishuka kwenye ule mti na
kurudi zangu nyumbani na tangu siku hiyo nilipata adabu”
Je nini kitaendelea? Endelea
kufuatilia hapo kesho.
Kwa mengi mazuri usiache kuperuzi blog hii na kupata habari na matukio ya papo hapo kemkem na ya kusisimua www.tangakumekucha.blogspot.com
|
Saturday, February 14, 2015
YALIYONIKUTA TANGA (18)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment