MWANANCHI
Santnam Singh mwenye
umri wa miaka 43 amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa
faini ya Sh 380,000/- baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kisu
katika Uwanja wa Kimataifa wa JNIA Dar ambapo mtuhumiwa huyo aliachiwa
huru baada ya kulipa faini.
Akisoma hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hassan Juma
amesema kwamba mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo kutokana na
kukiri kutenda kosa hilo na kutakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu
jela au kulipa faini ya Sh 380,000.
Upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka yake bila ya kuacha shaka kwa kutoa kielelezo cha mashitaka hayo ambacho ni kisu.
Katika utetezi wake, Singh alidai kwamba anategemewa na familia yake na kwamba anaomba apunguziwe adhabu, ombi ambalo lilitupiliwa mbali.
Singh alidaiwa kwamba Januari 10 mwaka huu, maeneo ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar alikutwa na kisu kinyume na sheria.
JAMBO LEO
Mlinzi wa Makao makuu ya BIMA ambaye
jina lake halijafahamika amezimia baada ya Polisi kupiga risasi juu kwa
bahati mbaya wakati wakichukua fedha katika tawi la Benki.
Mlinzi mwenzake aliulizwa mwenzake alipo baada ya tukio hilo akasema kuwa amerudi nyumbani.
“Askari alikuwa akiweka sawa silaha yake, lakini kwa bahati mbaya ikatoka..” aliongea shuhuda mmoja, Benard Adam ambaye ni mfanyabiashara.
JAMBO LEO
Maiti za watoto wachanga watatu
wanaokadiriwa kuwa na umri wa mwezi mmoja zimekutwa zikiwa ndani ya
mfuko wa rambo kwenye jokofu ndani ya nyumba ya mtu Johannesburg, Afrika
Kusini.
Mfanyakazi wa ndani amesema aligundua
harufu kali kutoka kwenye friji akahisi ni nyama imeharibika, baada ya
kufungua akakutana na miili ya watoto hao.
Mfanyakazi huyo amesema aliagizwa
kufanya usafi ili wakafanye mazishi ndipo alipogundua kuwepo kwa miili
ya watoto hao kwenye friji hiyo.
NIPASHE
Kamanda wa Kikosi cha Askari wa Usalama Barabarani Mohamed Mpinga
amesema madereva wengi hawana nidhamu wanapokuwa wakiendesha vyombo vya
usafiri na kusababisha 20% ya wanaopata ajali kufariki kutokana na
matumizi ya pombe.
“Wengi wa madereva wanapopimwa kipimo kinaonyesha wamelewa kwa asilimia 90, pia Kenya na Burundi ni kama Tanzania“—Kamanda Mpinga.
Aidha, alisema madereva wengi wanatumia
pombe za viroba kwa kuchanganya kwenye maji, suala ambalo linazidi
kuhatarisha usalama wa barabarani.
Kamanda Mpinga alisema
ajali kwa Tanzania zimepungua kwa 39% mwaka 2013-2014, upungufu huo ni
29%, ajali zilizosababisha vifo ni 23,842 mwaka 2013 na mwaka 2014 ajali
zilizosababisha vifo ni 14,360.
Mpinga amesema madereva
waliopata ajali na kupata ulemavu wakudumu ni 12%, waliopata majereha
ni 20,689 kwa mwaka 2013 na kwa mwaka 2014 waliopata majereha ni 14,530.
Mpinga alisema kuwa ajali zimepungua
kutokana na Jeshi la Usalama Barabarani kusimamia sheria pamoja na kutoa
adhabu kali kwa madereva wazembe na kufanya ukaguzi wa magari mabovu
mara kwa mara.
NIPASHE
Wizi wa fedha kwa njia ya mtandao
kupitia mashine maalum za kutolea fedha (ATM) unaendelea kuzitesa benki
mbalimbali nchini ambapo kwa sasa wahalifu hao wanahamisha fedha za
wateja wakiwa nje ya nchi kwa kutumia kadi za kutolea fedha.
Wizi huo hufanyika kwa kutumia kadi za
kutolea fedha zinazoingiliana na benki zingine (smart card) ambazo mteja
wa benki anaweza kutolea fedha akiwa popote duniani kupitia ATM.
Chanzo cha habari cha Gazeti la NIPASHE
kimetaarifu kuwa wezi hao hucheza na password za watu wanaopenda kutoa
fedha zao kupitia ATM zilizowekwa sehemu mbalimbali hasa kwenye vituo
vya kujazia mafuta ambapo mmoja ya waathirika wa tukio la aina hiyo
amesema juzi alipigiwa simu na ofisa mmoja wa benki akimuuliza kama siku
hiyo alitoa fedha akiwa nje ya nchi.
Alisema ofisa huyo alimpigia simu baada
ya benki kupata wasiwasi kwa kuwa taarifa hazionyeshi kama mteja huyo
huchukua kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa mara moja.
“Nilipigiwa
simu na mtu akaniuliza wewe ni fulani (akataja jina), akaniuliza
nimetoa fedha kiasi fulani nikiwa Mombasa? Nikamjibu sijatoa na
sijawahi kutoa fedha nje”.
Chanzo hicho kilisema, ofisa huyo
alimwambia kuna hamisho la fedha limefanyika kutoka kwenye akaunti yake
nje ya nchi na kumtaka aende kwenye tawi lolote la benki hiyo ili aombe
taarifa yake ya kibenki na kisha aandike barua ya kulalamika kuwa
hajatoa fedha hizo kwenye akaunti yake.
“Nilipoitazama nikaona fedha zangu zimehamishwa na mtu aliyekuwa Mombasa, Kenya,”;
alisema mtu huyo na kuongeza kuwa alitakiwa kuandika barua kwa meneja
wa benki hiyo kwenye Tawi hilo ili aombe kurejeshewa fedha hizo.
Alisema wakati huo akaunti yake ilikuwa
imefungwa na kadi imezuiwa kutoa fedha na kutaka kujaza fomu ya kupata
kadi nyingine ambayo alipewa ndani ya dakika tano na baada ya
kukamilisha taratibu za madai alipata taarifa iliyomjulisha kuwa fedha
zake zitarudishwa ndani ya siku 45.
Afisa mmoja wa benki ambaye hakupenda
jina lake litajwe gazetini alikiri kuwa kuna wizi wa fedha wa mara kwa
mara kwa njia ya mtandao ambao benki umeshaugundua.
Alisema wezi hao hutumia njia mbali
mbali kujua password za watu ikiwemo ya kuweka kamera ndogo kwenye ATM
na vile vile kwa kutumia utalaam wa kiteknolojia wa hali ya juu kusoma
taarifa za benki na kuzitumia kuiba fedha kwenye akaunti za watu.
Alishauri wanaopenda kutoa fedha kwenye
ATM waende kwenye ATM zilizo kwenye matawi ya benki husika kwa kuwa
wanaoweka kamera sio rahisi kwenda kwenye matawi ya benki.
Gavana wa BoT, Prof. Benno Ndulu
aliwahi kukaririwa akisema wameziagiza benki kuweka kifaa cha umeme
(electronic chip) kwenye kadi zao za ATM ambazo si rahisi kughushi.
NIPASHE
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la
NIPASHE umegundua Wanafunzi wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam,
wamejiingiza katika wimbi la utumiaji wa dawa za kulevya na uchezaji
kamari, hali inayoodhofisha elimu huku bangi, heroin na cocaine
zikiongoza kwa kuuzwa.
Wanafunzi hao kwa sasa wameunda mtandao
maalum wa kuwakutanisha na wafanyabiashara wa madawa hayo ili kuepuka
kukamatwa na polisi.
Moja ya eneo lililoshamiri kwa matukio
hayo ni Toangoma jirani na shule mbili za sekondari ya Malela na
Toangoma, ambapo hivi karibuni wanafunzi sita walikamatwa wakiwa na kete
116 ya bangi na misokoto sita huku mtu mmoja Bashir Hemed akitiwa mbaroni kwa kutuhumiwa kumiliki shehena ya bangi iliyokutwa eneo hilo.
Hamisi Zuberi ambaye
aliongoza zoezi la kupambana na mtandao huo, alisema wanafunzi hao sita
ni miongoni mwa wengine zaidi ya 100 waliokutwa wakinunua na kutumia.
“Ni
tukio baya hasa kutokea kwa idadi kubwa ya wanafunzi wakivuta bangi nje
ya shule, ni mtandao mkubwa unaowahusisha wafanyabiashara na wanafunzi,”– Hamisi Zuberi.
“Wanaokuja
kuuza majani (bangi) mbona wapo wengi tu, tunaomba serikali iongeze
kasi ya kuwakamata ili tuweze kusoma vizuri kwani mara nyingi wanapotoka
kuvuta wanatusumbua darasani,” alisema mwanafunzi mmoja
Makamu wa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Toangoma, Florian Kilindo alikiri kuzidiwa na mtandao huo ambapo walimu walioufuatilia walitishiwa usalama wao hivyo kuitaka serikali kuingilia kati.
“Imefika
wakati sisi kama walimu tumeona hatuwezi tena kuwadhibiti, kila mara
tumeomba msaada wa polisi kuja kuwakamata lakini bado mtandao unazidi
kukua na kuhatarisha usalama wetu na wanafunzi wengine darasani,” alisema.
Mwalimu Kilindo, aliwalaumu wazazi kukwepa majukumu ya kuwafuatilia watoto wao, badala yake wanaona kazi hiyo inafanywa na walimu pekee.
Uongozi wa shule hiyo umewasimamisha
masomo wanafunzi wanaohusishwa na utumiaji wa dawa hizo hadi hapo Bodi
ya shule hiyo itakapokaa na kuwajadili.
“Polisi
wametuambia wamewaachia huru kwa sababu hawana sheria ya kuwashikilia
wanafunzi kwa muda mrefu, hapa tunavyoongea wameachilia lakini sisi
tumewasimamisha masomo,” – Mwalimu Kilindo.
Diwani wa Kata ya Toangoma, Rashid Mikuki amesema amesikitishwa kuona wanafunzi wanaoacha shule na badala yake wanaishia porini kuvuta bangi.
Waziri wa Elimu na Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alipoulizwa kuhusu suala hilo, alionyesha kushtuka na kusema kwamba hakutarajia kulisikia na aliahidi kulifanyia kazi.
RAIA TANZANIA
Wiki mbili tangu tarehe ya mwisho
itangazwe na TRA kwa wanufaika wa fedha za Escrow kulipa kodi, taarifa
zilizolifikia gazeti la RAIA TANZANIA ni kwamba agizo hilo limeanza
kutekelezwa.
Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade
amesema fedha hizo zimekusanywa kutoka katika Ankara za malipo
(invoices) walizopelekewa wadaiwa mwishoni mwa mwaka jana japo amesema
kuhusu kiasi kilichokusanywa ni siri kama ambavyo taarifa za walipa kodi
wengine huwekwa siri.
“Sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa Sheria na walipa kodi wanatakiwa kulipa kodi husika. Siwezi kukutajia kiwango kilichokusanywa”—Rished Bade.
Wakati wa Bunge lililopita Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
alisema kiwango cha pesa kinachotakiwa kukusanywa ni sh. Bil 26 na
iwapo TRA wakikusanya kiwango hicho cha pesa basi ni furaha kubwa kwake.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment