Mkusanyiko wa Stori zilizopewa Headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania February 3, 2015 ziko hapa
MWANANCHI
Wabunge jana waliwaweka kitimoto
mawaziri wanne wakiwataka watoe maelezo ya kukwama kwa baadhi ya mambo
katika wizara zao na kusababisha matatizo kwa wananchi na Serikali
kukosa fedha.
Mawaziri hao ni wa Maliasili na Utalii; Lazaro Nyalandu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; William Lukuvi, Waziri wa Maji; Prof. Jumanne Maghembe na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Stephen Wasira.
Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa
shughuli za Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na ile ya Ardhi, Maliasili
na Mazingira, wabunge hao walionekana kukerwa na ahadi zisizotekelezeka
za mawaziri hao kiasi cha wao kukata tamaa.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola
akichangia taarifa hizo aliwashukia mawaziri watatu kwa wakati mmoja
akieleza kuhusika kwao kukwamisha baadhi ya mambo huku akisema migogoro
ya ardhi nchini haitakwisha kama viongozi ndiyo wanaohusika kulinda
baadhi ya watu.
“Wako viongozi wanahodhi ardhi na kusababisha matatizo, mwekezaji wa Oysterbay Villa, Lukuvi ndiye alimsaidia kupata eneo alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,” — Kangi Lugola.
“Sasa
leo amekuwa Waziri wa Ardhi, itakuwaje? Mimi nitaichoma moto mbeleko
inayombebea huyu mwekezaji kitendo kinachozuia Kinondoni kupata Sh3
bilioni. Huyu mwekezaji ana kiburi alizuia hata kamati kutaka kuingia
kwenye eneo hilo lakini nikatumia ubaunsa wangu tukaingia.”
Hata hivyo, hoja ya Lugola kuhusu Lukuvi na mwekezaji huyo ilipingwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe ambaye alisema waziri huyo alisaidia hata kubadilisha mkataba wa umiliki wa Oystebay Villa, hivyo amwache.
Lugola akiendelea kuchangia alimshukia Waziri Maghembe
kwamba anapeleka maji katika eneo lake tu wakati wananchi wa jimbo la
Mwibara na Bunda wakiteseka kwa mradi wao wa maji kutokukamilika.
MWANANCHI
Madaktari katika Chuo cha Tiba cha Amrita, Kochi huko India wamefanikiwa kufanya upasuaji wa aina yake wa kupandikiza mikono mipya kwa binadamu aliyekatika viungo hivyo.
Upandikizaji huo uliofanyika Januari 12
na 13, ulifanikiwa kwa mara ya kwanza, baada mwanamume mwenye umri wa
miaka 30, aliyekatika mikono katika ajali ya treni kuwekewa mingine.
Mikono hiyo mipya ilichukuliwa kutoka kwa kijana wa miaka 24 aliyepata
aliyefariki katika ajali ya gari.
Mkuu wa kitengo cha upasuaji katika chuo hicho, Prof. Subramania Iyer alisema; “Siku
14 baada ya upasuaji, mikono ilikubaliwa na mwili na ikaanza kujongea,
yaani aliyepandikizwa aliweza kuisogeza huku na kule. Mgonjwa alitolewa
chumba cha wagonjwa mahututi na huduma nyingine za kumchunguza
ziliendelea.”
Daktari katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Muhimbili (MoI), Prof. John Kahamba
alisema hiyo si mara ya kwanza kwa upandikizaji wa mikono kufanyika
duniani kwani na tofauti kubwa na upandikizaji wa figo au ini.
Prof. Kahamba
alisema upasuaji huo unafanyika kwa kuhakiki mambo mbalimbali ikiwamo
uwiano wa kundi la damu, uhai wa seli na misuli na mishipa midogo ya
fahamu.
“Upasuaji
mkubwa hufanyika, pamoja na kuangalia uwiano wa damu lakini lazima jopo
la madaktari wenye kazi tofauti lifanye kazi kwa pamoja. Kwa mfano,
wanaounganisha misuli na mishipa midogomidogo na hata wale wa kuhakiki
uhai wa seli“– Kahamba.
Prof. Kahamba alisema kama upandikizaji wa figo unavyofanyika, kadhalika upandikizaji wa mikono unahitaji umakini wa muda.
Anasema iwapo utachelewa kuunganisha
mikono baada ya kuitoa, seli zake zinaweza kufa na kushindwa kufanya
kazi zitakapopandikizwa kwenye mwili.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amekabidhi madaraka ya Uratibu wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika ya Mazingira (CAHOSCC) kwa Rais wa Misri, Jenerali Abdel Fatteh El Sisi.
Rais Kikwete
alibeba jukumu la uratibu wa CAHOSCC miaka miwili iliyopita baada ya
kifo cha aliyekuwa mratibu wa kamati hiyo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais Kikwete
alikabidhi jukumu hilo Januari 31 na kuwatahadharisha viongozi wa
Afrika juu ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye sekta ya
kilimo barani Afrika.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Kikwete
aliwapongeza viongozi wengine wa Afrika wakati wa mkutano wa 24 wa
Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa kwa kupata mafanikio wakati wa uongozi
wake.
Kikwete
alibainisha changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika kwenye
mabadiliko ya tabia ya nchi na kutaka ushirikiano kati ya nchi
zilizoendelea ambao ndiyo wachafuzi wakubwa wa mazingira na nchi
zinazoendelea kutoka Afrika.
NIPASHE
Wimbi la uvamizi na uporaji wa silaha
kwenye vituo vya polisi limeendelea kushamiri safari hii likiamia mkoani
Morogoro kwa kituo kidogo cha Polisi Mngeta, kilichopo Wilaya ya
Kilombero, kuvamiwa na kuporwa bunduki moja aina ya SMG na magazine moja
yenye risasi 30.
Tukio la Morogoro lilitokea juzi majira ya saa 9:30 usiku na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamtafuta kijana mmoja, Emmanuel Shewele (21) kwa tuhuma za kusababisha kuvunjwa kwa kituo hicho.
Mbali ya silaha hizo, wavamizi hao
waliiba vielelezo vya ushahidi ili kupoteza ushahidi wa kesi zake
kufuatia kushtakiwa mahakamani kwa kesi zaidi ya tano.
Kamanda wa Polisi Morogoro, Leonard Paulo,
alitaja vielelezo kuwa ni genereta moja, viti vinne vya plastiki, redio
moja aina ya sabufa, betri ya gari moja na spika moja ya redio.
Alisema tayari watuhumiwa watatu wamekamatwa ambao ni Ramadhani Shewele (20), Hamisi Hamidi (45) na Egnas Shewele (34), huku wakiendelea kumtafuta Emmanuel Shewele (21) wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha Nakaguru A, wilayani humo.
NIPASHE
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola
amesema atawashawishi wananchi wasikichague Chama Cha Mapinduzi (CCM)
katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba mwaka huu ikiwa
serikali haitatekeleza miradi ya kupekeleka maji katika Wilaya ya Bunda
mkoani Mara na hasa jimboni kwake.
Lugola
aliyasema hayo jana, wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya
utekelezaji ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na ile ya Kilimo,
Mifugo na Maji baada ya kuwasilishwa bungeni jana.
Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la maji
kutoka Tamau hadi Bunda ambao pia unakusudia kuvipatia maji vijiji vya
Bulamba Bizimbwe na Mwisenye umekuwa kizungumkuti kwa muda mrefu sasa.
Alisema inasikitisha kwenye kitabu cha taarifa ya Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Magembe hajaweka mradi huo na badala yake ameweka miradi mingi ya kwenye jimbo lake.
“Na
hata kwenye kitabu hiki cha taarifa yake Mheshimiwa Waziri, Hakuna mradi
huu wa maji ya Bunda, mradi mkubwa, lakini ukienda kwenye miradi yake
ya Same, Mwanga ndiyo imejaa kwenye kitabu hiki, kwa nini nisiamini
unafanya kazi kwa kupendelea maeneo yako“–Lugola.
Alisema wakazi wa Bunda wanahitaji maji
hayo kutoka Ziwa Victoria lilipo umbali wa kilometa 20 lakini mpaka
sasa ni zaidi ya miaka sita tangu mradi huo uasisiwe hawajapata.
Alisema kwa sasa taifa linaelekea kwenye uchaguzi ambao anaamini CCM kitaendelea kushinda kwa kishindo kwa kuwa Rais Kikwete amefanya mabadiliko ya mawaziri ambayo alitaka sasa yawe ni mabadiliko yenye tija.
Hata hivyo alimtaka Maghembe
kufanya mabadiliko haraka ya miradi ya maji kwa kuwa wakazi wa Bunda
akiwemo mwenyewe hawatakubali kuipigia CCM kura ikiwa hawatapata maji
mpaka kufikia kwenye uchaguzi huo.
MTANZANIA
TUME ya Utumishi wa Mahakama imesema
suala la majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wanaotuhumiwa kupokea zaidi
ya Sh milioni 400 kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow, limefika
kwenye tume hiyo na linafanyiwa kazi.
Kwa utaratibu wa tume hiyo, baada ya
uchunguzi taarifa hupelekwa kwa rais ambaye baada ya kupitia mapendekezo
yaliyotolewa kwenye ripoti ya uchunguzi, hutoa uamuzi.
Hayo yalielezwa jana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Hussein Katanga,
katika banda la Tume ya Utumishi wa Mahakama katika maonyesho ya Wiki
ya Sheria yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.Majaji wanaotuhumiwa kuingiziwa fedha hizo ni Prof. Eudes Ruhangisa (Sh milioni 404.25) na Aloysis Mujulizi (Sh milioni 40.4).
“Huo
ni ukweli, inatakiwa uwepo uwazi zaidi…Tunatakiwa kuwa wazi, hivi sasa
tunataka kuweka mabango wananchi wajue jinsi ya kupata haki kuepusha
rushwa“– Katanga.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Mahakama za Mwanzo, Warsha Ng’humbu aliyekuwapo
katika banda la Kurugenzi ya Ukaguzi, Malalamiko na Maadili, alisema
kwa kuwa suala hilo limefika kwenye tume, maana yake lilishapita katika
Kamati ya Maadili ya Majaji.
Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Enzeel Mtei alisema
tume hiyo inaundwa na wajumbe sita na ina jukumu la kumshauri rais juu
ya uteuzi wa Jaji Kiongozi au majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment