Tangakumekuchablog
Tanga, WAKAZI
wa mtaa wa Magaoni A kata ya Mabawa Tanga, wameitaka halmashauri ya jiji la
Tanga kumuamuru mkandarasi wa ujenzi zahanati ya Magaoni kwa kulifunika shimo
la choo ili kuepusha maafa kwa watoto na kuongezeka kwa mazalia ya mbu.
Wakizungumza na tangakumekuchablog eneo la tukio kufuatia kutumbukia mtoto katika shimo la choo la Zahanati
ya Magaoni jana, wakazi hao walisema shimo hilo lipatalo mita kumi yapata mwaka mmoja toka lichimbwe na
mkandarasi kutokomea kusikojulikana.
Walisema shimo hilo limekuwa kero
baada ya kuzalisha mazalia ya mbu na
kusababisha wakazi wa mtaa huo kuugua homa zisizoisha na hivyo kumtaka
mkurugenzi wa jiji kumuamuru mkandarasi kumalizia kazi yake kwa kulifukia.
“Toka zahanati hii imalizike kujengwa
haina faida yoyote kwetu kwani limebakia kama gofu----haina umeme wala
miundombinu ya maji na zaidi mkandarasi amechimba shimo na kujaa maji na
kuzalisha mazalia ya mbu” alisema Zubeda Said
“Leo asubuhi kuna mtoto ametumbukia
katika shimo eti anavua kambare---Mungu amemnusuru tu baada ya majirani kusikia
kelele zilizokuwa zikisikika katika shimo na kuokolewa na hivi sasa yuko hospitali
amelazwa Bombo” alisema Zubeda
Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto
alietumbukia katika shimo, Halima
Athumani, alisema shimo hilo limekuwa kero na nyakati za usiku sauti za vyura na
mbu hupiga kelele na kuwa kero.
Alisema mtaa huo haukuwa na mbu wengi
kama ilivyo sasa na hivyo kuwa na hofu ya kuzuka kwa magonjwa ya miripuko
yakiwemo ya malaria na matumbo na kuwataka viongozi wenye dhamana kulipatia
ufumbuzi.
“Nyakati za usiku hatulali kwa sauti
za vyura na mbu wengi na kuwa kero----ifikapo usiku huwa tunaingiwa na hofu na
kutokuwa na raha jambo ambalo tunajilazimisha kulala mapema japo hatuko tayari
kufanya hivyo” alisema Halima
Akizungumzia kero hiyo, Mwenyekiti wa
mtaa, Ramadhani Malodi, alisema malalamiko hayo ya wananchi ameshayafikisha
katika ngazi husika na kushangazwa hadi muda huo hakuna utekelezaji wowote.
Alisema pia taarifa ya kutumbukia
mtoto katika shimo la choo la kituo cha zahanati amelifikisha na kuarifu kuwa
ni vyema kufukiwa au kumaliziwa kwa kusakafiwa ili kuondosha kitisho cha maafa
kwa watoto.
“Kero zote za wananchi zilizokuja katika ofisi yangu nimezifikisha
kwa wahusika---mimi hapa nimewekwa na wananchi na niwajibu wangu kila
nifikishiwalo nalifikisha kwa wahusika” alisema Malodi
Akizungumzia kuhusu wananchi kuweka
mazingira ya usafi, Mwenyekiti huyo aliwataka kila mmoja kuhakikisha eneo lake
linakuwa katika usafi muda wote wa kazi ili kuepusha magonjwa ya miripuko
kuelekea kuipindi cha mvua za masika.
Alisema ameweka utaratibu wa kila
kaya kuhakikisha eneo lake linakuwa katika usafi na kuwa na chombo maalumu cha
kuhifadhia pamoja na kuisafisha mifereji ya maji taka.
Mwisho
No comments:
Post a Comment