HADITHI
YALIYONIKUTA TANGA (13)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Sote tukasimama. Kila polisi
akachukua bunduki yake.
Tulishindwa hata kujibu,
tukawa tunatazamana.
“Vipi jamani, mbona mmelala
hapa” Inspekta Amour akatuuliza tena.
Polisi mmoja akaeleza
kilichotutokea. Polisi hao waliokuja wakashangaa.
Waliusogelea mwili wa Sajenti
Erick na kuutazama.
“Huyu ndiye Sajenti Erick”
Amour akasema baada ya kuutazama mwili huo. Akaongeza.
“Sasa nini kilitokea?”
“Ni miujiza mitupu” nilijibu
mimi.
“Hiyo nyumba imetowekaje?”
“Hatujui. Muda huu
tunazinduka tunaona nyumba haipo”
“Ilikuwa kwa wapi”
“Sisi tulikuwa uani mwa hiyo
nyumba. Lile gari tulilokuja nalo lilikuwa mbele ya nyumba” polisi mwingine
alijibu.
SASA ENDELEA
“Kwa hiyo nyumba ilikuwa hapa
katikati?”
“Ndiyo. Ilikuwa kati ya sisi
na lile gari” nikajibu.
“Sasa wale watu mnaosema
mliwaona, wako wapi?”
“Hawapo tena, tumezinduka
hatuwaoni” koplo akajibu yeye.
“Walikuwa ni watu wa aina
gani?”
“Wale si watu, wale ni
majini” nikasema na kuongeza.
“Wale ndio wamemuua Sajenti
Erick. Yule mwanamke ndiye tuliyemkamata siku ile kwa tuhuma za kukutwa na
madawa ya kulevya”
“Lakini yule mwanamke
alikufa?” Amour akasema.
“Kwa kweli tumemuona na ndiye
aliyetupungia mkono, sote tukapotewa na fahamu” Koplo akaeleza.
Inspekta Amour akaguna na
kutupa mcho huku na huku.
“Yule binti yake ambaye
aliwatoroka alikuwa pamoja naye?” akatuuliza tena.
“Walikuwa wote pamoja na
mwenzao mwingine mwanaume” nikasema.
Nilitupa macho chini
nikayaona yale magazeti ambayo niliyachukua mle chumbani. Nikainama na
kuyachukua.
“Haya magazeti yana habari ya
yule mwanamke, niliyakuta katika chumba alichochinjwa Erick”
Nilikunjua gazeti mojawapo
nikampa Inspekta Amour. Amour alilichukua na kulitazama. Nilimpa na lile gazeti
jingine nalo akalitazama.
“Itakuwa ni yeye kweli”
alisema baada ya kusoma vile vichwa vya habari.
Pembeni na eneo hilo kuliwa na watu
wamesimama wakitutazama. Inspekta Amour alimuita mtu mmojawapo. Mtu huyo
alikuja kwa uoga akasimama kando ya Inspekta Amour.
“Wewe ni mwenyeji wa eneo
hili?” Amour alimuuliza.
“Sisi tunaishi kule kando,
hapa tunapita njia tu” Mtu huyo alijibu huku akionesha kuwa na wasiwasi
“Eti hapa mahali pana
nyumba?”
“Hili ni eneo la makaburi tu,
hakuna nyumba” Mtu huyo akamjibu.
“Hujawahi kuona nyumba mahali
hapa jana au juzi?”
“Sijawahi kuona nyumba”
“Sisi tulikuta nyumba
tulipokuja usiku” Koplo akasema.
“Eneo hili ni la makaburi tu”
Yule mtu alisisitiza.
“Kwani jana usiku ulifika
hapa?” Amour aliendelea kumuuliza.
“Jana sikuwahi kufika,
nilipita leo alfajiri nikaona hawa polsi wamelala hapa, nikaona na ule mwili
umekatwa kichwa…”
Alionesha mwili wa Sajenti
Erick.
“Nani aliyepiga simu polisi?’
“Ni mimi. Nilipiga simu baada
ya kuwaona hawa polisi wamelala hapa na pia ni baada ya kuona mtu aliyekatwa
kichwa”
Inspekta Amour akatutazama.
“Huu ni mkasa mzito, huyu mtu
tutamchukua kwa ajili ya ushahidi. Sasa tukibebe hiki kiwiliwili tukiingize
kwenye gari”
Baada ya Inspekta Amour
kutuambia hivyo tulikibeba kile kiwiliwili cha Sajenti Erick na kukiingiza
kwenye gari tuliyokwenda nayo usiku.
“Tutarudi tena kwa ajili ya
kulipiga picha hili eneo” Inspekta Amour akatuambia na kumuomba yule mtu
aliyemuita tuende naye polisi ili akaandikishe maelezo yake na kisha
angerudishwa kwa gari la polisi.
Baada ya hapo sote tulipanda
kwenye magari tukaondoka. Kwa mbali nilihisi kichwa kikiniuma na ile hofu ya
usiku bado ilikuwa ikitambaa kwenye mishipa yangu.
Nilijua nilipata hali hiyo
kutokana na kutolala usiku kucha pamoja na lile taharuki la usiku. Lazima
kichwa kiume na lazima mwili usisimke kwa hofu.
Tulifika kituo cha polisi
tukashuka kwenye gari. Tulimkuta kamanda wa polisi na afisa upelelezi wakitusubiri.
Inspekta Amour alikuwa amewapigia simu tukiwa ndani ya gari.
Mara tu tuliposhuka kwenye
gari, maafisa hao walisogea kenye gari lililokuwa na kiwiliwili cha Sajenti
Erick na kukitazama.
“Kichwa chake kiko wapi?”
Kamanda wa polisi akauliza.
“Kichwa chake hakikupatikana”
Inspekta Amour alimjibu.
Kamanda wa polisi akakunja
uso.
“Kwani ilikuwaje? Hebu njoo
huku ndani utueleze”
“Martin twende” Inspekta
akaniambia.
Tukaingia ndani ya kituo.
Kamanda wa polisi alituita kwenye ofisi ya mkuu wa kituo. Yeye na afisa
upelelezi walikaa. Sisi tukawa wima.
“Hili tukio ni kubwa hebu
tupeni maelezo, nini kilitokea?” Kamanda wa polisi akatuambia.
Inspekta Amour alieleza kwa
upande wake. Alieleza nilivyompigia simu saa tisa usiku na kuomba msaada wa
polisi.
“Alituambia yuko Magomeni na
kwamba alitoroka kutoka katika nyumba moja ambako aliukuta mwili wa Sajenti
Erick umekatwa kichwa. Na kwamba yeye mwenyewe pia amenusurika kukatwa kichwa
na bado hayuko salama.
“Mimi baada ya kupata habari
hii nilipata hofu kidogo nikatuma gari na askari sita muda ule ule. Ukapita
muda wa kama nusu saa hivi Martin akanipigia
simu tena akaniambia lile gari la polisi limempita, hawakumuona. Nikawapigia
kuwajulisha kuwa wamempita Martin, warudi nyuma”
“Baada ya hapo kukawa kimya.
Nilijaribu kupiga simu tena kuwaulizia lakini simu ikawa haipokelewi. Ilipokuwa
inakaribia kuwa asubuhi mtu mmoja alitupigia simu akatuambia ameona polisi
wamelala juu ya makaburi na kuna mtu mmoja amekatwa kichwa.
“Hapo nilichukua askari na
gari na kuelekea eneo la tukio. Tulizunguka sana
hadi tukafika katika eneo hilo.
Tuliwakuta askari wamelala kwenye eneo la makaburi na kiwiliwili cha Sajenti
Erick kipo hapo hapo”
Inspekta Amour aliendelea
kueleza jinsi walivyotuona tukizinduka na kutuhoji maswali na sisi tukaeleza
kilichotutokea.
Je nini kitafuata? Usikose
kuendelea na hadithi hii hapo kesho.
Niko tayari kukupatia kila kinachonifikia mtu wangu muda na wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment