Thursday, February 12, 2015

YALIYONIKUTA TANGA (15)

HADITHI
 
YALIYONIKUTA TANGA (15)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Kamanda akanyamaza na kututazama. Kikapita kimya kifupi kabla ya kukitanzua kimya hicho.
 
“Sasa andikisha maelezo yake, yatawekwa kwenye faili la marehemu pamoja na maelezo yenu nyote” Kamanda akamwambia Inspekta na kunigeukia mimi.
 
“Wewe utatupeleka katika hilo eneo, tutachukua mpiga picha” akaniambia.
 
Wakati Inspekta anachukua maelezo ya yule mwananchi, kamanda wa polisi na afisa upelelezi walitoka nje ya kituo wakakikagua tena kiwiliwili cha Sajenti Erick kabla ya kuamuru kipelekwe hospitali kwa uchunguzi zaidi.
 
Baada ya hapo aliitwa mpiga picha wa polisi. Dakika chache baadaye kamanda wa polisi, afisa upelelezi, mpiga picha wa polisi na mimi tulikuwa kwenye gari tukielekea katika eneo lilipotokea tukio.
 
Nikiwa ndani ya gari nilikuwa nimeinamisha kichwa changu kwa mawazo. Tukio hilo lilikuwa limenitia fadhaa sana na sikujua hatima yake ingekuwa nini.
 
Hofu yangu ilikuwa kuzuiwa likizo yangu ambayo ningeianza siku mbili tu kutoka siku ile.
 
SASA ENDELEA
 
Tulipofika katika lile eneo tulishuka kwenye gari, nikawaonesha maafande wangu mahali ilipokuwa ile nyumba.
 
“Nyumba ilikuwa hapa” niliwambia.
 
“Kwa sasa ndiyo imeyayuka?” Kamanda akauliza.
 
“Ni kama imeyayuka afande kwa maana tulipozinduka hatukuiona tena”
 
“Na hilo kaburi lililokuwa na mwili wa marehemu Erick ni lipi?”
 
Nikawaonesha kaburi hilo ambalo lilikuwa wazi.
 
“Ni hili hapa”
 
Kamanda akamwambia mpiga picha wa polisi apige picha eneo hilo.
 
“Hili kaburi lilioko wazi utalipiga picha peke yake” aliendelea kumueleza.
 
Wakati mpiga picha huyo akiendelea kufyatua picha., afisa upelelezi alimwambia.
 
“Na hii sehemu inayodaiwa ilikuwa nyumba usisahau kuipiga picha. Jaribu kupiga picha nyingi zaidi kwa sehemu tofautu tofauti”
 
Tuliwa tumesimama katika eneo hilo huku kamanda wa polisi akiendelea kunihoji na picha zikiendelea kupigwa, watu mmojammoja walianza kufika na kutuangalia wakiwa wamesimama kwa mbali.
 
Afisa upelelezi aliwaita wakasogea karibu.
 
“Nyinyi ni wenyeji wa eneo hili?” akawauliza.
 
“Ndio ni wenyeji wa eneo hili” Kijana mmoja akamjibu.
 
“Nini kilitokea asubuhi hapa?”
 
“Palikuwa na polisi waliokuwa wamelala juu ya makaburi”
 
“Wewe uliwaona?”
 
“Watu waliokuwa wakipita njia wote waliwaona”
 
“Na labda mlijua polisi hao walilala juu ya makaburi kwa sababu ya nini?”
 
“Hatukujua lakini polisi wengine walifika asubuhi wakawaona”
 
“Eti hili eneo lina historia gani?”
 
“Historia ya namna gani?”
 
“Inasemekana kuna miujiza inatokea katika eneo hili ni kweli?
 
“Ni kweli. Siku nyingine ukipita usiku hapa unakuta mambo ya ajabu”
 
“Kama mambo gani?”
 
“Unaweza kukuta watu wamekaa wanasoma wamevaa nguo nyepe tupu au unaweza kukuta mwanamke mrefu ananyonyesha mtoto wake”
 
“Sasa nyinyi wenyeji wa hapa mnayachukuliaje matukio kama hayo?”
 
“Hapa mahali kwa kweli kuna majini. Wale polisi tuliowakuta wamelala hapa asubuhi bila shaka walikumbwa na majini hao”
 
Mwanamke mmoja aliyekuwa akisikiliza mazungumzo hayo aliingilia.
 
“Pana jini anaitwa Maimuna na mama yake anaitwa Fatuma. Kuna siku wanaonekana lakini hawadhuru mtu”
 
“Hao majini wanapatikana kwa wapi?”
 
“Eneo lao ndilo hili hapa lakini huwezi kuwaona mpaka usiku”
 
“Usiku ndio wanaonekana?”
 
“Mara moja moja wanaonekana”
 
“Sawa. Asante sana”
 
Afisa upelelezi akamgeukia kamanda wa polisi.
 
“Kinachonishangaza mimi ni kuwa maelezo ya polisi waliokuja huku ni kwamba yule mwanamke waliyemuona ni yule aliyekamatwa na kete za madawa ya kulevya na kufia mahabusi, sasa swali ninalojiuliza muda wote je majini wanafanya biashara ya madawa ya kulevya?”
 
“Au si majini ni watu?” Kamanda naye akauliza swali lake.
 
“Hapana ni majini kama wanavyosema hawa wenyeji wenyewe. Huyo Maimuna ndiye yule msichana niliyewaeleza na yule mwanamke alituambia jina lake anaitwa Fatuma kama alivyotueleza huyu msichana hapa” nikasema.
 
“Kwa hiyo siku ile nyinyi mlikamata majini?” Kamanda aliniuliza.
 
“Ndio, wale walikuwa majini” nikasisitiza.
 
“Majini pia wanafanya biashara ya madawa ya kulevya?’
 
Hapo sikuwa na jibu kwa sababu yale madawa ya kulevya, Sajenti Erick aliwabambikia tu.
 
“Itabidi tufanye uchunguzi wa kuthibitisha kama ni kweli hao majini ndio walikuwa wakazi wa ile nyumba ya barabara ya nane alipokamatwa yule mwanamke” afisa upelelezi akasema.
 
“Sasa suala la msingi ni kutafuta ile nyumba ni ya nani na kama tutakuta watu mle ndani wahojiwe ili watoe maelezo” Kamanda akaongeza.
 
“Sisi tunachofahamu ni kuwa wanaojenga nyumba au kupangisha ni watu. Sasa kama majini pia wanamiliki nyumba au kupangisha tutakwenda kujua vizuri” afisa upelelezi akasema.
 
Baada ya hapo tulirudi kwenye gari tukaondoka. Kichwa changu kilikuwa kimevurugika sana. Ile kesi ilikuwa kama imenilemelea mimi. Hoja za maafande wangu zilikuwa zikinitibua mtima. Nikahisi kama vile mwisho wa siku nitakamatwa na kushitakiwa mimi.
 
Nilikuwa na hamu ya kuwaona wazazi wangu na ndugu zangu huko kwetu Kagera lakini likizo yangu ilikuwa kwenye hatari ya kufutwa kutokana na uchunguzi huo.
 
Sikudhani kama polisi wangeniruhusu niende likizo wakati kulikuwa na tukio la uchunguzi kama lile ambalo lilikuwa linanihusu sana.
 
Kwa kweli nilifikia mahali nilijuta kutaka kuanzisha uhusiano na yule msichana ambaye sikuwa nikimfahamu. Matokeo yake ndio hayo ya kukumbwa na mkasa ulioyatatanisha maisha yangu.
 
Nilijua kuwa kama polisi watashindwa kuyathibitisha maelezo yangu watanihusisha mimi na mauaji ya Sajenti Erick. Na kama nitahusishwa na mauaji hayo ni wazi kuwa nitashitakiwa mimi kwa kufunguliwa kesi ya mauaji.
 
Je nini kitaendelea? Usikose kufuatilia hadithi hii hapo kesho.
 
Nitahakikisha nakufikishia kila linalonifikia mtu wangu muda na wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment