Thursday, February 12, 2015

BODABODA TANGA WACHACHAMAA USAJILI WA NAMBA ZA PIKIPIKI



Tangakumekuchablog

Tanga, WAFANYABIASHARA  wa Pikipiki maarufu kama bodaboda Tanga, wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza muda wa usajili wa namba za pikipiki vyenginevyo watasitisha utoaji wa huduma barabarani.

Wakizungumza  katika kongamano la kujadili changamoto zinazoikumba sekta hiyo, madereva hao wamesema muda uliowekwa wa kubadilisha namba za pikipiki ni mdogo na hivyo kutaka kuongezwa.

Walisema endapo Mamlaka haitoweza kuongeza muda watasitisha utoaji wa huduma kutokana na wamiliki wengi kuwa na pikipiki zaidi ya moja na hivyo kushindwa  kumudu gharama za usajili.

Wameshauri ni vyema zoezi hilo kuongezwa miezi sita zaidi ili kuwapa nafasi wamiliki kubadilisha vyombo vyao na kuacha kuingia katika mgogoro na madereva  jambo ambalo linaweza kuwaathiri watumiaji wa kipato cha chini.

“Vipato vyetu kwa siku ni vidogo tofauto na wamiliki wa magari na utakuta baadhi ya siku kunabeba abiria watu au watano ambao hawakidhi mahitaji ya chombo wala ya familia zetu” alisema Bakari Kimwaga

“Serikali inalazimka kuangalia vipato vyetu tunavyopata kwani kuna baadhi ya watu wengine wanamiliki pikipiki zaidi ya tatu na ukiangalia muda uliowekwa ni mdogo----tunaomba kuongezewa muda zaidi” alisema

Akizungumza katika kongamano hilo  mmiliki  wa bodaboda mbili, Rajab Shamte, alisema kuweka muda maalumu wa mwisho wa kubadilisha namba hizo ni ukandamizaji na kupendekeza pikipiki mpya ndizo ambazo zinatakiwa kuwa utaratibu huo.

Alisema kuna vyombo vingi ambavyo baadhi yake vimekuwa chakavu  na wamiliki wake wanaweza kushindwa kumudu gharama za usajili na hivyo kuwawia vigumu.

Alisema  ili kuwapa unafuu wamiliki wa pikipiki ni vyema Mamlaka ya Mapato Tanzania kuongeza muda wa usajili vyenginevyo  wanaweza kuingia mzozo na madereva.

                                              Mwisho

No comments:

Post a Comment