HADITHI
YALIYONIKUTA TANGA (16)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Kwa uzoevu wa kipolisi
niliokuwa nao kesi za mauaji ya aina ile uhusishwa na imani za kishirikina na
aghalabu ukipatikana na hatia hukumu yake ni kunyongwa.
Nilikuwa bado kijana mdogo sana. Nilikuwa sijaoa na
wazazi wangu walikuwa wakinitegemea. Kama
nitanyongwa litakuwa ni pigo kwa familia yangu.
Tulirudi kituo cha polisi.
Timu nyingine ya polisi ikatakiwa kwenda kwenye ile nyumba ya barabara nane
kujua kama mle ndani kulikuwa na watu wanaoishi na kama
wamo watoe maelezo kuhusiana na ile nyumba na kuhusiana na yule mwanamke
aliyekuwa na duka la vitu vya dhahabu.
Kwa bahati njema na mimi
niliingizwa katika msafara huo kwa vile ndiye niliyekuwa nikiifahamu vizuri
nyumba ile kutoka siku ile tuliyomkamata yule mwanamke.
Tulipofika katika nyumba
hiyo, lile duka lilikuwa bado limefungwa. Kiongozi wa msafara wetu Meja Elias
alibisha mlango. Lakini hatukupata jibu.
“Nadhani hakuna watu humu
ndani” akasema baada ya kubisha sana.
“Tunaweza kuwauliza majirani
kuhusu wenyeji wa nyumba hii” polisi mwingine akashauri.
SASA ENDELEA
Nyumba tuliyokuwa tunaifanyia
utafiti ilikuwa katikati ya nyumba mbili. Tulikwenda katika nyumba iliyokuwa
upande wake wa kulia, tukabisha mlango.
Mwanamke mmoja alitoka ndani
kuja kutusikiliza lakini alipoona polisi uso wake ulinywea hapo hapo.
“Habari ya saa hizi?” Meja
Elias alimsalimia.
“Nzuri. Karibuni” Mwanamke
huyo akatukaribisha bila uchangamfu.
“Samahani. Tuna tatizo
kidogo. Tunaomba msaada kutoka kwa majirani wa nyumba hii” Meja alimwambia.
“Msaada gani?”
“Tulitaka kujua hii nyumba ni
ya nani?” Meja alimuuliza akimuonesha ile nyumba.
“Hiyo nyumba mwenyewe alikufa
zamani. Wakati huo sisi tulikuwa wadogo. Hatumjui vizuri”
“Alikuwa ni nani?”
“Alikuwa ni bibi mmoja wa
kisomali”
“Hivi sasa wanaishi watu
gani?”
“Kuna mama mmoja kama muarabu hivi na binti yake ndio waliokuwa wakiishi
humo ndani lakini siku hizi hatuwaoni tena”
“Huyo mama alikuwa
amepangisha au…?”
“Hapo hatujui”
“Kwa hiyo kwa sasa hivi hii
nyumba haikai watu?”
“Kwa mchana hatuoni watu
wanaoingia wala kutoka, inakuwa kimya tu lakini ikifika usiku mwingi tunasikia kama watu wamo ndani”
Meja alipojibiwa hivyo
akatutazama.
“Sasa nyinyi majirani
mnaelewa nini mnaposikia kama kuna watu wakati
wa usiku mwingi lakini mchana hamuwaoni?” Meja akaendelea kumuuliza yule
mwanamke.
“Hatuelewi kitu, hapa ni
mjini hatuchunguzani”
“Usiku wa jana mliwasikia hao
watu?”
“Ni kila siku usiku”
“Mnawasikia kuanzia saa
ngapi?”
“Kuanzia saa nane usiku ndio
sauti zinaanza kusikika, zinaendelea hadi saa kumi alfajiri”
“Mnahisi ni sauti za
binaadamu au…?”
“Ni za binaadamu”
“Labda tuseme wenyewe
wanakuja usiku na kuondoka alfajiri?”
“Labda”
Pakapita kimya kifupi kabla
ya Meja kumwambia yule mwanamke.
“Asante
sana, kama
tutakuwa na maswali mengine tutakuja kukuuliza”
“Haya karibuni”
Tukaondoka.
Tulipofika kituo cha polisi tukaanza
kufanya mchanganuo wa mazungumzo yetu na yule mwanamke. Polisi walibaini kwamba
ingawa wenyeji wa nyumba ile hawakuwa wakitambulika, kulikuwa na
hali isiyo ya kawaida kwa wenyeji hao.
Imani kuwa wenyeji hao
hawakuwa watu wa kawaida na ndio wale waliotufanyia vitisho kule Magomeni
ilianza kuwaingia polisi, hali ambayo kwa upande wangu nilihisi ingeweza
kunipatia ahueni.
Kwa vile polisi ni chombo cha
dola na kunaendesha shughuli zake kisheria ukawekwa mkakati mwingine wa kwenda
usiku katika nyumba ile ili kuonana na hao watu ambao sauti zao zinasikika
wakati wa usiku.
Tulipanga twende tukakae
kando kidogo kuanzia saa saba ili tuone kama
kutakuwa na watu wakiingia. Ikifika saa nane tusogee karibu. Kama
tutazisikia hizo sauti tubishe mlango.
Mkakati huo ulipokubalika
nikaambiwa kwamba naweza kwenda kupumzika na nionekane tena hapo kituoni
kuanzia saa sita usiku. Nikashukuru kuona sikuwekwa ndani. Nilikuwa nimechoka sana na nilikuwa na
usingizi. Akili yangu ilikuwa haifanyi kazi kabisa.
Nikarudi nyumbani.
Nilipoingia chumbani kwangu kwanza nilikitoa mvunguni kile kisanduku
kilichokuwa na mapambo ya dhahabu, nikakifungua na kukiangalia ndani. Nilipoona
dhahabu zilikuwemo, nikakifunga na kukirudisha mvunguni.
Nilikwenda kuoga. Nilipotoka
bafuni nikajitupa kitandani. Ingawa kichwa kilikuwa kizito kwa usingizi lakini
mawazo hayakunipa nafasi ya kulala. Yale matukio ya majini si tu yalinitia
wasiwasi bali pia yalinipa hofu ya kufungwa.
Nilihisi maisha yangu
yalikuwa hatarini kwa namna mbili. Kwanza ni endapo wale majini wataendelea
kuniandama ili wanimalize kama walivyommaliza
Sajenti Erick. Na pili ni endapo polisi wataamua kunikamata mimi na kunishitaki
kuhusiana na mauaji ya Sajenti huyo.
Mawazo hayo ndiyo
yaliyonikosesha usingizi japokuwa sikuwa nimelala usiku kucha uliopita nikiwa
kwenye kizaa zaa cha majini hao.
Nilisali, niliomba Mungu na
hatimaye usingizi ulinipitia bila kujua. Wakati niko kwenye usingizi niliota
nikimuona Sajenti Erick akichinjwa, mwili wake usio na kichwa ukawa unanijia
machoni mwangu.
Picha ya kuchinjwa kwake
ilinijia kama sinema kwenye ndoto hiyo.
Alikuwa amefungwa kamba mikono na miguu.
Yule mwanamke wa kijini
alikuwa amemshikia upanga akamuuliza.
“Kwanini mlituzushia kesi
mimi na mwanangu?”
Sajenti Erick hakuwa na la kusema
zaidi ya kuomba msamaha aachiwe.
“Kisanduku changu cha dhahabu
kiko wapi?” Mwanamke aliendelea kumuuliza.
“Sijachukua kisanduku” Erick
alijibu.
“Unajua kafara lako ni nini?”
“Sijui”
“Ni kuchinjwa kama kuku, damu yako itakuwa fidia yako”
Hapo hapo upanga ukapita
kwenye shingo ya Erick. Erick alianza kukoroma na kutoa macho. Upanga
uliendelea kukeketa shingo yake taratibu. Mkoromo wa Sajenti Erick wakati
anachinjwa ndio ulioniamsha usingizini.
JE NINI KITATOKEA? Usikose
kuendelea na hadithi hii hapo kesho.
Usiache kuperuzi blog hii kila wakati kwa habari motomoto na za papo kwa papo mtu wangu
No comments:
Post a Comment