Monday, October 12, 2015

MUSSA WA CUF ADAI KUIFUFUA BANDARI NA VIWANDA TANGA



Tangakumekuchablog
Tanga,MGOMBEA Ubunge jimbo la Tanga mjini, Mussa Mbarouk (CUF), amesema endapo atachaguliwa kuwa mbunge atahakikisha shehena za meli za mafuta na upakuzi  wa mizigo bandari ya Tanga unafanyika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana, kata ya Magomeni, Mussa alisema njama zote za kuzuia matumizi ya bandari ya Tanga atazizuia ukiwemo wa ushushaji wa mafuta bandarini hapo.
Alisema hakuna sababu kwa wafanyabiashara kushusha shehena zao kupitia bandari ya Dar es Salaam na Mombasa nchini Kenya wakati bandari hiyo iko na kina kirefu cha maji ambacho meli yoyote inaweza kutia nanga.
“Ndugu zangu wananchi pamoja na wafanyabiashara niwaahidini kuwa mukinichagua kuwa mbunge wenu nitahakikisha bandari yetu inafanya kazi kama zilivyo bandari nyengine” alisema Mussa na kuongeza
‘Kama kuna njama zozote za kuhujumu uchumi wa Tanga na taifa kwa jumla kupitia bandari yetu niseme kuwa sitokubali----haiwezekani mfanyabiashara wa Tanga ashushe kontena zake kupitia mbandari nyengine---kwa nini” aliuliza Mussa
Mgombea huyo alisema wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi watashusha bidhaa zao kupitia bandari hiyo ikiwa na pamoja na kuipunguzia mizigo bandari ya Dar es Salaam .
Alisema wafanyabishara wengi wamekuwa wakishusha shehena zao kupitia ya Dar es Salaam  na kusababisha kero ya foleni na hivyo kusema kuwa akichaguliwa kuwa mbunge wao bandari hiyo itakuwa sawa kama bandari nyengine.
Akizungumzia kuhusu ajira kwa vijana, mgombea huyo alisema atatoa fursa za uwekezaji kwa kutenga eneo maalumu la viwanda vidogovidogo ikiwa na pamoja na kuwatafutia soko ndani na nje ya nchi.
Alisema vijana wengi hawana kazi na wamekuwa wakikaa vijiweni kupiga soga kutokana na kutokuwa na kazi hivyo akichaguliwa atatenga eneo maalumu la viwanda vidogovidogo na kukaribisha wawekezaji.
“Vijana nichagueni niwe mbunge niwaonyesheni njia ya kujikwamua na maisha---nitawatengea eneo la viwanda vidogo vidogo-----nifungue njia ya upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi” alisema Mussa
Mussa aliwataka wananchi kumchagua kwa kura nyingi ili kuwa Mbunge wao na kuwaletea maendeleo na kuwataka kuacha kukichagua chama cha CCM kwani kimeshindwa kuwaondolea kero wananchi.
                                                  Mwisho

No comments:

Post a Comment