Thursday, October 8, 2015

VITUKO VIWANJA VYA KAMPENI, CUF NAO WAJIBU MADONGO

Tangakumekuchablog

Tanga,MGOMBEA, Udiwani kata ya Mabawa Tanga, Abrahman Hassan (CUF), amewataka wananchi wa kata hiyo kumchagua kwa kura nyingi ili akamilishe uzio wa  makaburi ya Mabawa kuzuia maficho ya wezi na watu wenye tabia mbaya kufanya vitendo viovu usiku mbele ya macho ya maiti.

Akizungumza wakati wa kampeni ya Udiwani kata ya Mabawa na kufanyika eneo la gongagonga  leo, Hassan  alisema maiti makaburi ya Mabawa wanaona mambo mengi lakini hawaaseni ila siku ya hukumu watayasema yote na kuwa mashahidi.

Alisema wezi na watu wenye tabia mbaya wamekuwa wakiyafanya makaburi kama maficho yao lakini wanajidanganya kwani maiti zilizoko makaburini wanawaona lakini wanawamezea tu hadi siku ya hukumu.

“Ndugu zangu kata ya mabawa nawaomba kwa heshima na taadhima kubwa munichague tena kuwa diwani wenu ili nikamilishe uzio wa makaburi----kila mtu anajua kuwa yale ni maficho ya wezi na watu wenye tabia mbaya” alisema Hassan na kuongeza

‘Hao wanaofanya hivyo wanajidanganya kuwa hawaonekani----wale maiti makaburini wanawafumbia macho tu lakini watambue siku ya kiama watayasema yote na kuwa mashahidi” alisema

Kwa upande wake, mgombea Udiwani kata ya Mwanzange , Rashid jumbe (CUF) , alisema tarehe 26 atamkaribisha Omari Nundu nyumbani kwake kula pilau na biriani kusherehekea ushindi wa mgombea Ubunge wa CUF , Mussa Mbarouk

Alisema ameshandaa ng'ombe wawili na gunia tatu za mchele hivyo ushindi wa Mussa Mbarouk utasherehekea na Omari Nundu pamoja na timu yake ya kampeni na kudai kuwa wasijali watakula na kushiba.

“Ndugu zanguni matayarisho ya kusherehekea ushindi wa Mussa Mbarouk na mimi mwenyewe kama diwani yamekamilika----lakini niwaambieni kuwa pia tumemualika na Nundu na timu yake ya kampeni” alisema Jumbe

Jumbe alisema kuna kitu kimoja ambacho hakijakamilika nacho ni ukwaju wa juisi na kudai kuwa siku hiyo kutakuwa na aina ya mbili ya kinwaji hicho hivyo anafikiria pia kuandaa juisi ya ubuyu.

Aliwataka wananchi wote kuhudhuria tafrija hiyo kwani haitakuwa na ubaguzi  na kudai kuwa ushindi huo ni wa watu wote lakini akasema kutakuwa na madaraja maalumu likiwemo la ugeni wa Omari Nundu.

                                                   Mwisho

No comments:

Post a Comment