MAHAKAMA
ya hakimu mkazi Morogoro imemuachia huru leo Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda aliyekuwa akituhumiwa
kwa makosa ya uchochezi baada ya mahakama kutoridhishwa na ushahidi wa
upande wa mashtaka na hivyo kuonekana hana hatia.
********
Historia ya kesi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda.
Hati
ya Mashitaka ya Kesi hiyo ilikuwa na jumla ya Mashitaka matatu lakini
Julai 22 mwaka 2015, Hakimu Mkazi Mary Moyo alitoa uamuzi wa kumfutia
shitaka la kwanza kwasababu lilishatolewa uamuzi na Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam, na hivyo mahakama hiyo ya Morogoro siku hiyo ilitoa
uamuzi wa kumuona ana kesi ya kujibu katika mashitaka mawili
yaliyosalia ambalo ni kosa la pili na la tatu .
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Morogoro ilimfungia dhamana Sheikh Ponda baada ya
kukubaliana na hati ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), wakati
huo Dk.Eliezer Feleshi ambaye kwasasa ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya
Dar Es Salaam liloomba Mahakama hiyo imfungie dhamana mshitakiwa huyo
chini ya Kifungu cha 148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai ya
Mwaka 2002.
Hatua
hiyo ya kufunguliwa kesi katika Mkoa wa Morogoro ilikuja ikiwa ni muda
mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Agosti 19
Mwaka 2013 saa Tatu asubuhi, kumfutia kesi ya jinai Na.144/2013
katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano baada ya DPP kudai kuwa
hana nia ya kuendelea kumshitaki katika kesi hiyo No.144/2013 kwa
mujibu wa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya
mwaka 2002.
Hata
hivyo baada ya hakimu Liwa kumwachilia huru,Ponda ambaye aliletwa
mahakamani hapo saa 12 asubuhi na wanausalama wa polisi na magereza
chini ya ulinzi mkali, alikamatwa tena na kupakizwa kwenye magari ya
wanausalama hao ambapo baadhi ya wanausalama hao waliliambia gazeti hili
kuwa wanampeleka Ponda mkoani Morogoro kwaajili ya kufunguliwa makosa
matatu ya uchochezi, kufanya mkusanyiko haramu na kisha akarejeshwa
gereza la Segerea Dar es Salaam , lakini baadae Uongozi wa Jeshi la
Magereza uliamua kumuamisha Ponda kutoka Gereza la Segerea na
kumuamishia Katika Gereza Moja Mkoani Morogoro.
Sheikh
Ponda alifikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi,
baada ya kuwasili kwa helikopta ya Jeshi la Polisi katika uwanja wa
gofu mjini Morogoro.
Akisoma
mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro,
Richard Kabate, Mwanasheria Kiongozi wa Serikali, Bernard Kongola,
alidai kuwa Agosti 10, mwaka 2013, katika eneo la Uwanja wa Ndege,
Manispaa ya Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu wasikubali uundwaji wa
kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwa madai kuwa zimeundwa na
BAKWATA, ambao ni vibaraka wa CCM na serikali.
Alidai
kuwa Sheikh Ponda ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Juma Nassor
aliwaagiza waumini hao kuwa endapo watu hao watajitokeza kwao na
kujitabulisha kwamba ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge
milango na madirisha wawapige.
Ilielezwa
kuwa kauli hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, iliyotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka 2010, ambayo
ilimtaka Ponda ndani ya mwaka mzima kuhubiri amani na Kuwa Raia Mwema.
Katika
shitaka la pili, Kongola alidai kuwa Agosti 10, mwaka huu, katika eneo
la Uwanja wa Ndege, Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu kuwa serikali
ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi
ili kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi, kwa sababu asilimia 90 ya
wakazi hao ni Waislamu.
Kwamba,
Ponda aliwaambia wafuasi wake kuwa serikali haikufanya hivyo kwa
wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya
uwindaji baada ya kudai ni mali yao, kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wa
huko ni Wakristu.
Shitaka
la tatu ambalo linafafana na lile la pili, ambalo nalo linadaiwa
kutendwa Agosti 10, mwaka huu, ambapo kauli ya Ponda inadaiwa kuumiza
imani za watu wengine kinyume cha kifungu cha sheria namba 390 na kanuni
ya adhabu namba 35 cha mwaka 2002.
Oktoba 18
mwaka 2012, Ponda na wenzie 49 walifikishwa Katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kwa Mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa matano, kosa la
kwanza ni la kula njama, kujimilikisha mali, kuingia kwa jinai katika
kiwanja cha Chang'ombe Markas,wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.
Milioni 59 na kosa la uchochezi ambapo katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa
ikiwakilishwa na wakili Mwandamizi wa Serikali , Tumaini Kweka .Mahakama
pia iliwafunga dhamana ya Ponda na mshitakiwa wa pili tangu 0ktoba 18
Mwaka 2012 hadi siku Kesi hiyo iliyotolewa hukumu Mei 9 Mwaka 2013.
Mei 9
mwaka 2013 Hakimu Mkazi Victoria Nongwa akitoa hukumu yake katika kesi
hiyo ya Ponda na wenzake alisema anawaachiria huru washitakiwa 49
kwasababu upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi dhidi yao na
kwamba anamtia hatiani Ponda kwa kosa moja tu la kuingia kwa jinai na
kwamba na anamuachiria huru katika makosa manne yaliyosalia kwasababu
pia jamhuri ilishindwa kuthibitisha mashitaka hayo dhidi ya Ponda.
Sheikh
Ponda alikataa rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga
hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mei 9 mwaka 2013 ambapo alishinda
rufaa yake.
Hata
hivyo siku Chache baada ya Kufungwa Kifungo hicho cha nje Mei 9 mwaka
2013, Ponda alikwenda Mkoani Morogoro na kufanya mkutano ambao alidai wa
Kutenda makosa ya jinai ambao alikamtwa Agosti Mwaka 2013 na kuwekwa
chini ya ulinzi na kufunguliwa Kesi Mahakama ya Kisutu Na.144/2013
ikafutwa na DPP na ndipo akafunguliwa kesi hiyo Mkoani Morogoro ambayo
imetolewa hukumu Leo na kuachiwa huru.
CHANZO : OTHMANI MICHUZI