Thursday, November 12, 2015

KAULI MBIU YA HAPA NI KAZI TU , SASA KILA KONA

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Ataka kauli za “njoo kesho” zikome

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kushoto) akijadiliana jambo na Kamishna wa Nishati, Mhandisi Hosea Mbise (katikati). Wa kwanza kulia ni Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, James Andilile.
Wajumbe wa kikao wakimsikiliza katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi (kushoto) akizungumza wakati wa kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kulia). Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi- EWURA, Profesa Jamidu Katima.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kulia) akipokea nyaraka mbalimbali kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi- EWURA, Profesa Jamidu Katima. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi.

Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini zimeagizwa kutochelewesha kushughulikia maombi ya wawekezaji pale wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanapoonesha dhamira ya kuwekeza. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo ametoa agizo hilo hivi karibuni wakati wa kikao chake na Watendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi hiyo.

Mhandisi Chambo aliwaagiza watendaji hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na badala yake wazingatie Sheria na maadili ya kazi zao, kutokana na ukweli kwamba sekta ya Nishati ni sekta nyeti inayohitaji watendaji waadilifu na wabunifu.

“Akitokea mwekezaji ambaye ameonesha nia ni vema ajibiwe haraka bila kuchelewa iwe amekubaliwa au kukataliwa ombi lake; hakuna sababu ya kumzungusha mwekezaji; tuzidishe kasi ya uwajibikaji,” alisema Mhandisi Chambo.

Alisema lengo la Serikali ni kuongeza uwekezaji hususan kwenye sekta za Nishati na Madini na hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha uwekezaji kwani fursa za uwekezaji zilizopo nchini ni nyingi.

Aliwaasa EWURA na Taasisi nyingine kuacha tabia ya woga, na kusema kwamba endapo itatokea mwekezaji akatuma maombi ya kuwekeza nchini, wanapaswa kupitia maombi husika, kujiridhisha na kutoa maamuzi kwa haraka na kwa kujiamini.

“Tufikie mahali tufanye maamuzi. Msiwe na woga kwenye kutekeleza jambo lenye maslahi mapana ya Kitaifa; majibu ya njoo kesho hatutayavumilia,” alisema.

Vilevile Mhandisi Chambo alisema ni vyema taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini zikashirikiana na Wizara katika kufanya upembuzi yakinifu wa miradi katika maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji. Aidha, aliwaagiza watendaji kukaa pamoja kujadili maeneo ya kipaumbele ili upembuzi yakinifu ufanyike kwa lengo la kurahisisha majadiliano na wawekezaji.

Alisema ni vyema ikaundwa timu ya wataalamu kutoka katika Taasisi na Wizara ambao watahusika moja kwa moja na suala la kubaini maeneo pamoja na kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi yenye tija na manufaa na hivyo kufikia mwafaka mapema na kuanza utekelezaji wa mradi husika pale mwekezaji anapojitokeza.

“Ikitokea mwekezaji akaonesha dhamira ya kuwekeza kwenye maeneo husika ni vema taarifa za awali zikawepo. Hii itavutia wawekezaji wengi zaidi lakini pia itaharakisha majadiliano,” alisema. Aidha, Mhandisi Chambo aliwapongeza EWURA kwa kufanya vizuri kwenye masuala ya mafuta na kuwaasa kujitahidi kufanya vizuri katika majukumu mengine yaliyo chini yao. Naye Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi aliahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu pamoja na kumpatia ushirikiano wa kutosha. Kikao hicho ni mwendelezo wa vikao vya Katibu Mkuu huyo na Menejimenti pamoja na Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ili kupata ufumbuzi wa changamoto zinazozikabili.

No comments:

Post a Comment