Sunday, November 22, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETINI LEO, NOV 22

Uchambuzi huu wa Magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, Candle inafundisha lugha za kigeni ikiwemo Kiingereza na Kifaransa. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Aphonce Mawazo aliyeuawa wiki iliyopita iko katika sintofahamu baada ya chama hicho kudai kuzuiwa na polisi kuuchukua mwili huo katika Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) ulikohifadhiwa.
Viongozi wa kitaifa wa Ukawa na Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe akiambatana na aliyekuwa mgombea urais, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, wakurugenzi wa Chadema na wabunge wa upinzani waliwasili jijini Mwanza, lakini hadi tunakwenda mitamboni hawakuwa wamechukua mwili huo.
Taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari, Tumaini Makene baadaye jioni ilisema vikao vilikuwa vinaendelea na kuwa taarifa za kina zingetolewa baadaye.
Viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa, walifika BMC jana saa 5.35 asubuhi kuuchukua mwili, lakini hawakufanikiwa na wakaondoka wakieleza kuwa wanakwenda kufanya mazungumzo kujadili suala hilo. Makene alisema: “Baada ya viongozi hao kuwasili na kupewa taarifa za awali kuhusu maandalizi ya ratiba ya utoaji wa heshima za mwisho kwa Kamanda Mawazo, wamesikitishwa sana na kitendo cha Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kuzuia shughuli hiyo kufanyika jijini humo.”
Akizungumzia kwa nini Mawazo aagwe Mwanza na baadaye Geita, Makene alisema mbali ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita, pia alikuwa kiongozi wa Kanda ya Ziwa ambayo inajumuisha mikoa ya Kagera, Mwanza na Geita.
Msimamo wa polisi Hata hivyo, polisi walikanusha madai ya kuwazuia Chadema kuchukua mwili huo lakini wakasisitiza kuwa wamezuia shughuli za kuaga mwili huo zilizopangwa kufanyika katika ofisi za Kanda ya Ziwa za chama hicho.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo alisema wamefanya mazungumzo na baba mdogo wa marehemu, Mchungaji Charles Lukiko kuwa mwili huo watauchukua kesho (leo) na kwenda kuzika mkoani Geita.
“Sisi hatujawazuia Chadema kuchukua mwili wa Mawazo, ila wao wameingiza mambo ya kisiasa, tunachosema polisi ni kwamba hatutaki shughuli za kuaga mwili huo zifanyike mkoani hapa, wala mkusanyiko wa aina yoyote.
” Mkumbo alisema wamezuia mikusanyiko ya aina yoyote kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Baadaye Mchungaji Lukiko alisema familia itauchukua mwili wa marehemu kati ya leo na kesho kutoka Bugando na kuupeleka moja kwa moja Geita kwa ajili ya mazishi.
“Bado kuna mvutano, Chadema wapo kwenye vikao vyao, wanataka kuuaga mwili wa mwenzao, lakini na sisi kama familia tunatarajia kati ya Jumapili au Jumatatu tutauchukua.
Kwa sasa siwezi kusema zaidi ya hapo,” alisema Mchungaji Lukiko. Shughuli hizo za kuaga mwili zilitarajiwa kufanyika jana kwenye Viwanja vya Furahisha au Ofisi za Chadema Kanda ya Ziwa. Awali, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Kigaila Benson alisema: “Tunashangaa polisi kutuzia kuuga mwili wa Mawazo, tulikubaliana kwamba mwili utaagwa katika ofisi za Kanda, lakini wametugeuka na kutuzuia kufanya hivyo utadhani sisi ni wahalifu.
“Mawazo hajafa kwa kipindupindu, wala hatuendi kula chakula tunataka tumuage ndugu yetu, wanavyotumia nguvu kubwa sijui inaashiria kitu gani, ni jambo la kusikitisha kwani angekuwa kafa mtu wa upande wa pili angeagwa na ulinzi angepewa.
” Mkurugenzi wa Chadema Kanda ya Ziwa, Peter Makere alisema Chadema ni jeshi kubwa zaidi na kwamba kwa vyovyote lazima mwili wa mwenzao uagwe kabla ya kwenda kuzikwa Geita.
Ulinzi mkali kila kona Jana, Jiji la Mwanza lilipambwa na askari polisi waliyokuwa na sare na waliokuwa wamevalia kiraia kila kona baadhi yao wakiwa wamebeba silaha za moto na wengine mabomu ya machozi na wengine wakiwa na mbwa.
Polisi walitanda katika Barabara Kuu inayoingia kutoka mikoa kati, Hospitali ya Rufaa Bugando na kwenye ofisi za Chadema Kanda ya Ziwa zilizopo kona ya Bwiru. Mawazo aliuawa Novemba 14 baada ya kuvamiwa na kundi la watu wanaodaiwa ni wafuasi wa CCM na tayari watu watano wamefikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji.
MWANANCHI
Sh200 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe ya uzinduzi wa Bunge zilizozuiwa kutumiwa na Rais John Magufuli zinaweza kununua vitanda vya wagonjwa 500.
Akizungumza katika hafla baada ya kuzindua Bunge juzi mjini Dodoma, Dk Magufuli alisema anafahamu kwamba Bunge limepata zaidi ya Sh225 milioni kwa ajili sherehe hiyo, lakini akaagiza zitumike kati ya Sh10 na 15 milioni na nyingine ziende kutatua tatizo la wagonjwa kulala chini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Rais alitoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa wadau mbalimbali wamechanga kiasi cha Sh225 milioni kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge katika siku ya uzinduzi wa Bunge.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa kiasi hicho cha fedha kinatosha kununua idadi hiyo ya vitanda kwa gharama ya Sh400,000 kwa kila kimoja.
Mbali na idadi hiyo, fedha hizo zinaweza kununua vitanda 80 vya kawaida vya kujifungulia vyenye thamani ya Sh2.5milioni wakati fedha hizo pia zingeweza kununulia vitanda 38 vya kisasa vya kujifungulia vyenye thamani ya Sh5.2milioni kila kimoja.
Katika hafla hiyo, Dk Magufuli alisema alipata taarifa za kuwapo kwa michango hiyo ya fedha na kutoa maelekezo kuwa zitumike kiasi kidogo kwa ajili ya hafla hiyo na sehemu kubwa zipelekwe Muhimbili ili zikatumike kununulia vitanda na hivyo kupunguza tatizo la wagongwa wanaolala chini kutokana na uhaba wa vitanda unaoikabili hospitali hiyo.
“Nilipoambiwa kwamba zimechangwa Sh225 milioni kwa ajili ya sherehe, nikasema fedha hizo zipelekwe Muhimbili zikasaidie kununua vitanda,” alisema Dk.
Magufuli na kuongeza; “kwa kufanya hivyo tutakua tumejinyima sisi wenyewe lakini tutakuwa tumewafaidisha wenzetu ambao wana matatizo makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo.
Sherehe ya Sh24 milioni Ofisa wa Bunge, Said Yakubu alisema jumla ya michango iliyopatikana ni Sh225 milioni na kwamba fedha zilizotumika katika hafla hiyo ni Sh24 milioni pekee, baada ya kuzingatia maagizo ya Rais.
Katika sherehe hiyo Rais alikabidhi vyeti vya kutambua mchango wa wadau waliochangia fedha wakiwamo Benki za NMB, CRDB na Benki ya Afrika pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF na PPF.
Novemba 9, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza Muhimbili na kukutana na matatizo mbalimbali ikiwamo wagonjwa kulala sakafuni na mashine za vipimo na uchunguzi za magonjwa mbalimbali zikiwa hazifanyi kazi kwa takribani miezi miwili.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), limemkamata raia wa Uingereza, Faiz Abdullah Ali (55) kwa tuhuma za kukutwa na kilo 22 za dawa za kulevya aina ya mirungi ikiwa imefungwa kwenye kanga na kuhifadhiwa ndani ya mabegi mawili.
Mirungi hiyo imekamatwa siku nne baada ya watu wawili kutiwa mbaroni uwanjani hapo, wakiwa na kobe hai 201 wenye thamani ya Sh30.4 milioni kwenye boksi, wakisafirishwa kwenda Kuala Lumpa, Malaysia.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Martin Otieno alidai jana kuwa mtuhumiwa huyo, mwenye asili ya Somalia, alikamatwa juzi saa 3.40 usiku katika eneo la ukaguzi wa mizigo ya abiria akiwa na mirungi hiyo.
Otieno alisema polisi wa JNIA kwa kushirikiana na kikosi cha kazi, walitilia shaka mabegi hayo ya mtuhumiwa huyo, mzaliwa wa Kismayu, Somalia kabla ya kusafirishwa kwa ndege ya Shirika la Emirates kuelekea London Uingereza kupitia Dubai.
“Mirungi hiyo ilikuwa imefungwa kwenye kanga na kuwekwa kwenye mabegi mawili moja la rangi ya silver na jingine jeusi ili mashine ya ukaguzi isitambue kilichomo ndani, lakini kutokana na mashine hizo kuwa za kisasa ilionyesha kilichomo ndani kuwa ni mirungi.
“Kama mtu anataka kusafirisha mirungi kwenye ndege anaweza kuhatarisha maisha ya wananchi ,” alisema Otieno. Alisema walipokagua hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo, ilionyesha kuwa aliingia nchini Novemba 10.
Alisema taarifa zaidi zinaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kuingia nchini Julai 20 na kukaa kwa siku tano na kwamba polisi wanafuatilia shughuli alizokuwa akifanya kwa kipindi hicho.
Otieno alisema mtuhumiwa huyo alipohojiwa alidai kuwa aliwasili nchini kwa ajili ya kufanya utalii. Hata hivyo, alisema wanaendelea kumhoji na kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini washirika wake.
Kumekuwa na jitihada za Serikali kupambana na biashara haramu za dawa hizo huku wadau wakitaja rushwa na wanasiasa kuwa ndivyo vinavyochangia kukithiri kwa biashara hiyo kwa miaka ya hivi karibuni.
Serikali iliwasilisha muswada wa kupinga dawa ya kulevya bungeni Machi mwaka huu kwa lengo la kupambana na biashara hiyo nchini.
MWANANCHI
Ushiriki wa aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia Ackson katika masuala ya siasa na hatimaye kuchaguliwa Naibu Spika wa Bunge, umezidi kuibua maswali huku akidaiwa kuwa amekiuka kanuni za watumishi wa umma.
Wasomi, wanaharakati na wanasheria wameeleza kushangazwa na uteuzi huo, kama ilivyokuwa Alhamisi alibobanwa kwa maswali bila majibu kuhusu ni lini msomi huyo wa sheria alichukua kadi ya CCM na kuwania uspika na baadaye unaibu spika kupitia chama hicho.
Hata hivyo, Dk Ackson amekanusha kukiuka kanuni za utumishi wa umma akisema ile inayolalamikiwa kukiukwa (Kanuni za Utumishi wa Umma 2009), ilifutwa kupitia waraka mpya uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Januari, mwaka huu.
“Angalia hiyo ‘circular’ kifungu cha (5), kinasemaje, usiangalie hiyo kanuni tena kwani imefutwa na huo waraka, ukisoma unaonyesha wazi. Zote hizo unazoniambia nilizifahamu kabla ya kuchukua hatua yoyote, sijakurupuka tu,” alisema.
Wiki iliyopita Dk Ackson akiwa mwanasheria wa Serikali alichukua fomu ya kuwania uspika wa Bunge kinyume na matakwa ya kanuni za utumishi wa umma, lakini baadaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho na kuwania unaibu spika, baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge.
Mchakato wa Dk Ackson kuteuliwa kugombea hadi kushika nafasi hiyo umezua maswali watu mbalimbali wakihoji ukiukaji wa kanuni hiyo inayozuia wanasheria wa Serikali kujiunga na mambo ya siasa.
Akijibu maswali ya wabunge wakati akiomba kuchaguliwa kuwa naibu spika, Dk Ackson alishindwa kueleza ni lini alichukua kadi ya CCM, hadi Spika wa Bunge Job Ndugai alipoingilia kati akamruhusu kwenda kuketi.
Wachambuzi Akizungumzia suala hilo, mwanaharakati kutoka HakiElimu, Godfrey Bonaventure alisema kitendo cha Dk Ackson kuteuliwa kushika nafasi hiyo kinaleta maswali mengi katika kanuni za utumishi wa umma na masuala ya siasa.
“Miongozo iliyopo imeweka bayana kuwa wapo watumishi wa umma ambao hawatakiwi kujihusisha na siasa kutokana na unyeti wa majukumu yao,” alisema.
Alisema suala kubwa ambalo Dk Ackson anatakiwa kujibu kwa usahihi ni je, lini alianza kuwa mwanachama wa CCM? “Watu wanaotakiwa kuhusika kwenye uamuzi mkubwa hawatakiwi kujihusisha kwenye siasa.
Hili suala lina mitego ambayo inavuruga mfumo wetu wa uwajibikaji, inatupa shaka kwa sababu hawa watu maamuzi yao ni magumu, uspika ni wajibu mkubwa,” alisema.
Bonaventure aliitaka Serikali kuheshimu miongozo yote ya utumishi wa umma ili vyombo hivyo viwe huru kufanya uamuzi. “Alipoulizwa swali bungeni kuhusu lini alikuwa mwanachama wa CCM hakuweza kutoa jibu sahihi, bila shaka angesema ni lini angeibua maswali mengi zaidi,” alisema.
Alisema iwapo Dk Ackson angesema amekuwa mwana CCM kwa muda mrefu angeibua maswali, lakini pia angesema amechukua kadi ya CCM hivi karibuni angeibua hoja atawezaje kukifahamu chama na kujua namna ya kuliongoza Bunge katika kipindi kifupi? Mwanasheria wa kujitegemea, George Shayo alisema sheria inaweka wazi kuwa watumishi wa Serikali hawatakiwi kushiriki katika siasa.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema sheria zinakataza watumishi wa umma kujihusisha na siasa. Profesa Safari ambaye pia ni wakili, alisema ingawa baadhi ya vipengele vimefanyiwa marekebisho lakini wafanyakazi wa Mahakama na wanasheria wa Serikali hawatakiwi kujihusisha na siasa.
“Ndiyo maana hata wakati Jaji Augustino Ramadhani alipochukua fomu ya urais, tulimsema sana. Hata hizi sarakasi za Dk Ackson zinachekesha, zinashangaza,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema anafahamu kuwa kuna sheria kuhusu wafanyakazi wa umma lakini haiwakatazi kujihusisha na siasa bali upo utaratibu wa kufanya hivyo.
NIPASHE
Mradi wa mabasi yaendayo hataka DART unatarajia kuanza kutoa huduma ya usafiri mwezi ujao jijini Dar es salaam.
Meneja miundombinu wa DART Mohamed Kuganda amesema ujenzi wa miundombinu ya mradi umekwenda vizuri na kusisitiza katika ya mwezi ujao huduma zitaanza kufanya kazi.
“Ujenzi wa miundombinu umefikia pazuri, wahusika wanakimbizana na muda kukamilisha sehemu zilizobakia”.
Alisema barabara za mradi ambazo zimefumuliwa kutokana na wakala wa usimamiaji TANROADS kutoridhishwa na baadhi ya sehemu za barabara hizo na kuongeza kuwa ufumuaji wake hautaathiri mipango ya mradi.
Alisema mradi huo utafanikiwa kama ulivyopangwa endapo wadau watatimiza majukumu yao ya ndani ya muda waliojiwekea.
NIPASHE
Mkazi wa kata ya Goweko, Wilaya ya Uyui, Hadija Ramadhan amejifungua kiumbe cha ajabu kinachofanana na mbweha.
Kiumbe hicho kilikuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani ambao walisafiri hadi kijijini hapo kwenda kushuhudia.
Diwani mteule wa kata ya Goweko Shaban Katalambula alisema kiumbe kilichozaliwa kinafanana na Mbweha ambacho kilizaliwa na baada ya muda kidogo kilifariki.
Kwa upande wa mkunga aliyemzalisha mwanamke huyo Hobokela Mwasisya alisema kiumbe hicho cha ajabukilizaliwa juzi saa 3 na kufariki muda mchache baadaye.
Alisema mwanamke huyo ambaye ni uzao wake wa tano alienda katika zahanati hiyo akilalamika kuumwa tumbo lakini wakati wa kujifungua hakutokwa damu jambo lililowashangaza wananchi hadi alipokimbizwa hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi zaidi.
HABARILEO
Baadhi ya wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Hai, wanalazimika kujisaidia katika mifuko ya plastiki maarufu kama ‘Malboro’ kutokana na ubovu wa miundombinu ya vyoo vya hospitali, kujaa na kukosa huduma ya maji safi.
Ubovu wa miundombinu ya vyoo hivyo katika wodi pia unasababisha kutiririka hovyo kwa maji taka, hali inayotishia kuibuka kwa ugonjwa wa kipindupindu.
Baadhi ya ndugu wa wagonjwa, Eva Mushi na Joyce Gabriel walisema iwapo hali hiyo haitarekebishwa katika kipindi kifupi kijacho itawalazimu kuhamia hospitali binafsi ili kuepuka kupata maradhi ya milipuko.
Kwa upande wake Ofisa Afya wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jonas Mcharo alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi na kuongeza kuwa tayari ametoa agizo la kufungwa kwa vyoo hivyo ili kupisha ukarabati wake.
Akizungumzia changamoto hiyo Mganga Mkuu wa wilaya ya Hai, Dk Paul Chaote alithibitisha kuwapo kwa hali hiyo na kudai kuwa yanatokana na matumizi mabaya ya vyoo vya hospitali na kuahidi kutafuta fedha za ukarabati.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dk Irene Haule alisema hali ya upatikanaji maji hospitalini hapo ni ngumu na kama hali ikiendelea hivyo watafunga vyoo vyote na kutaka wagonjwa kutafuta eneo jingine la kujisaidia.
HABARILEO
Aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Temeke, Abbas Mtemvu amefungua kesi ya uchaguzi namba 2 ya mwaka huu katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam akipinga matokeo ya ubunge katika jimbo hilo.
Katika kesi hiyo iliyofunguliwa juzi ambayo inasimamiwa na wakili wa kujitegemea Selefina Nkoba wa kampuni ya Uwakili ya Nkoba & Company, Mtemvu anawashitaki mkurugenzi wa uchaguzi katika jimbo la Temeke, Mwanasheria Mkuu (AG) na aliyetangazwa mshindi wa ubunge katika jimbo hilo, Abdallah Mtolea wa Chama cha Wananchi(CUF).
Mtemvu alisema anao ushahidi wa wazi kuthibitisha kwamba matokeo katika Jimbo la Temeke yalibadilishwa, kura zake akapewa aliyepewa ushindi ambaye ni Mtolea.
“Ushahidi katika hili ninao wa kutosha kutoka kwa wananchi mbalimbali na wapiga kura, kura nilizopata mimi alipewa waliyemtangaza kuwa ni mshindi,” Mtemvu.
Kwa mujibu wa matokeo ya Uchaguzi katika jimbo la Temeke, Abbas Mtemvu ameangushwa na mgombea wa CUF Mtolea aliyeshinda kwa kura 103,231 dhidi ya Mtemvu aliyepata kura 97,557.
HABARILEO
Serikali ilishinda kesi zote zilizofunguliwa na wagombea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wasimamizi wa uchaguzi ambapo kesi hizo ni kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Hayo yalisema na Mkurugenzi Divisheni ya Mashauri ya Madai na Usuluhishi, Obadia Kamea wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wanasheria waandamizi wa serikali yenye lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kuendesha kesi zinazohusu uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba mwaka huu.
Alisema katika uchaguzi mkuu kesi zilizofunguliwa dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi ambao ni wakurugenzi wa wilaya, mawakili wa serikali walizitetea zikashinda na kwamba hilo lilisababisha kuokoa mamilioni ya fedha ambazo zingekwenda kwenye chaguzi ndogo.
Kamea alisema kulikuwa na jumla ya kesi 48 ambapo kati ya hizo kesi 14 zilishinda kwa mapingamizi.
“Kesi nyingine 34 zote tulishinda na tulishindwa kesi moja ambayo ilikuwa ni ya Mbunge wa Igunga, Dk Dalali Kafumu lakini tulipokata rufaa kesi hiyo ilishinda na Dk Kafumu akarejeshewa ubunge wake,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yatakuwa ni chachu kwa mawakili katika kuendesha mashauri kwani watafundishwa mbinu mbalimbali za namna ya kuendesha kesi zikiwemo za uchaguzi.
Jaji Ferdinand Wambali wa Mahakama Kuu ambaye ni mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo, alisema washiriki watafundishwa taratibu za kimataifa zinazohusu migogoro ya uchaguzi ambapo Tanzania ni moja ya nchi zilizoridhia baadhi ya mikataba.
Awali, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP), Awa Dabo alisema mafunzo hayo ni chachu ya watumishi kufanya kazi zao kwa weledi hasa kwenye mashauri yanayohusiana na uchaguzi mkuu. Mafunzo hayo yanafanyika chini ya ufadhili wa UNDP kupitia Mradi wa Kuendeleza Demokrasia (DEP)
Kwa habari,matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment