HADITHI
YALIYONIKUTA TANGA (17)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Wakati naamka nilisikia sauti
ya mwanamke ikiniambia.
“Bado wewe sasa!”
Nikazinduka na kutazama huku
na huku. Sikuona kitu. Moyo ulikuwa ukinienda mbio na mwili ulikuwa umenitota
jasho.
Sikutaka kulala tena,
nikatazama saa na kuona ilikuwa saa kumi na moja jioni. Nikaenda tena kuoga.
Nilipotoka bafuni nilivaa nikatoka kwenda kutafuta chakula. Siku zote huwa
nakula kwenye mikahawa kwa sababu sikuwa na mke.
Wakati nakula kwenye mkahawa
mmoja jirani na stendi ya mabasi niliwaza ile ndoto niliyokuwa nimeota. Mwili
wangu ulinisisimka nilipoona ile picha ya upanga ukikereza kwenye shingo ya
Erick kama msumeno.
Nikajiuliza ni kwanini
nimeota ndoto ile? Au wale majini waliniotesha kunionesha jinsi mwenzangu
alivyochinjwa?
Hapo hapo ile sauti
iliyosikika ikiniambia “Bado wewe!” ilinijia akilini mwangu.
Nikahisi kama lilikuwa onyo
la kunijulisha kwamba na mimi siko salama.
SASA ENDELEA
Kwa sababu ya hofu nilitamani
niende nikairipiti ile ndoto kwa maafande wangu ili lolote litakalonitokea
wajue limetokana na majini hao, lakini niliona ningeonekana mzembe
ninayehofishwa na ndoto niliyoota mwenyewe.
kulikuwa na kitu kingine
kilichonifanya nisite kusema ukweli. Ni kile kitendo cha kidhalimu ambachoo
mimi na marehemu Erick tuliwafanyia yule mwanamke na binti yake, cha
kuwabambikia kesi na kumkamata yule mwanamke bila kujua kuwa alikuwa ni jini.
Kitendo kile ndicho
kilichosababisha balaa lote na kwa muda ule kuyaweka rehani maisha yangu.
Lakini mbali na kitendo hicho, pia ule wizi nilioufanya wa kukichukua kile
kisanduku cha dhahabu na kukihamishia nyumbani kwangu, uliwaudhi wale majini.
Nisingeweza kuusema uovu huo
tulioufanya kwa sababu pia ungeniweka mahali pabaya kikazi kwani ningeweza
kufukuzwa kazi ambayo ilikuwa ndio tegemeo la maisha yangu.
Nilikuwa nimepanga
nitakapokwenda likizo nikichukue kile kisanduku kwani ile dhahabu iliyokuwemo
ilikuwa na thamani kubwa na ingetosha kunipa utajiri.
Baada ya kumaliza kula sikuwa
na mahali pengine pa kwenda. Lakini kama si lile tukio ambalo lilikuwa
limefadhaisha akili yangu ningekuwa na sehemu nyingi za starehe ambazo
ningeweza kwenda kupoteza wakati.
Nikaona nirudi kituoni ingawa
niliambiwa nipumzike hadi saa sita usiku. Nilipofika kituoni nilikaa hadi saa
sita usiku ambapo baadhi ya maafisa wetu walifika na kuandaa kikosi cha kwenda
nyumbani kwa yule mwanamke itakapofika saa nane usiku.
Muda huo ulipofika, polisi
sita tulipanda kwenye gari. Polisi wawili walipewa bunduki. Tulilisimamisha
gari nyumba ya tatu kutoka nyumba ile ya watuhumiwa wetu.
Afande wangu Meja Elias
aliniambia nishuke peke yangu niende nikajaribu kubisha mlango wa ile nyumba
nione kama kuna watu au sauti zozote
zinazosikika. Nikashuka na kwenda kwenye mlango wa nyumba hiyo.
Ingawa nilibisha mlango,
nyumba ilikuwa kimya na hakukuwa na sauti yoyote iliyosikika kwa ndani. Nikarudi
kuwambia wenzangu kuwa nyumba ilikuwa kimya.
“Nadhani hawajakuja”
nikawambia.
“Basi tukae tusubiri hapa
hapa” Meja Elias akasema.
Tulitarajia kuwa muda si
mrefu tutawaona watu hao wakiwasili. Tulisubiri kwa muda mrefu. Tulikuwa
tunazungumza, mwisho maneno yalituishia tukawa kimya.
Muda si mrefu Meja Elias
akatuambia.
“Mimi nasinzia, wakitokea
mtaniamsha”
Baada ya dakika tano hivi
nikamuona askari mwingine akisinzia na kugemea siti ya gari. Haukupita muda na
mimi nikaanza kusikia usingizi. Baada ya hapo sikujijua tena. Mpaka nafumbua
macho kulikuwa asubuhi kumekucha! Tulilala hapo hapo.
Wakati naamka wenzangu wote
walikuwa wamelala. Nikaanza kuwaamsha.
“Vipi jamani, mbona
tumejisahau?” nikawauliza.
Wengine walikuwa wakitoka
ute. Kila aliyezinduka macho yalikuwa mekundu kuonesha alikuwa katika usingizi
mzito.
“Vipi?” Meja Elias aliuliza
kwa kubabaika.
“Mbona tumelala hadi
asubuhi?” nikauliza.
“Kwani kuna nini?” Askari
mmoja akauliza.
“Si tulikuja hapa kuwatega
watu wa nyumba ile…” nikawambia.
Hapo ndipo walipozinduka.
“Kweli tumejisahau, kumbe
sote tulilala?” Meja Elias akauliza.
“Naona tumelala sote”
nikasema.
“Si bure iko namna”
“Mimi pia nimefikiria hivyo
hivyo” nikakubaliana naye.
“Itabidi turudi kituoni, kama walikuja wameshaondoka” Meja Elias akasema.
“Lakini afande si vibaya kama tutakwenda kuwauliza wale majirani” nikamwambia.
“Tuwaulize nini?”
“Tuwaulize kama hizo sauti
wanazozisikia usiku zilisikika usiku wa jana”
“Sawa. Ngoja twende
tukawaulize”
Mimi na Meja Elias tukashuka
kwenye gari na kuelekea kwenye ile nyumba. Meja alibisha mlango. Mwanamke
yuleyule wa jana yake akatokea tena.
“Habari ya asubuhi?” Meja
akamsalimia.
“Nzuri, za kazi?” Mwanamke
huyo naye akatuuliza.
“Tunashukuru, si mbaya”
“Ndiyo”
“Nadhani umetukumbuka?’
“Ndiyo, nawakumbuka”
“Tumekuja kuuliza tena kama zile sauti zilisikika tena jana usiku”
“Tena jana ndio kulikuwa kama kuna sherehe, watu walikuwa wakiimba, wakicheka na
wengine wakila vyakula. Harufu ya pilau tuliisikia hadi alfajiri”
“Hizo sauti mlianza kuzisikia
kama saa ngapi?”
“Muda ule ule wa saa nane, kama si saa nane ni nane na nusu”
Meja akanitazama na kutikisa
kichwa kwa fadhaa. Nilikijua alichokuwa anawaza. Muda ule ndio tulioanza
kulala.
“Kwani wana matatizo gani?”
Mwanamke huyo akamuuliza Meja.
“Tulikuwa tunataka kumjua
mwenye nyumba”
Je nini kitatokea? Usikose
kuendelea na hadithi hii kesho
Mambo haya na mengineyo mazuri unayapata kupitia blog hii www.tangakumekucha.blogspot
No comments:
Post a Comment