HADITHI
YALIYONIKUTA TANGA (19)
ILIPOISHIA
Baada ya kumaliza kisa chake
polisi mwingine naye akatueleza kuwa dada yake alichunukwa na mwanaume ambaye
alikuwa jini na akataka amuoe.
“Alikuwa akimuona wazi wazi?”
nikamuuliza.
“Ndiyo alikuwa akimtokea na
kumuona kama hivi tulivyokaa hapa” Polisi huyo
akasema na kuongeza.
“Basi dada yangu alihangaika sana kwenda kwa waganga
kumuondoa yule jini. Waganga wengi walishindwa”
“Alikuwa akifanya naye
mapenzi?” Meja Elias akamuuliza.
“Ndiyo alikuwa akifanya naye
mapenzi”
“Sasa walikuwa wanakwenda
wapi?”
“Kwenye mahoteli”
“Nani anapangisha chumba hapo
hoteli?”
“Ni yule jini. Yaani amekaa kama mwanaadamu tu. Anavaa nguo kama
hizi tunazovaaa, sema alikuwa muarabu. Mwenyewe alimwambia ni mwenyeji wa
Misri’
Na mimi nikamuuliza.
“Alikuwa akija naye
nyumbani?”
“Nyumbani hakuwahi kufika
naye. Yaani yule jini anapofika kutoka huko kwao anampigia simu dada yangu,
hapo hapo dada yangu akili zinapotea anakwenda mwenyewe mahali alipoambiwa
wakutane”
“Na alikuwa akimpa pesa?”
nikamuuliza.
“Alikuwa akimnunulia vitu
alivyokuwa anahitaji”
SASA ENDELEA
“Sasa mwisho wao uliishaje?”
nikamuuliza.
“Yule dada yangu alivyojaribu
kwenda sana kwa
waganga yule jini alimtia kichaa”
“Ha! Baadaye alipata kichaa?”
“Alipata kichaa. Aliaguliwa sana. Mpaka hivi karibuni
akapata mganga mmoja aliyetoka Pemba ndiye
aliyemponesha”
“Na huyo jini ameishia wapi?”
Meja akamuuliza.
“Hajamuona hadi leo”
“Mimi nimesikia Wapemba
wanawakamata majini” Meja akasema.
“Hata mimi niliwahi kusikia
hivyo hivyo. Nilisikia wanawatia kwenye chupa au kuwafungia kwenye sanduku”
Yule polisi aliyekuwa akitusimulia alisema.
Pakapita ukimya kidogo. Mimi
nilikuwa nikiwaza juu ya simulizi hizo zilizokuwa zikitolewa hapo. Nilishangaa
kusikia kuwa majini wanafungiwa kwenye chupa. Nikajiuliza wanapata wapi pumzi?
Sikutosheka kujiuliza peke
yngu, nikauliza.
“Sasa jini unapomfungia
kwenye chupa atapata wapi pumzi?”
“Wanajua wenyewe waganga”
alinijibu yule polisi.
“Kwani hawa majini ni nini,
ni upepo tu na miujiza miujiza. Popote tu anaweza kukaa. Wewe unaambiwa majini
wanaishi chini ya bahari, wewe unaweza kuishi chini ya bahari? Kuna hewa huko?”
Meja akatoa hoja yake.
Hakuna aliyejibu. Mazungumzo
yalikuwa ya kutisha lakini yalisaidia kupitisha muda na kukimbiza usingizi.
Ghafla gari la polisi la doria likatupitia.
Polisi mmoja alishuka kwenye
gari hilo akatuuliza kama
tulikuwa na tatizo lolote. Tulipomjibu kuwa hatukuwa na tatizo alirudi kwenye
gari.
“Tutawapitia baadaye”
akatuambia kabla ya gari hilo
kuondoka.
Baada ya gari hilo kuondoka, sote
tukapitiwa na usingizi kwa mpigo lakini haukupita muda mrefu tukazinduka mmoja
mmoja. Kilichotuzindusha zilikuwa ni kelele za vicheko zilizokuwa zikitokea
ndani ya ile nyumba.
Tuliona pia mwanga wa taa
ukitokea mle ndani. Tukajua kuwa wale watu tuliokuwa tukiwasubiri walikuwa
wameshafika. Hatukujua waliingia kwa mlango gani. Kama
ni kwa mlango ule wa mbele watakuwa wametuona tukiwa tumelala.
Vicheko vilikuwa vikiendelea
mle ndani. Tukatazamana kisha sote tukainuka. Meja Elias ndiye aliyekwenda
kubisha mlango. Hatukupata jibu.
Meja akaujaribu ule mlango
akaona ulikuwa wazi, akaufungua na kuchungulia ndani. Kitendo hicho cha
kufungua ule mlango kikazinyamazisha zile kelele zilizokuwa zikisikika. Kukawa
kimya.
Ghafla na zile taa zilizokuwa
zikiwaka zikazimika. Kukawa kiza.
“Kachukue tochi kwenye gari,
wametuzimia taa” Meja akaniambia.
Nikakimbilia kwenye gari letu
na kuchukua tochi. Nikenda nayo na kumulika kwenye ule ukumbi. Ukumbi ulikua
mtupu.
Meja akapiga hodi lakini
hakukuwa na jibu.
“Tuingie ndani” Meja
akatuambia.
Alitangulia yeye kuingia
nikafuatia mimi niliyekuwa na tochi. Wenzetu wakafuatia nyuma. Hatukuwa na
wasiwasi kwa sababu tulikuwa na bunduki lakini nilijiambia kama
ni majini wasingeweza kutishika na bunduki zetu.
Wakati tunaingia tulisikia
vicheko kwa uani mwa nyumba hiyo. Tukaenda hadi uani huku nikiendelea kumulika
tochi. Tulipofika uani hatukuona mtu. Na vile vicheko havikusikika tena.
Tukashangaa sana. Tukaanza kutafuta kwenye vyumba vya
uani. Kila chumba tulichoingia kilikuwa kitupu. Ghafla tukasikia tena sauti ya
vicheko ikitokea ukumbini kule tulikotoka. Tukasita na kutazamana.
Tukaamua kiurudi ukumbini.
Hatukukuta watu. Tukafungua milango ya vyumba na kuchungulia ndani. Tukasikia
sauti ya vicheko ikianza kusikika tena kwa uani.
“Hii nyumba ni ya majini
kweli!” Meja akatuambia.
“Tunasikia watu wanacheka
lakini hatuwaoni” Polisi mwingine akasema.
“Sasa tufanyeje?” nikauliza.
Hofu yangu kubwa ilikuwa ni kukutana na
yule mwanamke chinjachinja.
“Tutafute swichi zilipo
tuwashe taa” Meja akasema.
Nikamulika mulika tochi pale
ukumbini, tukaziona swichi. Meja akawasha taa za nyumba nzima. Tuliendelea
kupekua kwenye vile vumba vya ukumbini. Hatukukuta mtu. Vile vicheko vya uani
vilikuwa vikiendelea.
Tukaamua kutoka uani ambako
sasa kulikuwa na mwanga wa taa. Vile vicheko vikakoma. Tukafungua tena milango
ya vyumba vya uani tukidhani labda kulikuwa na watu waliokuwa wamejificha
lakini hatukuona mtu. Vicheko vikaanza tena kusikika ukumbini.
“Hapa tutazunguka hadi
asubuhi, hawa watu wanaocheka hatutawaona” nikawambia wenzangu. Lengo langu ni
kutaka tuondoke.
Hapo hapo tukasikia gari
likisimama nje, tukajua lilikuwa gari la polisi la doria. Tukatoka sote. Mimi
nilikuwa wa kwanza kutoka.
Tulipofika nje tukaona kweli
lilikuwa gari la polisi la doria. Polisi wanne walishuka na kutufuata.
“Vipi jamani, mmewaona hawa
watu?” Polisi mmoja akatuuliza.
Meja akawaeleza vituko
vilivyokuwa vikitokea mle ndani. Hapo hapo tukasikia sauti ya vicheko imeanza
tena. Vicheko hivyo vilisikika nyumb nzima.
“Si watu hao wanacheka?”
Polisi mmoja akatuuliza.
“Ndiyo, lakini ukiingia
hukuti mtu” Meja alimjibu.
“Hebu twendeni, tuone”
Tukarudi tena humo ndani
pamoja na polisi hao. Sauti zilizokuwa zikisikika ukumbini zikaacha, zikabaki
sauti zilizokuwa zikisikika uani. Tulikwenda uani. Sauti hizo nazo zikaacha.
Wale polisi tulioingia nao
wakashangaa.
“Mbona hivi!” mmoja akauliza.
“Hii ni miujiza ya mwaka”
Meja akamjibu.
Wale polisi waliotoka kwenye
gari la doria wakataka kuingia kwenye vile vyumba vya uani ili kuhakikisha kama kweli hamkuwa na watu.
Tukawaacha waingie, waliingia
kila chumba na kuchunguza ndani. Hawakuona mtu. Wakarudi ukumbini na kuendelea
kufungua vyumba vya ukumbini ambavyo pia havikuwa na watu. Wakati wa zoezi hilo zile sauti za vicheko
zilikuwa zimenyamaza.
Baada ya hapo tulitoka nje
tukiwa tumekubalina kwamba ile nyumba ilikuwa na miujiza. Uamuzi huo
ulinifurahisha kwa sababu ungekomesha ule upelelezi wetu na mimi ningepata
nafasi ya kwenda likizo ambako ningefanya mashauri mengine.
Je nini kitafuatia? Endelea
kufuatilia kesho.
|
Monday, February 16, 2015
YALIYONIKUTA TANGA SEHEMU YA (18)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment