Hizi ni Story 8 kubwa zilizopewa headlines kwenye Magazeti ya leo Tanzania February 17, 2015.
MWANANCHI
Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande baada ya kuwepo malalamiko ya ubabaishaji katika zabuni mbalimbali za mamlaka hiyo.
Hatua hiyo ya Sitta imekuja wiki tatu baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuiongoza wizara hiyo akitokea Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla, wizara hiyo ilikuwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe.
Sitta, ambaye pia hujulikana kama Mzee
wa Viwango, amewaambia waandishi wa habari jijini hapa leo kuwa wadau
mbalimbali wamesema taratibu za zabuni TPA haziendeshwi kwa uwazi na
uaminifu.
“Wanasema
hakuna uwazi katika zabuni, kuna dalili ya ubabaishaji. Katika kamati
za kutathmini zabuni majina ya watu yanabadilika badilika na hata baada
ya mshindi kupatikana bodi huchelewa kutoa barua inayohusu uamuzi wa
kumpata mshindi huyo”:- Sitta.
Kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji ndiye
msimamizi mkuu wa shughuli za bandari, amesema ameamua kumsimamisha
Kipande kupisha uchunguzi kwa kipindi hicho na nafasi yake itachukuliwa
na Meneja Bandari ya Dar es Salaam, Awadh Massawe.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa kamati ya hesabu za Serikali ‘PAC’ Zitto Kabwe amewataka wamiliki wa malori ya mafuta kutafuta biashara nyingine ya kufanya kabla Serikali haijaachana na usafirishaji huo.
Akitoa maoni yake kabla ya kukagua
mitambo ya kupima ujazo wa mafuta yanayopakuliwa kutoka melini ,alisema
matumizi ya barabara kusafirisha mafuta hayana tija kwa Serikali.
“Kuna
haja ya Serikali kujenga mabomba ya mafuta kuelekea mikoani ili kuongeza
ufanisi wa ukusanyaji wa mapato,tutaishauri Serikali inunue asilimia 50
ya hisa za kampuni ya Tiper ili iiendeshe kwa asilimia 100,wamiliki wa
malori ni vyema wakaanza kufikiria biashara nyingine watakayofanya“:-Zitto.
Alisema kama suala hilo litatekelezwa Serikali itanusuru uharibifu wa barabara unaotokana na uzito mkubwa wa malori
NIPASHE
Wakati Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza likiendelea kumsaka mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Pendo Emmanuel (4) kwa siku ya 51 sasa aliyeibwa kijiji cha Ndami,
Kwimba na watu wasiofahamika Desemba 27, mwaka jana, mtoto mwingine
albino ameibwa mbele ya wazazi wake katika kijiji cha Ilelema, wilayani
Chato, Geita.
Mtoto huyo, Yohana Bahati,
mwenye umri wa mwaka mmoja, aliibwa usiku wa kuamkia jana, akiwa
amebebwa na mama yake, Esther Bahati (30), ambaye alivamiwa na watu hao
na kupigwa mapanga akiwa jikoni kisha kuporwa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo,
alisema tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 2:00 usiku, wakati
mama huyo akiwa jikoni anapika chakula na watu hao kumvamia na kumkata
mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Watu
wasiofahamika walimjeruhi mama wa mtoto kisha kumtwaa mgongoni pasipo
kumdhuru na kutoweka sehemu isiyojulikana mpaka sasa hajapatikana wakati
jeshi la polisi likiendelea kuwasaka waliotenda uhalifu huo”:- Konyo.
Konyo alisema Esther baada ya kujeruhiwa
kwa mapanga, aliwahishwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita
kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa usoni, mikononi na
mabegani alipokuwa akijaribu kupambana na watu hao wasimchukue mwanaye.
Alisema kutokana na tukio hilo, polisi
mkoani Geita inamshikilia baba wa mtoto huyo, Bahati Misalaba, ambaye
wakati tukio hilo linatokea alikuwa akiota moto nje ya nyumba hiyo.
NIPASHE
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Dodoma, Frola Mhele, ameambia Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuwa aliyekuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Pcificus Clerofas Simon, alipelekwa kwake kuungama kumuua aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni Chanel Ten Mkoa wa Iringa, Daud Mwangosi, kwa bomu bila kukusudia.
Mhele aliyasema hayo jana mbele ya Jaji wa Mahakama hiyo, Paulo Kihwelo, wakati akitoa ushahidi wa kesi ya mauaji ya Mwangosi.
Hakimu huyo ambaye ni shahidi wa tatu,
alidai kuwa mtuhumiwa huyo alipelekwa kwake kuungama wakati akiwa
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mjini Iringa.
Alidai Septemba 5, 2012 saa 7:24 mchana,
polisi walimpeleka mtuhumiwa huyo katika mahakama hiyo kwa ajili ya
ungamo na kuchukua maelezo.
Shahidi huyo alidai alimkagua mtuhumiwa
mwilini mwake na kumkuta akiwa na jeraha bichi kwenye mkono wake wa
kulia katika kidole cha kati kutoka mwisho na majeraha ya zamani.
Mhele alidai alipomuuliza kuwa jeraha
amelipatia wapi, alimjibu alilipata wakati bomu lilipolipuka na kwamba
hakujua kama amepata jeraha hilo.
MTANZANIA
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,
Juma Ndaki, amesema watu waliopambana na askari polisi na wale wa Jeshi
la Wananchi (JWTZ) ni kikundi cha wahuni.
Harakati za mapambano baina ya polisi na wahalifu hao zilidumu kwa takribani saa 48, huku Mkuu wa Mkoa huo, Said Magalula akikiri kwamba wameshindwa kuwakamata watu hao.
Jana Ndaki aliwaambia waandishi wa
habari kuwa, jeshi hilo linawashikilia watu kadhaa kutokana na tukio la
majambazi kushambiliana na askari polisi usiku wa kuamkia Jumamosi.
“Kuna watu kadhaa tumewakamata kuhusika na tukio hilo na upelelezi zaidi unaendelea ili kuweza kuwakamata wote waliohusika.
“Niwatoe
hofu wananchi, tukio zima lilihusisha kikundi kidogo cha wahuni ambacho
walikuwa wanajificha katika Mapango ya Kijiji cha Mleni kwa ajili ya
kufanya shughuli za kiuhalifu “ :-Ndaki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said
Magalula, alisema hali katika Mji wa Amboni ni salama na kuwa,
waliookuwa wanapambana na polisi ni majambazi na si magaidi.
MTANZANIA
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM),
amesema kwa muda wa miaka kadhaa sasa baadhi ya vyama vya siasa
wilayani Ludewa vimekuwa vikimshawishi atoke kwenye chama chake jambo
ambalo amekuwa akilipinga.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kijiji cha Nsele,
Kata ya Kilondo wilayani hapa, alisema hata mapokezi aliyoyapata
yalikuwa ya vyama vyote, vikiwamo vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), huku baadhi yao wakimshawishi ahamie kwenye vyama vyao.
Filikunjombe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
alisema wapinzani wanamthamini na kuona kazi zake akiwa CCM, hivyo
ataendelea kuwajibika kwa wananchi akiwa ndani ya chama hicho.
“Nimekuja
hapa nimepokewa na vijana na viongozi wa vyama vyote, hasa vya Chadema,
CUF na TLP, na wengine wakati wananibeba walidiriki kuniambia kuwa wana
hofu nitakatwa jina kwenye chama changu na kama itakuwa hivyo nijiunge
na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),:- Filikunjombe.
Akizungumzia maendeleo ya Kata ya
Kilondo, mbunge huyo alisema awali ilikuwa haina huduma za maendeleo
ambapo Januari 30, mwaka huu alikwenda na wahandisi wa umeme na kuzindua
mradi wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya wilayani humo.
Lakini kutokana na kasi ya utekelezaji
wa mradi huo vijiji vyote vya Kata ya Kilondo kabla ya kufikia Desemba
mwaka huu vitakuwa vimepata huduma ya umeme ili wananchi wa maeneo hayo
waweze kupata huduma za maendeleo.
HABARILEO
Mwanafunzi wa Darasa la Saba, Adam Abdul Sapi (13) ametawazwa kuwa Chifu mpya wa Wahehe, akirithi nafasi ya baba yake, aliyefariki na kuzikwa jana mkoani Iringa.
Rais Jakaya Kikwete alishiriki jana maziko ya Chifu huyo wa Wahehe, Abdul Sapi Mkwawa (66) yaliyokwenda sanjari na hafla ya kumsimika mtoto huyo kushika wadhifa huo wa kimila.
Maziko ya kiongozi huyo aliyefariki
Februari 14, mwaka huu, yalifanyika katika kijiji cha Kalenga, nje
kidogo ya mji wa Iringa ndani ya makumbusho yaliyowekwa fuvu la babu
yake,Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga Mkwawa.
Mbali na Rais Kikwete, wengine
waliohudhuria maziko hayo ambayo taratibu zake zilitumia takribani saa
2.30 kuanzia saa 7 mchana ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Tanzania Bara, Phillip Mangulla, wakuu wa mikoa ya Iringa na Mbeya na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa.
Kabla ya kifo chake kilichosababishwa na
maradhi ya sukari na figo, Abdul Sapi Mkwawa aliyekuwa mtoto wa tatu wa
Spika wa kwanza mweusi nchini, Adam Sapi Mkwawa, alikuwa akifanyakazi
katika kiwanda cha maji Afrika cha Kidamali, Iringa.
HABARILEO
Kampuni ya Acacia
inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mkoani Shinyanga, imesema ndani
ya miaka miwili, itasitisha shughuli za uchimbaji na uzalishaji madini
hayo, kutokana na soko kuzidi kushuka.
Meneja Mkuu wa mgodi huo, Filbert Rweyemamu
alisema hayo juzi katika kikao cha pamoja baina ya mgodi na wajumbe wa
Kamati ya Kijiji cha Mwime, iliyoundwa na uongozi wa mtaa wa Mwime kwa
ajili ya kusainiana mkataba wa shughuli za maendeleo.
Rweyemamu alisema shughuli za uzalishaji
na uendeshaji ni tofauti na mauzo, hivyo kampuni inazidi kutumia
gharama kubwa za uendeshaji.
“Kutokana
na mgodi kusitisha shughuli za uzalishaji ndani ya miaka miwili ijayo;
siyo kwamba dhahabu zimeisha dhahabu ni nyingi mno, isipokuwa
tunashindwa kumudu gharama za uzalishaji wilaya ya Kahama ina dhahabu
tangu hatujaingia, makampuni mengi yalichimba na kuondoka na sisi
tunaondoka”, alisema meneja huyo.
Bei ya dhahabu kwa mwaka 2014, imekuwa
chini ya dola 1,300 kwa ounce moja kwa muda mrefu. Kufikia Novemba, bei
ilikuwa 1,129 kwa ounce moja, hali ambayo imeleta mtikisiko wa
uendeshaji wa kampuni za uchimbaji wa dhahabu.
Baada ya kujadili upya, walibaini baadhi
ya miradi ya vyoo vitano vinavyogharimu Sh milioni 51 na visima vitano
vinavyogharimu Sh milioni 140, havikuwemo katika rasimu hiyo, hali
iliyopingwa na Meneja wa mgodi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment