Tangakumekuchablog
Tanga,MGOMBEA
Udiwani kata ya Mnyanjani kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Suleiman Khafidh,
amesema endapo wananchi watamchagua kuwa
diwani atanunua helkopta kwa ajili ya wajawazito na wazee kuwapeleka hospitali.
Akizungumza katika mkutano wa
kampeni juzi uwanja wa mpira wa Mnyanjani, Khafidh alisema ili kukomesha
wajawazito kujifungua njiani kutokana na mitikisiko ya ubovu wa barabara
atawachukua kwa helkopta kutoka
nyumbani hadi hospitali.
Akitoa kali hiyo aliwafanya wananchi
kumshangilia na kutakiwa kuitekeleza ahadi hiyo mapema ili kuweza kuvuna
wanachama na kuwa na uhakika wa kuinyakua kata hiyo ya uwakilishi kupitia
halmashauri.
“Ndugu zangu wananchi mimi ndie
mgombea mdogo kuliko wagombea wote wa nafasi ya ubunge na udiwani hivyo damu
yangu inachemka----akili za kijana ikiwaza na kudhamiria ni kutekeleza tu” alisema Khafidh na kuongeza
“Nawaahidi mama zangu na wazee wangu
wa kata hii endapo mutanichagua kuwa diwani wenu nitanunua helkopta kwa ajili
yenu na kuwapeleka juu kwa juu hadi hospitali na kuondokana na adha ya ubovu wa
barabara ambapo wakati mwengine wajawazito hujifungua barabarani” alisema
Akizungumzia fursa kwa vijana,
mgombea huyo alisema atajenga shule maalumu ya lugha ya Kichina na Kiingereza
ili kurahisisha mawasiliano katika nyanja za kibiashara na huduma za kijamii.
Alisema kundi kubwa la watu hasa
vijana hawajui lugha za kigeni na badala yake wanashindwa kuwasiliana na watu
wa mataifa mengine jambo ambalo limekuwa likiwapa nafasi wageni kuhodhi nafasi
za ajira.
“Ndugu zangu niko na dhamira ya
kweli kuifanya kata hii kuwa eneo la maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuwa
mfano kwa kata nyengine----nitajenga chuo maalumu cha lugha ya kiingereza na
kichina” alisema Khafidh
Alisema ili kuweza kuitekeleza
dhamira yake hiyo amewataka wananchi kumpa kura nyingi kuwa Diwani wao na
kusema kuwa atalipa fadhila hiyo kwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment