Monday, October 5, 2015

MKUU WA MKOA WA TANGA AWAPA SOMO WAJASIRIAMALI WANAWAKE

Tangakumekuchablog

Tanga,MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, amewataka wajasiriamali wanawake kuunda vikundi ili kuweza kupata mikopo katika taasisi za fedha  na kulitumia soko la pamoja la Afrika ya Mashariki (EAC)

Akizungumza katika uzinduzi wa Sakina Saccoss  iliyomo ndani ya Umoja wa Wajasiriamali wanawake wa Maawal Woman Group , Mahiza alisema kazi za mikono za wanawake zinapotea machoni mwa jamii na kuitaka Saccoss hiyo kuwa mfano kwa wengine..

Aliitaka kikundi hicho cha Sakina   kuwa cha mfano kwa kubuni mbinu mbalimbali za kjipatia mapato kwa tengezeza bidhaa ambazo zitawavutia wateja wa ndani na nje ya nchi na kupelekea kusimama wenyewe na kuacha kutegemea wafadhili.

“Napata faraja  kuona wanawake wenzangu kufikia kuwa na saccoss yenu wenyewe na nimeelezwa kuwa muko zaidi ya wanachama mia mbili ---cha msingi umoja huu udumishwe na kuwa kichocheo kwa wengine” alisema Mahiza na kuongeza

“Nataka mutambue kuwa kazi za mikono ziko na soko kubwa ndani na nje ya nchi----hivyo jamani tulitumie soko la pamoja la jumuiya yetu ya Afrika ya Mashariki kupitia saccoss yenu ili musimame na kuwa taasisi” alisema

Mahiza alisema wenzao katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wamekuwa wakilitumia soko kikamilifu na kusema kuwa ni jambo la kushangaza kuona wajasiriamali wa Tanzania hawana habari nalo.

Alisema kazi  nyingi za mikono nchini  ni za nje ilhali wajasiriamali wa ndani wako na bidhaa nzuri ambazo kama zitafika katika masoko zinaweza kuitangaza Tanzania kiuchumi na kiutalii.

Akizungumza katika uzinduzi huo, mlezi wa Sakina Saccoss, Amina  Kassim alisema wanakabiliwa na changamo nyingi zikiwemo vifaa vya ofisni na mtaji wa kutunisha Saccoss yao na kukuza miradi ya vikundi vya ujasiriamali.

Alisema ufinyu wa mtaji umepelekea kushindwa kufikia malengo kwa wakati ikiwemo kukuza miradi ya wanachama wao kwa kuwawezesha mikopo ili kuweza kuwa wabinifu wa kazi zao.

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa mbali ya uchanga wetu lakini tumeweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo ikiwemo kufungua matawi wilayani ----lakini mtaji bado ni mdogo” alisema Kassim

Alisema endapo watawezeshwa wanaweza kuyafikia malengo ikiwemo kukopeshana na kutanua miradi yao na kuondokana na umasikini majumbani jambo ambalo litawavutia watu wengi.

                                                     Mwisho

No comments:

Post a Comment