Tangakumekuchablog
Tanga, POLISI
Mkoani Tanga inawashikilia wahamiaji
haramu sita wenye asili ya Ethopia wakiwa
wamefichwa katika msitu wa Kichalikani Wilayani Mkinga na baadhi yao wakiwa
wamechoka kwa njaa.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana ofisini kwake , Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zuberi Mombeji, alisema
tukio hilo lilitokea juzi saa 11 alfajiri wakati wa doria baada ya kupata taarifa za kufichwa
kwa watu hao.
Aliwataja wahamiaji hao kuwa ni
Warikine Hizza (30), Namamba Amita (36), Tamery Ashored (29), Daudi Manemeo
(25) Luosed Kedaw (28) na Tahmed Afford (29) na kusema kuwa wote wanashikiliwa
kituo kikuu cha polisi Chumbageni.
“Wakati wa operesheni zetu za
kawaida tulipata taarifa za kufichwa kwa wahamiaji haramu na ilichukua maasa
ishirini na nne hadi kuwakamata kutokana na mvua kubwa na wao kuhamishwa
hamishwa” alisema Mombeji na kuongeza
“Tuliwagundua wakiwa wamefichwa
katika pango la mbuyu mnene huku wakiwa wamechoka kwa njaa---inavyonekana
wenyeji wao walikuwa kama wamewatekeleza” alisema
Kamanda Mombeji alisema watuhumiwa
hao wanahojiwa na mara baada ya uchunguzi itawafikisha mahakamani kujibu tuhuma
za kuingia nchini bila kibali na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na polisi
kukomesha uingizaji wa wahamiaji haramu na bidhaa za magendo.
Katika tukio jengine, polisi
Wilayani Handeni inamshikilia, Bashiru Hamis (44) mkazi wa Ilala Dar es Salaam kwa tuhuma za kupatikana
na bastola moja yenye risasi 9 wakati wakijiandaa kufanya tukio la kihalifu.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 3
usiku Mkata Wilayani Handeni wakati polisi ilipopata taarifa kutoka kwa raia
wema kuwepo kwa watu hao ambao walikuwa wameweka kambi katika nyumba ya kulala
wageni.
“Tulipata taarifa kutoka kwa raia
wema kuwepo kwa watu wawili ambao nyendo zao hazikuwa za kiungwana na walikuwa
wanatoka nyakati za usiku na kurejea alfajiri kila siku” alisema Mombeji
Kamanda Mombeji alisema hali hiyo
iliwalazimu wananchi kutoa taarifa kituo cha polisi na ndipo ilipowekwa mitego
na kunaswa Hamis wakati mwenzake aliwahi kutoroka na hivyo jeshi la polisi linaendelea
kumtafuta.
No comments:
Post a Comment