Wednesday, November 4, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO NOV 04 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo pia kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na ufundi, Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

MWANANCHI
Wagombea wa urais wa Zanzibar wa vyama sita, wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN), Ban Ki Moon kumwomba asaidie kutatua mgogoro wa Zanzibar uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Vyama hivyo ni Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, Chaumma, Sau, DP na NRA ambavyo mbali na kumweleza Ban kwamba hawakuridhishwa na kufutwa kwa matokeo na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, pia wamemwomba aingilie kati mkwamo huo.
Katika barua hiyo, vyama hivyo vimesema vimevunjwa moyo na Jecha kufuta matokeo, wakati alitakiwa aendelee na kumtangaza mshindi ili kuepusha machafuko.
Mgombea wa NRA, Seif Ali Iddi alisema wameamua kuandika barua hiyo wakiamini kuwa UN inaweza kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Katibu mkuu wa Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir alisema wamepeleka barua UN kwa sababu hawana imani na Mwenyekiti wa ZEC na hawatambui uamuzi wake kwa kuwa hakukuwa na malalamiko.
“Tunataka matokeo ya Zanzibar yatangazwe, pia tunataka mgogoro huu umalizwe na Jumuiya ya Mataifa iingilie kati na tunaomba kamati ya wataalamu kuchunguza na kupata ushahidi wa uchaguzi wa Zanzibar ulivyokwenda.” Juma alithibitisha kumwandikia barua Ban iliyotiwa saini na wagombea hao sita wakitaka kuona mgogoro huo unatatuliwa kwa njia za kidiplomasia kwa kuwa wanaamini Serikali ya Tanzania haina nia ya kuutatua.
Vyama hivyo vimemweleza Ban kwamba, uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki na baadhi ya majimbo yalishatangazwa huku waangalizi wa ndani na wa kimataifa wakishuhudia lakini jambo la kusikitisha matokeo yasitishwa.
Makamu mwenyekiti wakati anatangaza matokeo alisitishwa asiendelee huku tukasikia kupitia televisheni kwamba matokeo yamefutwa na Mwenyekiti Jecha. Sasa tunajiuliza, ni kwa nini yafutwe na mamlaka hayo ya kuyafuta kayatoa wapi?” Juma.
Barua hiyo iliyopokewa na ofisa wa UN, Alvaro Rodriguez ilisema jambo la kushangaza katika kufutwa kwa matokeo hayo ni kwamba hakuna malalamiko yaliowasilishwa na chama chochote cha siasa ambayo yangeweza kuonyesha kasoro za uchaguzi huo ilhali waangalizi wa ndani na nje wote waliona uchaguzi umekwenda kwa salama, amani na haki.
Wagombea hao walisema Umoja wa Mataifa ndiyo taasisi pekee inayoweza kutatua mgogoro huu na si Serikali ya Tanzania kwa madai kuwa tayari imeshavunja Katiba ya nchi kwa kushindwa kusimamia suala zima la hali iliyojitokeza Zanzibar. “…Inajua kwamba mwenyekiti hana mamlaka lakini kwa sababu ni mtu wao wanamwachia tu.” Tangu kufutwa kwa matokeo Novemba 28 na Jecha, hali ya kisiasa Zanzibar bado haijatulia huku wananchi wakiwa na hofu ya kutokea kwa vurugu licha ya wanasiasa.
MWANANCHI
Wakati Bunge la Kumi na Moja likitarajiwa kuanza vikao vyake wiki ijayo mjini Dodoma, Samuel Sitta na Anne Makinda, waliokalia kiti cha Spika wa mabunge mawili yaliyopita, wanatajwa kuwamo kwenye mchuano mwingine wa kuwania nafasi hiyo ya kuongoza chombo hicho cha kutunga sheria.
Majina ya makada hao wawili wa CCM, ambao mwaka huu hawakugombea ubunge kwenye majimbo yao, ni miongoni mwa watu kadhaa wanaotajwa kuwania kuongoza Bunge la 11 ambalo linatarajiwa kuanza vikao vyake wiki ijayo.
Kada mwingine wa CCM ambaye amekuwa akitajwa kwa muda mrefu ni mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu ambaye anatarajiwa kutoa upinzani mkubwa kwa wawili hao endapo ataingia kwenye mchakato wa kuwania nafasi hiyo.
Wengine wanaotajwa kuitaka nafasi hiyo ni mbunge mteule wa Peramiho, Jenister Mhagama, mbunge mteule wa Kibakwe, George Simbachawene na Job Ndugai ambaye ni Naibu Spika wa Bunge lililomaliza muda wake.
Kiti cha spika kinaweza kuwaniwa na mtu yeyote ambaye atapitishwa na chama chake bila ya kujali kama ni mbunge. CCM hutoa fursa kwa wanachama wake kuomba nafasi hiyo na baadaye kikao cha wabunge wa chama hicho hukutana kupitisha jina la mgombea mmoja.
Iwapo mgombea hatakuwa mbunge mteule, ni lazima jina lake lipitishwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Iwapo wawili hao wataingia kwenye kinyang’anyiro hicho, Sitta, aliyeongoza Bunge la Tisa ambalo linasifika kwa kuruhusu hoja zilizoibana Serikali, na Makinda, aliyeongoza Bunge la Kumi lililoibua kashfa zilizolazimisha mawaziri kujiuzulu, watakuwa wakipambana kwa mara ya pili baada ya kukutana mwaka 2010 wakati CCM ilipomtosa Sitta kwa hoja ya “kutaka Spika mwanamke”.
Habari kutoka kwa watu walio karibu naye zinasema Sitta, ambaye ni Waziri wa Uchukuzi, atapeleka jina lake CCM kwa ajili ya kuteuliwa kuwania nafasi hiyo.
Taarifa hizo zilithibitishwa na msemaji wa mbunge huyo wa zamani wa Urambo Mashariki, John Dotto ambaye alilieleza gazeti hili kuwa Sitta atawania nafasi hiyo kutokana na uwezo na uzoefu alionao wa kuendesha Bunge. Alisema Sitta anaamini kuwa uwezo wake aliouonyesha katika kuendesha Bunge la Tisa (2005 hadi 2010) akitumia kaulimbiu yake ya “Spika wa Kasi na Viwango”, utamfanya aendane na kasi ya utendaji wa Rais Mteule, Dk John Magufuli.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Sitta ana nafasi kubwa ya kuibuka mshindi kutokana na rekodi yake na pia kukubalika na wabunge wengi wa CCM na hata wa vyama vya upinzani.
Hata hivyo, Sitta hakupatikana kueleza kiundani kuhusu suala hilo kutokana na kuwa nje ya nchi. Alitarajiwa kurejea jana jioni.
Baada ya kuongoza Bunge lililomlazimisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujiuzulu, Sitta alijaribu kutetea nafasi yake mwaka 2010, lakini akagonga mwamba. Baadhi ya watu walimuona kuwa ni mtu aliyekuwa akiruhusu mijadala ya kuibana Serikali, kitu kilichofanya ajijengee uadui na baadhi ya vigogo.

Kwa upande wa Zungu, ambaye alikuwa mmoja wa wenyeviti wa Bunge la Kumi, hakutaka kukanusha wala kuthibitisha suala hilo alipoulizwa na gazeti hili.
Zungu aliliambia gazeti hili jana kuwa chama chake bado hakijatoa mwongozoo wowote hadi kufikia jana jioni na hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo.
Mtu mwingine anayetajwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni Naibu Spika anayemaliza muda wake, Job Ndugai, ambaye pia hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa bado anauguza ‘majeraha’ ya Uchaguzi Mkuu.
Ndugai, ambaye amerudi bungeni akiliwakilisha Jimbo la Kongwa, alisema wiki hii atavieleza vyombo vya habari kama atawania nafasi hiyo.
Jibu kama hilo lilitolewa na Mhagama, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Kumi kabla ya kuteuliwa kuwa waziri. Mbunge huyo wa Peramiho alisema hawezi kuzungumzia vyema suala hilo kwa sababu yupo katika matayarisho ya hafla fupi ya kuapishwa kwa Rais Mteule.
MWANANCHI
Polisi jana waliimarisha ulinzi katika maeneo mengi nchini kukabiliana na maandamano yaliyodaiwa kupangwa na wafuasi wa Chadema nchini kupinga kile walichoita ubakaji wa demokrasia.
Hata hivyo, katika maeneo hayo hapakuwapo na maandamano yaliyoombewa vibali na wafuasi hao na kuzuiwa na polisi.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja, alisema jana kuwa jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachoonyesha viashiria vya uvunjifu wa sheria na kutaka kuvuruga amani.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana wakati wa mkutano wa amani uliofanywa na kamati ya ulinzi na usalama ya viongozi wa dini wa mkoa huo kuwa ulinzi utaimarishwa hadi Rais mteule, Dk John Magufuli atakapoapishwa kesho.
“Tuliahidi vikosi vyetu vya usalama vitaimarisha ulinzi wakati wa kampeni, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi. Tumefanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo hadi mchakato huo utakapokamilika kesho,” alisema.
Ulinzi Katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, polisi waliovalia vifaa vya kudhibiti ghasia walikuwa katika doria tangu saa 12 asubuhi katika maeneo mbalimbali. Huko mkoani Geita, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha alisema jana kuwa Kamanda wa Polisi wilayani hapo, George Kyando amezuia maandamano yaliyokuwa yafanyike asubuhi. Katibu wa Chadema, Mkoa wa Geita,
Soud Ntanyagara alisema waliomba kibali cha maandamano ambayo yangeanzia mjini Ushirombo saa 5.30 asubuhi hadi Uwanja wa Kilimahewa lakini yalikataliwa. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema hatapokea barua yoyote ya kuomba maandamano kwa kuwa mwelekeo wake ni wa kuvunja amani. Hata hivyo, Katibu wa Chadema mkoa huo, Calist Lazaro alisema wamesitisha maandamano hayo kwa sababu za kichama na si kwa amri ya kamanda huyo.
Mkoani Mwanza, kiongozi wa operesheni Kanda ya Ziwa Magharibi, Chadema, Tungaraza Njugu alisema maandamano yamekuwa magumu kwa sababu polisi wamekuwa wakisambaratisha makundi ya watu. Malumbano yaliibuka kati ya Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani akisema yeyote atakayethubutu kuandamana atakabiliana na nguvu za Dola huko Katibu wa Chadema Wilaya ya Moshi, Mohamed Ally akisema kuandamana ni haki ya kikatiba ya kila mtu.
MWANANCHI
Watu sita wamefariki dunia Mkoani Singida  katika matukio manne tofauti likiwemo tukio la wanawake wawili kuuawa kikatili kwa kukatakatwa kwa jembe sehemu mbalimbali za miili yao na mume wao.
Kamanda wa Polisi Singida Thobias Sedoyeka aliwataja wanawake hao mbele ya waandishi wa habari kuwa ni Mwanahamisi Juma na Mwanahamisi Abrahani wote wakazi wa kata ya Mgori, Singida.
Alisema Mustapha Said ambaye alikuwa mume halali wa mwanahamis Juma anatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo na alitekeleza unyama huo baada ya kuwakuta wanawake hao wakilifanyia usafi shamba lao kwa ajili ya kupanda mbegu.
Kamanda Sedoyeka alisema mwanaume huyo naye aliuawa na wananchi waliokuwa wamejaa hasira kali.
Chanzo cha mauaji hayo inasemekana mwanaume huyo huyu alikua ametalikiana na mke wake wake wa kwanza na walikua katika ugomvi wa shamba lao.
MTANZANIA
Wakati maandalizi ya kuapishwa Rais mteule Dk. John Magufuli kesho yakiendelea, taifa limeanza kupokea wageni baada ya muhubiri maarufu duniani wa Kanisa la Church of All Nations la nchini Nigeria, T.B Joshua kuwasili jana mchana akiwa na msafara wa watu 40.
Muhubiri huyo aliyewasili Dar es Salaam jana mchana akitumia ndege binafsi, alilakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Dk. Magufuli, aliyeambatana na mkewe, Janeth Magufuli pamoja na mtoto wake wa kiume.
T.B Joshua amekuja kushuhudia kuapishwa kwa Dk. Magufuli katika sherehe zitakazofanyika kesho Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwasili kwa muhubiri huyo, alikwenda Ikulu kwa ajili ya mazungumzo mafupi na Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa iliyotolewa Ikulu jana, ilisema kuwa mara baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, T.B Joshua, alikwenda Ikulu moja kwa moja kumsalimia Rais Kikwete na kumpongeza kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu kwa uhuru na amani, huku akiondoka madarakani akiwa mtu mwenye furaha.
“T.B Joshua amempongeza Rais Kikwete pia kwa kumpata Dk. Magufuli kama mrithi wake, akimtaja rais huyo mteule kama rais wa Tanzania wa baraka na fanaka tele katika awamu hii mpya,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Muda mfupi baada ya muhubiri huyo kuwasili  nchini, picha zake zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Baadhi ya picha hizo ni zile zilizomuonyesha akiwa uwanja wa ndege na msafara wake pamoja na na Dk. Magufuli na mkewe.
Nyingine zilimuonyesha akiwa ameketi ndani akiwa na Dk. Magufuli na mkewe pamoja na mtoto mdogo wa kiume wa rais huyo mteule.
Dk. Magufuli ni kati ya wanasiasa wa Tanzania waliowahi kwenda nchi Nigeria kwenye kanisa la muhubiri huyo ambaye ni maarufu kwa kutabiri mambo mbalimbali ya kimataifa.
Katika safari hiyo ya Dk. Magufuli nchini Nigeria, aliambatana na mkewe na mtoto wake huyo mdogo wa kiume, ambapo pamoja na kufanyiwa maombi, pia alifanya mazungumzo ya faragha na muhubiri huyo wa kimataifa anayeheshimiwa duniani kwa kuwa na waumini wengi.
Mbali na Dk. Magufuli mwanasiasa mwingine aliyewahi kwenda katika kanisa la T.B Joshua na kufanyiwa maombi ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye aligombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Pamoja na viongozi hao, pia Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alikwenda nchini Nigeria katika maombi.
 Mhubiri huyo wa kimataifa mwenye heshima duniani, jana baada ya kutoka Ikulu, alikwenda kumtembelea Lowassa nyumbani kwake Masaki na kufanya naye mazungumzo.
MWANANCHI
Watu wanne akiwemo askari Polisi, mkaguzi na wasimamizi wa mitihani ya kidato cha nne Arusha wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kukutwa wakivujisha mtihani wa Kiswahili uliokuwa unatarajiwa kufanyika Novemba 20 mwaka huu.
Mtihani huo ulijulikana kuwa umesambaa katika shule ya Sekondari Arusha baada ya wanafunzi kugawiwa na wakati wanausoma ndipo walipogundua kuwa si wa Novemba 2 kama ulivyopangwa bali ni wa Novemba 20 ndipo walipoamua kutoa taarifa wasimamizi.
Mkurugenzi wa jiji la Arusha Idi Juma alisema mtihani huo ni wa watahiniwa wa kujitegemea ambao hufanya mitihani miwili na watu hao walijichangaya badala ya kuchukua mtihani wa Kiswahili wa awamu ya kwanza walichukua wa awamu ya pili.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakuweza kuwataja majina wahusika kwa madai kuwa bado wanaendelea na upelelezi kubaini chanzo cha tukio hilo.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete, amemteua Ramadhan Kaswa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi kuanzia Oktoba 30, mwaka huu, 2015.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam jana ilisema kabla ya uteuzi wake, Kaswa alikuwa KatibuTawala wa Mkoa Msaidizi, Mkoa waTanga.
Septemba 14, mwaka huu, Rais Kikwete aliteua wakuu wa mikoa wapya ambao ni Amos Makalla, aliyepelekwa mkoani Kilimanjaro na Jordan Rugambana, aliyeteuliwa kwenda mkoani Lindi.
Wengine ni Mlinga Mkucha, aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Dk. Tulia Ackson, kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Oktoba 23, mwaka huu, Rais Kikwete aliteua Naibu Makatibu wakuu wapya watano, kuhamisha wawili na Makatibu Tawala wa mikoa wawili.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment