HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Nikafungua mlango wa gari na kushuka. Nikiwa nje ya gari
nilimpungia mkono wa kumuaga na yeye akanipungia.
Nikaondoka zangu. Na yeye akaondka na gari. Nilipitia kwenye bucha
ya nyama nikanunua kilo moja ya nyama kisha nikaenda kwenye duka ninalonunulia
vitu. Nikanunua kilo mbili za mchele na mahitaji mengine kisha nikarudi
nyumbani.
Sebuleni nilimkuta shemeji Zacharia akiangalia Tv. Ibrahim
hakuwepo. Nikajua alikuwa chumbani amelala. Sikuingia chumbani kwa kuwa nilijua
angeniuliza ninakotoka kwa vile nilichelewa sana.
Nikaingia katika chumba kingine ambacho huweka nguo zangu za
kufanyia kazi za nyumbani. Nikabadili nguo nilizokuwa nimevaa kisha nikaingia
jikoni na kutayarisha ile nyama. Nyama ilipokuwa jikoni nilichambua mchele. Nilikuwa
nimekusudia kupika pilau.
Baada ya masaa mawili pilau ikawa tayari. Nikatenga chakula juu ya
meza. Nikamwaambia shemeji akamchukue kaka yake waende wakale. Mimi
nilijipakulia kwenye sahani yangu nikaenda kuketi uani peke yangu.
Wakati ninakula kile chakula nilikuwa nikimuwaza Chinga na jinsi
nitakavyoweza kuwa naye. Nilijiambia itakuwa ni uzembe kuacha aoe mke mwingine
wakati alikuwa ameshanipenda na amekuwa akinipa pesa nyingi.
“Nitaendelea kuishi na hili zezeta hadi lini? Mwisho nitakosa hata
nguo ya kuvaa” nikajisemea peke yangu.
SASA ENDELEA
Baada ya kumaliza kula chakula nilirudi ndani. Nilimkuta Ibrahima
na mdogo wake na wao wamemaliza kula.
Zacharia aliondoa vile vyombo akaviingiza jikoni kisha akatoka
kusafisha meza. Nilijua kuwa alifanya hivyo kwa kuniogopa mimi kwani tayari
alikwishaiona hali ilivyo pale nyumbani.
Tangu kaka yake apofuke macho nilikuwa mkali kama
simba na sikuwa na adabu kwa kaka mtu wala kwa mdogo mtu.
“Ukimaliza kusafisha meza uje uoshe vyombo” nikamwambia Zacharia.
“Nioshe vyombo?” akaniuliza kwa mshangao. Ilikuwa ndiyo mara yangu
ya kwanza kumwambia hivyo.
“Sasa kumbe ulitaka aoshe nani? Kama
hutaki mwaambie kaka yako aje aoshe yeye!” nikamwaambia kwa jeuri na kuongeza.
“Mmenifanya mimi ni kama mtumishi wenu.Chakula nitafute mimi, kupika nipike
mimi na vyombo pia nioshe mimi!. Haitawezekana”
Zacharia akanyamaza kimya.
“Zacharia nenda kaoshe” Ibrahim akamwaambia mdogo wake.
Zacharia alipomaliza kusafisha meza aliingia jikoni kuosha
vyombo.Mimi nilikwenda kuoga kisha nikabaki chumbani nikijua kuwa Ibrahim
asingeingia tena muda ule.
Mchana ukapita. Ilipofika usiku wakati Ibrahim ameingia chumbani
kulala, mimi niliketi sebuleni kuangalia Tv peke yangu. Zacharia pia alikuwa
ameshaenda kulala.
Lakini lengo langu halikuwa kuangalia Tv. Lengo langu lilikuwa
kumpigia simu Chinga tuzungumze. Nikambipu na muda uleule akanipigia.
“Vipi Chinga umeshalala?” nikamuuliza baada ya kupokea simu.
“Hapana, nilikuwa namalizia bia yangu ya pili ndipo nikalale”
akaniambia.
“Kumbe unakunywa?”
“Bia zangu hazizidi mbili. Ni za kupatia usingizi tu. Uko wapi?”
“Niko nyumbani”
“Mbona umenipigia, jamaa yuko wapi?”
“Yuko chumbani ameshalala, mimi nipo sebuleni.Nilitaka tuzungumze
kidogo”
“kuhusu nini?”
“Kuhusu yale mazungumzo yetu. Ni kwamba mimi nimeshakubali lakini
sasa huyu mwanaume nitamuachaje?”
“Si umdai talaka tu”
“Hawezi kuitoa.Mimi ndio tegemeo lake kwa
sasa”
“ Hilo si tatizo.Tukutane hapo
kesho tuzungumze hilo
suala”
“Tukutane wapi?
“Sema wewe”
“Au nikufuate hapo hoteli?”
“Saa ngapi?”
“Usiku itakuwa vizuri”
“Utaweza kutoka usiku?”
“Nitatoka hivyo hivyo. Mchana sitaweza kuja hapo. Kuna macho ya
watu wengi”
“Sasa nikufuate na gari au….?”
“Nitakuja na teksi. Wewe niambie upo chumba namba ngapi”
“Nipo chumba namba 15, kipo ghorofa ya kwanza”
“Mimi nitakuja humo chumbani moja kwa moja”
“Sawa lakini utaniambia saa utakayo kuja”
“Nitakuambia kesho”
“Haina tatizo. Sasa utanipigia saa ngapi hapo kesho?”
“Siwezi kukuambia kwa sasa lakini nitakupigia wakati wa mchana
kukujulisha. Na huo usiku nitakapo ondoka pia nitakujulisha”
“Sawa nitakusubiri”
“Okey.Usiku mwema”
“Na kwako pia’
Chinga akakata simu. Moyo
wangu ukawa umefarijika kwa kuzungumza naye. Nikainuka na kuingia chumbani. Wakati
ninapanda kitandani kulala nilidhani kuwa Ibrahim alikuwa usingizini. Niligeuka
upande wangu nikajilaza. Mara nikasikia sauti yake akiniita.
Kwanza nilinyamaza. Aliponiita mara ya pili
nikamuuliza.
“Unasemaje?”
“Unajua mke wangu hivi sasa tabia yako imebadilika sana …..” akaniambia.
Hapo hapo nikajua alikokuwa anaelekea. Nikamkata kauli.
“Unaanza…unaanza…unaanza! Sitaki maneno. Kama
huna maneno ya maana ya kuniambia nitatoka humu chumbani nikuachie chumba chako
nikatafute pa kulala”
Ibrahim akanyamaza. Uwanja wa kusema ukawa ni wangu.
“Mwanaume una gubu kama nini. Kila
unalofanyiwa huridhiki. Unataka roho yangu au unataka nini?.Hebu niambie!”
“Salma mimi sina gubu isipokuwa tabia yako unayoionesha tangu mimi
nipate matatizo ya macho…..”
Sikumngoja amalize maneno yake, nikainuka kwa jazba na kuketi
kitandani.
“Sitaki maneno mengi. Kama mimi nimekuwa sina tabia nzuri
kukuletea chakula wewe na ndugu yako ule, basi nipe talaka yangu niondoke. Halafu
utafute huyo mke mwenye tabia nzuri” nikamwaambia kwa ukali huku nikimnyooshea
mkono wa kudai talaka.
“Salma wewe hutaki kuambiwa ukweli. Ukiambiwa ukweli unakuja juu. Mbona
juzi na jana wakati nikiwa mzima hukudai talaka?”
“Hukuwa na gubu kama ulivyo hivi sasa.
Maneno yamekuwa hayaishi. Balaa gani hili jamani!.Ule muda wa kulala na
kupunzisha mwili, ndiyo unaanza maneno. Sasa mimi nitaondoka hapa kwako hata kama hutanipa talaka!”
Nikashuka kwenye kitanda huku nikiendelea kugomba.
“Sitalala tena humu ndani. Nimechoka na kelele zako”
“Sasa unakwenda wapi?” Ibrahim akaniuliza aliposikia ninafungua
mlango.
Sikumjibu kitu nikatoka na kwenda sebuleni. Nikajilaza kwenye kochi. Baada ya muda
kidogo nilimuona akitoka chumbani huku akiniita.
“Salma! Salma!”
Alikuwa akipapasa kwenye kuta akielekea sebuleni.
Nikamnyamazia kimya. Alipoona kimya akadhani labda nilikuwa
nimetoka nje na kwenda zangu. Akapapasa ukuta hadi kwenye chumba anacholala Zacharia.
Akamgongea.
“Zacharia! Hebu fungua mlango!” sauti yake ilikuwa imefadhaika.
Zacharia alipofungua mlango nilisikia akimwaambia.
“Shemeji yako ametoka, sijui amekwenda wapi. Hebu toka umuangalie”
“Kwani amekuambia anakwenda wapi?” Zacharia akamuuliza.
“Hakuniambia. Tulisemeshana kidogo akatoka kwa hasira, sijui
amekwenda wapi”
Zacharia akatoka na kuja sebuleni, akawasha taa na kuniona
nimelala kwenye kochi.
“Shemeji si huyu hapa” akasema.
“Yuko wapi?” Ibrahim akamuuliza kwa pupa.
“Amelala kwenye kochi
”
Ibrahim akapapasa kuta na kuja pale sebuleni.
“Yuko wapi?” akauliza tena.
Wakati wote huo nilikuwa nimenyamaza kimya.
“Shemeji kaka anakuuliza” Zacharia akaniambia.
Mimi nikaendelea kunyamaza.
“Salma!” Ibrahim akaniita.
Sikumjibu.
ITAENDELEA kesho usikose
No comments:
Post a Comment