Tangakumekuchablog
TUME
ya Jumuiya ya Madola inayosimamia Makaburi ya Vita vya Kwanza vya Dunia
(CWGC) inatarajiwa kuzindua makaburi mapya ya askari wa Kihindi
waliokufa katika vita hivyo vya kwanza vya dunia Mkoani Tanga.
Akizungumza
na waandishi habari jijini Tanga, Ofisa ufundi wa Jumuiya hiyo, Daniel
Achini, alisema uzinduzi huo utafanyika mwezi Novemba 11, 2016.
Achini
alisema uzinduzi huo utafanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo ya CWGC,
Victoria Wallace ukishuhudiwa na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cook
na Balozi wa India, Sandeep Arya.
Sherehe hizo pia zitahudhuriwa na Balozi wa Ujerumani, Egon Konchake na viongozi wa Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Alisema
makaburi hayo mapya yapatayo 62 yamezikwa miili ya askari wa Kihindi
waliokufa vitani katika eneo la Jasin kati ya Januari na Julai, 1915.
Makaburi hayo yamejengwa maeneo ya Usagara na Jasin, karibu na jiji.
Kumbukumbu
ya makaburi ya Wahindi na yale ya Usagara yaliyoko hapa Tanga ni sehemu
tu ya makaburi mengi yanayohudumiwa na Tume hiyo ya CWGC.
Ofisa
huyo alieleza kuwa makumbusho ya Jasin, ulikuwa ni mji wa mbele wa
kujihami katika pwani ya kaskazini ya mji wa Tanga na ambao ulichukuliwa
na Wajerumani mwezi Januari, 1915. Alisema vikosi vya Jind na Kashmiri
ndivyo vilivyoulinda mji, ambao ulitekwa na kuchukuliwa tena na vikosi
vya wanajeshi 2,000 wa Kijerumani tarehe 18 Januari, 1915.
Makumbusho
ya makaburi ya Tanga ambayo yapo katika eneo la Usagara, yanahifadhi
kumbukumbu ya vifo 394 vilivyotokea katika vita vikali vilivyopiganwa
katika mji wa Tanga kati 1914 na 1916 baina ya mataifa makubwa ya
Uingereza na Ujerumani.
Achini
alifafanua kwamba moja ya kazi muhimu ya Tume hiyo barani Afrika ni
pamoja na kutunza makaburi na kumbukumbu za vifo zaidi 190,000
vilivyotokea katika vita vya kwanza na pili vya dunia katika nchi zaidi
ya 40 zilizopo Afrika.
"Nchini
Tanzania, tunavikumbuka vifo zaidi ya 55,000 vilivyotokea katika vita
vyote katika viwanja 12 vya makaburi", alidokeza Achini.
Alitaja
baadhi ya maeneo ya makaburi yanayohudumiwa na CWGC yanapatikana Dar es
Salaam, Morogoro, Dodoma, Iringa na Moshi Zanzibar.
Mwisho
No comments:
Post a Comment