HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE
ILIPOISHIA
Ibrahim akaingia chumbani na mimi nikaingia humo humo ili kama
amesikia kitu aniulize. Lakini Ibrahim hakuniuliza chochote.
Ilipofika saa nne nilitoka bila kumuaga nikaenda sokoni.
Niliporudi niliingia jikoni. Nilikuwa nimenunua samaki,mchele na
vitu vingine. Pesa ya Chinga ilikuwa inafanyakazi.
Nikaanza kupika. Hadi saa saba mchana wali ukawa tayari.
Nikawatengea Ibrahim na mdogo wake kwenye meza na mimi kama
kawaida yangu nilijipakulia kiasi changu nikaenda kukaa uani.
Wakati ninakula nilijiuliza, mbona Ibrahim hakuniuliza kitu wala
hakuonesha kukasirika?.Huenda hakuyasikia mazungumzo yangu na Chinga. Moyo
wangu ukapata faraja kidogo.
Ilipofika mida ya jioni nikamwaambia Ibrahim kuwa ninakwenda kwa Rita
kuzungumza. Si kwamba nilikuwa nimebadilika na kuamua kumpa heshima yake ya
kumuaga kila ninapotaka kutoka, lahasha. Kumuaga huko kulikuwa ni kuzuga
tu kama vile namfanya mjinga. Mbona nikiwa na
safari zangu za maana nilikuwa simuagi!
Nilichukua muda mwingi nikiwa kwa jirani yangu Rita tukizungumza
hili na lile lakini kubwa tuliloliongelea ni kuhusu uhusiano wangu na Chinga.
Kwa vile msimamo wa Rita ulikuwa nisiachane na Ibrahim kwa kuwa
mimi ndiye niliyemsababishia matatizo ya macho, sikumueleza undani wangu kuwa
nilitaka niolewe na Chinga kwa sababu angeupinga uamuzi wangu huo.
SASA ENDELEA
Nilikuwa na ahadi ya kumpigia Chinga jioni ile, nikaona nimpigie
nikiwa kwa Rita. Nikambipu, yeye akanipigia.
Katika maongezi yetu tulipanga kukutana kesho yake usiku pale pale
hoteli. Baada ya hapo nikamwaambia kuwa nilikuwa nyumbani kwa shoga yangu Rita
na kumtaka asalimiane naye.
Nikampa simu Rita, wakasalimiana. Baada ya hapo Rita akanirudishia
simu.
Nilikaa kwa Rita hadi saa mbili usiku nikarudi nyumbani kwangu.
Kulikuwa na wali uliobaki mchana, Nikaona tule huo huo. Nikachemsha
chai na kuitia kwenye chupa kisha nikaandaa chakula hicho mezani. Kama kawaida yangu nilijitengea chakula changu na kwenda
kuketi uani peke yangu.
Nilipomaliza kula na kurudi ndani nilikuta chakula kimebaki kingi.
Kumbe Ibrahim hakula, alikunywa chai tupu. Na mimi kwa jeuri yangu sikutaka
kumuuliza kwanini hakula chakula kwani nilishagudua tangu niliporudi kutoka kwa
Rita, Ibrahim alikuwa amekasirika.
Alionekana kuwa mnyonge sana.Nilihisi labda alinifikilia nilikuwa
natoka kwa mwanaume. Kama alinidhania hivyo
alikuwa amejikangaja.
Licha ya kwamba nilitaka kumfanya mpumbavu lakini Ibrahim alikuwa
mtu mwenye subira na busara pia, kwani alisubiri hadi usiku wakati tunajiandaa
kulala chumbani ndipo aliponitolea undani wake.
Akanieleza kwamba amegundua kuwa nilikuwa na mwanaume mwingine wa
nje.
Kwanza nilidhani alikisia kwa vile nilivyokwenda
kwa Rita, nikamwaambia atoke aende akamuulize Rita kama nilikuwa kwake ama
nilikuwa kwa mwanaume.
Lakini Ibrahim alikuwa timamu, akaniambia.
“Achilia mbali habari ya Rita.
Mimi sizungumzii juu ya kwenda kwako kwa Rita. Unaye mwanaume na jana ulikwenda
kwake uliponiambia unakwenda kwa shangazi yako.”
Ingawa ukweli wake usingekuwa tishio kwangu kwa sababu tayari nia
yangu ilikuwa kuachana naye lakini aliponiambia vile nilishituka na kidogo
nilinywea. Hata hivyo nikajihazahaza kwa kutoa kicheko cha uongo nikijifanya
namshangaa.
“Wewe sasa huo upofu wako utakutia kichaa, uliniona wapi na huyo
mwanaume?” nikamuuliza ili nijue alijuaje kuwa nilikwenda kwa mwanaume.
“Ni kweli nimekuwa kipofu lakini sina kichaa, nipo timamu.
Ninachokuambia nina hakika nacho. Wewe una mwanaume ambaye una mpango naye
uondoke kwangu, lakini ninakwambia binaadamu haishi kuumbwa na utu ni bora
kuliko kitu.
“Yaliyonikuta mimi, na wewe yanaweza kukukuta. Na ni utu wako
pekee utakaokupa thamani ya ubinaadamu na siyo kitu. Nilitaka kukuambia hivyo
tu.Maneno yangu yameisha”
“Lakini nataka uniambie nani amekuambia kuwa nina mwanaume na nina
mipango ya kuondoka kwako.Au unahisi hisi tu?” nikamuuliza. Kusema kweli sauti
yangu ilikuwa imenywea kidogo.
“Asubuhi ulikuwa unazungumza na nani kwenye simu pale uani?”
Ibrahim akaniuliza.
Moyo ukanipasuka. Sasa nikagundua kuwa Ibrahim aliyasikia
mazungumzo yetu na Chinga tulipokuwa tunazungumza kwenye simu wakati wa
asubuhi.
Ukweli ni kwamba nilitahayari kwa sababu sikutaka Ibrahim ajue
jambo hilo
lakini kwa vile alikuwa ameshalijua sikuwa na jinsi.
Nikamjibu kwa kumropokea
“ Kama kazi yako ni kusikiliza watu wanaoongea kwenye simu
utasikiliza mengi sana”
Baada ya hapo sikumsema tena. Nikapanda kitandani upande wangu nikalala.
“Mimi nakuonya kama mume wako lakini kama
unanidharau endelea na mwenendo wako” Ibrahim akaniambia.
Hapo ndipo aliponipandisha madudu yangu.
“Babu wee usiniletee kelele! Mimi nataka kulala, unanionya kitu
gani nisichokijua?” nikamwambia kwa sauti ya dharau.
“Kuelezana kupo. Mimi ni mume wako hata kama
umenidharau. Siwezi kuona una mahusiano na mwanaume wa nje nisikuambie” Ibrahim
akaniamia kwa sauti tulivu.
“Huyo mwanaume umenifumania naye au ni umbea wako wa kusikiliza
simu za watu? Kwani wewe unanipa pesa yako au ninajihudumia mwenyewe? Mume ni
pesa siyo maneno matupu. Mimi sijioni kama
nina mume, nisingehangaika mchana kutwa kwenda kuombaomba kwa watu. Wenye waume
zao huwaoni nini?”
“Sawa bibi, kama leo umefikia
kuniambia hivyo ili kunionesha kuwa umepata mwanaume mwenye pesa nakuombea
heri. Ibrahim leo ni kipofu lakini narudia kukuambia kuwa binaadamu haishi
kuumbwa na utu wa mtu si pesa”
Maneno yake yakazidi kunipandisha.
“Usiniapize mwana wa mwenzio. Binaadamu haishi kuumbwa maana yake
nini?” nikamuuliza kwa ukali.
Ibrahim hakujibu kitu. Nikaendelea kumwaambia.
“Sasa kama mimi nimeshakuwa Malaya,
nina wanaume je wewe unachukua uamuzi gani?”
“Uamuzi unao wewe mwenyewe” Ibrahim akaniambia kwa sauti
iliyonyeea.
“Basi nipe talaka yangu niondoke. Huo ndiyo uamuzi wangu. Kwanza nimeshachoka na maisha ya kuhangaika!”
Ibrahim akanyamaza kwa vile nilikuwa nimemfikisha mahali
asipopataka.
“Usijitie kunyamaza, umeyataka mwenyewe. Nipe talaka yangu!”
nikaendelea kumwaambia.
Lakini Ibrahim aliendelea kubaki kimya, nikawa ninasema peke
yangu. Mwishowe na mimi mikanyamaza.
Asubuhi kulipokucha nikajitia kufura. Sikusafisha nyumba wala
sikuchemsha chai. Nilitoka bila kumuaga mtu nikaenda kwa Rita..Nilikunywa chai huko
huko kisha nikaingia chumbani mwake nikalala mpaka saa sita. Nilipoamka
nikarudi nyumbani.
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment