HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE 21
ILIPOISHIA
“Ni kwa sababu mchana nilikuwa na kazi ya kufua nguo”
“Sasa Salma tutafanya nini?. Unadhani suala lake litakuwa
kikwazo tusiwe pamoja?”
“Litakuwa kikwazo. Wewe si unataka kunioa?”
“Na umesema hataweza kukupa talaka hata kama
utaidai?”
“Hataweza kunipa”
“Je ukiifuatilia Bakwata?”
“Bakwata nikawaambie nini?”
“Kwamba huyo mwanaume hana uwezo wa kuishi na wewe, kwa hiyo
unataka muachane”
“Bakwata hawatakubali, wataona ninamkataa kwa sababu amepofuka.
Wataninasihi niendelee kuwa naye hivyo hivyo”
Chinga akapiga funda jingine la bia. Alipoirudisha birauli
aliniambia.
“Hatutakosa njia nyingine. Nakupa muda uendelee kufikiri lakini
jaribu kumshinikiza akupe taraka”
“Wewe utakuwa hapa Tanga mpaka lini?”
“Sina muda mrefu. Naweza kuondoka siku yoyote nitakayoamua”
“Basi tuendelee kufikiria njia nyingine. Kwa vile sina nia ya
kuendelea kuishi naye, kama hataniacha yeye
nitamuacha mimi!”
“Lakini umenipenda?” Chinga akaniuliza ghafla. Macho yake
yalionesha kuwa ulevi ulikuwa umeanza kumchukua. Iliwezekana alianza kunywa
muda mrefu.
SASA ENDELEA
“Kama nisingekupenda nisingekuja huku” nikamjibu.
“Kama ni kweli kunywa bia kidogo”
“Nimekuambia situmii”
“Onja kidogo”
“Nitaonya siku nyingine”
“Basi njoo uketi hapa”
Alimaanisha nikaketi naye kitandani.
“Hapa nilipokaa panatosha”
Chinga akainuka na kunifuata akanishika mkono na kuniinua.
‘Mbona uko hivyo Salma? Hebu twende tukakae pale”
“Chinga utasababisha nichelewe nyumbani” nikajidai kulalamika huku
nikimfuata kwenye kitanda. Nikaketi na yeye akaketi.
“Wewe umeshaamua kuwa na mimi, unajali nini kuchelewa? Wewe ni
wangu tu au si kweli?”
Nikanyamaza kimya na kubaki kumtazama machoni. Akatabasamu na
kunipitishia mkono kiunoni.
“Una macho ya kimahaba
kweli!” akaniambia kisha akanibusu midomoni. Kilichofuatia baada ya hapo
sitakisema. Ni aibu.
Ilikuwa saa nne ikikaribia kuwa na nusu Chinga aliponirudisha
nyumbani. Nilimwaambia asimamishe gari nyumbni kwa jirani yangu Rita ili
Ibrahim na mdogo wake wasijue kuwa nimeletwa na gari.
Chinga akanipa shilingi laki moja kabla sijashuka kwenye gari.
“Ahsante” nikamwaambia kabla ya kuagana naye.
Nikashuka kutoka kwenye gari na kutembea kuelekea nyumbani.
Nilikuta mlango wa mbele ukiwa umefungwa. Nikabisha. Zacharia
akaja kunifungulia, nikaingia.
“Habari ya saa hizi?” akanisalimia.
“Nzuri” nikamjibu huku nikizuga kwa kuangalia kwenye runinga.
“Unatazama kanda?” nikamuuliza.
Niliona deki imewashwa na kuonesha filamu za kina Kanumba.
“Ndiyo shemeji” Zacharia akanijibu huku akifunga mlango kisha
akaniuliza.
“Vipi hali ya shangazi?”
“Bado anaumwa” nikamjibu huku nikiketi kwenye sofa.
Nikajifanya nataka kuangalia ile kanda. Zacharia aliondoka kwenye
mlango naye akaja kuketi.
“Kwani ana tatizo gani?” akaniuliza.
“Ni uzee tu. Kila mahali panamuuma. Na presha yake pia iko juu”
nikadanganya. Kwa kuwa sikutaka tuendelee na mazungumzo yale nikamuuliza.
“Kaka yako ameshalala?” nikamuuliza Zacharia.
“Ameingia chumbani muda mrefu”
“Mmekula nini?”
“Tumekunywa chai. Nilikwenda kununua mkate”
Nikajidai kumuuliza “Mmenibakishia na mimi?”
“Tumekuachia silesi zako”
“Mmefanya vizuri, njaa inaniuma”
Baada ya hapo tukabaki kimywa tukiangalia ile kanda. Kukaa kwangu
pale na kuangalia ile kanda ilikuwa ni kuvunga tu kwani nilijua nilikuwa
nimechelewa kurudi na nilikuwa na ile hisi ya kutenda dhambi.
Ghafla Ibrahim akatoka mle chumbani na kumuuliza mdogo wake.
“Shemeji yako hajarudi hadi muda huu?”
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment