HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE 20
ILIPOISHIA
Ushauri wa Rita haukunifurahisha. Ulikuwa kinyume na mawazo yangu.
Mawazo yangu yalikuwa ni kupanga jinsi ya kuachana na Ibrahim ili niolewe na
Chinga. Hata hivyo sikutaka kumfichulia Rita undani wangu. Nikamwaambia
“Naenda kumla tu. Si amejileta mwenyewe?”
“Huyo mumeo umemwambia unakwenda wapi?”
“Nimemwambia ninaenda Makorora kwa shangazi amaumwa”
Wakati tunazungumza na mimi nilijisogeza karibu na kioo cha kabati
na kuweka sawa nywele zangu pamoja na kuukwatua uso wangu kwa kutumia vipodozi
vya Rita.
Ilinichukua karibu nusu saa kujiweka sawa. Nilipohakikisha kuwa
nilikuwa nimependeza nikavaa baibui langu kisha nikatoa simu yangu na kumpigia
Chinga.
Simu ilipopokelewa nikamuuliza.
“Uko wapi Chinga?”
“Nipo hotelini” Chinga akanijibu kwenye simu kabla ya kuniuliza.
“Utakuja muda gani?”
“Ndio ninakuja”
“Unakuja sasa hivi?”
“Ndiyo ninatoka. Nitakwenda kukodi teksi”
“Sawa, basi ninakusubiri”
“Okey” nikakata simu na kumwambia Rita.
“Natoka. Jamaa ananisubiri hotelini”
Rita akanisindikiza hadi mlango wa mbele, nikatoka. Nilitembea kwa
miguu hadi kwenye kituo cha daladala ambako nilisubiri teksi itakayopita
niisimamishe. Katika eneo hilo
hakukuwa na kituo cha teksi cha karibu.
Nilipoona teksi haitokei na muda unazidi kwenda nikaamua kupanda
bodaboda.
SASA ENDELEA
“Nipeleke Chuda” nikamwaambia kijana mwenye pikipiki.
“Chuda sehemu gani?” akaniuliza
“Karibu na hoteli ya Mtendele”
Sikutaka kumwambia anipeleke moja kwa moja katika hoteli hiyo
kwani angenishuku vibaya.
“Kaa twende” akaniambia.
Nikajipakia nyuma yake. Pikipiki ikaondoka. Ingawa giza lilikuwa linaingia na
isingekuwa rahisi kwa mtu anayenifahamu kunitambua, niliuziba uso wangu kwenye
mgongo wa dereva wa bodaboda ili nisijulikane.
Mwendo wa nusu saa ukatufikisha Chuda.
“Simama hapa hapa” nikamwaambia kijana wa bodaboda tulipokuwa
tunaikaribia hoteli ya Mtendele.
Kijana akasimamisha pikipiki. Nikashuka na kumlipa pesa zake kisha
nikatembea kwa miguu kuelekea upande ilikokuwa hoteli ya Mtendele.
Nilipofika nilijipenyeza kwenye geti bila kusita. Kwenye ukumbi
kulikuwa na wateja wachache wakipata vinywaji. Sikuwajali, nikaenda mapokezi na
kumkuta msichana mwenzangu niliyemuulizia Chinga.
“Aliacha agizo kwamba akitokea mgeni wake aende chumbani kwake.
Yuko chumba namba 15, kipo ghorofa ya kwanza” msichana huyo akaniambia.
Nikapanda ngazi hadi ghorofa ya kwanza, nikakitafuta chumba namba
15 nikakiona.Nikaenda kubisha mlango. Nilibisha mara moja tu kasha nikasubiri.
Baada ya sekunde chache mlango ulifunguliwa. Chinga akatoa kichwa ukumbini.
“Oh! Salma karibu ndani” akaniambia aliponiona.
Alinipisha kwenye mlango, nikaoingia. Ilikuwa ni mara yangu ya
kwanza tangu niolewe na Ibrahim kuingia katika chumba cha hoteli na
mwanaume.
Kusema kweli baada ya kuingia humo chumbani niligwaya nikajihisi
kuwa ni mwenye hatia. Lakini nikajikaza ili nitimize lile nililokuwa
ninalitaka. Niliamini kabisa kwamba wakati ule sikuwa mimi kama
mimi, kulikuwa na nguvu ya shetani iliyokuwa ikinisukuma ndani ya moyo wangu.
Humo ndani kulikuwa na kitanda kipana cha sita kwa sita. Upande
mwingine kulikuwa na kabati la kioo. Katikati ya chumba kulikuwa na meza
iliyokuwa na chupa nne za bia, moja ikiwa tupu. Kulikuwa na pakiti la sigara na
kibiriti. Kando ya meza palikuwa na sofa moja.
Nikajua kuwa Chinga alikuwa ameketi kwenye sofa hilo akinywa bia. Nikataka kwenda kuketi
kitandani lakini nilibadili mawazo nikaenda kuketi kwenye lile sofa. Chinga
akafunga mlango. Alipoona nimeketi kwenye sofa yeye akakaa kitandani.
“Habari za nyumbani?” akaniuliza huku akitabasamu.
“Nzuri, za hapa?”
“Hapa kwema. Leo umependeza” akaniambia
Aliponiambia hivyo niliona aibu kwa sababu nilijua alishuku
kuwa nilijikwatua kwa ajili yake
“Kawaida tu” nikamwaambia kwa kuvunga kisha nikabadili mazungumzo
haraka.
“Ulikuwa unakunywa bia?” nikamuuliza
“Si unajua tena….” akanijibu bila kumaliza sentensi yake.
Akanyoosha mkono na kuichukua bilauli iliyokuwa imejaa kilevi akaipiga funda
kisha akairudisha juu ya meza
“Nikuagizie bilauli yako unywe kidogo kidogo?” akaniambia.
“Situmii na sina muda. Nimekuja mara moja tu tuzungumze ile habari
yetu kisha nirudi”
“Tunahitaji muda wa kutosha Salma. Mbona unaonekana kuwa na haraka
hivyo?”
“Si unajua bado niko mikononi kwa mtu. Kuondoka kwenyewe ni kwa
kuiba”
“Kwani umemwaambia unakwenda wapi?”
“Kwa shangazi Makorora. Nilidanganya kuwa shangazi anaumwa ili
nije huku”
“Hakushituka kuona unaondoka usiku?”
“Ni kwa sababu mchana nilikuwa na kazi ya kufua nguo”
“Sasa Salma tutafanya nini?. Unadhani suala lake litakuwa
kikwazo tusiwe pamoja?”
“Litakuwa kikwazo. Wewe si unataka kunioa?”
“Na umesema hataweza kukupa talaka hata kama
utaidai?”
“Hataweza kunipa”
“Je ukiifuatilia Bakwata?”
“Bakwata nikawaambie nini?”
“Kwamba huyo mwanaume hana uwezo wa kuishi na wewe, kwa hiyo unataka
muachane”
“Bakwata hawatakubali, wataona ninamkataa kwa sababu amepofuka.
Wataninasihi niendelee kuwa naye hivyo hivyo”
Chinga akapiga funda jingine la bia. Alipoirudisha birauli
aliniambia.
“Hatutakosa njia nyingine. Nakupa muda uendelee kufikiri lakini
jaribu kumshinikiza akupe taraka”
“Wewe utakuwa hapa Tanga mpaka lini?”
“Sina muda mrefu. Naweza kuondoka siku yoyote nitakayoamua”
“Basi tuendelee kufikiria njia nyingine. Kwa vile sina nia ya
kuendelea kuishi naye, kama hataniacha yeye
nitamuacha mimi!”
“Lakini umenipenda?” Chinga akaniuliza ghafla. Macho yake
yalionesha kuwa ulevi ulikuwa umeanza kumchukua. Iliwezekana alianza kunywa
muda mrefu.
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose uhondo huu nini kitatokea
No comments:
Post a Comment