HADITHI
YAMENIKUTA SALMA MIE 23
ILIPOISHIA
Akanyamaza kidogo kabla ya kuniuliza.
“Unamuonaje mgonjwa?”
“Bado anaumwa” nikamdanganya
“Cha mno ni nini hasa” akaendelea kuniuliza
“Mwili wote unamuuma. Pia ana presha”
“Presha gani, ya kushuka au ya kupnada?”
“Presha ya kupanda”
“Sasa amepata tiba?”
“Alipelekwa hospitali, anatumia dawa”
Nilipomjibu hivyo akanyamaza tena kidogo, kisha akaniambia.
“Mimi naenda kulala”
Sikumjibu kitu. Akageuka na kurudi chumbani. Kusema kweli nilikuwa
nimemchukia. Nilikuwa nikimuona kama mtu
anayenipotezea muda wangu bure.
Wakati alipotoka kule chumbani na kuja kuniuliza, nilidhani
angegomba. Nilikuwa nikingoja aseme neno lolote la kunituhumu nimnyambue kisha
ningetoka usiku ule ule na kurudi kwa Chinga.
Mkanda ulipokwisha nilikwenda mezani nikanywa chai na silesi
walizoniachia kisha nikaingia chumbani.
Asubuhi kulipokucha wakati ninafanya usafi wa nyumba nilienda uani
nikampigia simu Chinga kumsalimia.
Akafurahi nilivyompigia simu asubuhi ile.
“Umeshaamka au bado umelala?” nilimuuliza baada ya kukosa maneno
ya kuzungumza.
“Bado niko kitandani”
“Kitandani hadi muda huu?”
“Ni harakishe nini, sina pa kwenda”
SASA ENDELEA
“Una raha mwenzetu. Natamani nije tulale sote”
“Sasa nani anakuzuia?”
“Si huyu ‘mnoko’ anayenipotezea muda wangu” nilimaanisha Ibrahim.
“Jana uliporudi alikuambia nini?”
“Hakuniambia kitu, si anajua nilikuwa kwa shangazi”
“Sasa mbona unasema anakuzuia usije huku?”
“Hanizuii lakini si ndiye kikwazo changu. Natamani niliue
niondoke”
Chinga akacheka kwenye simu.
“Usimuue utapata hatia, tumia taratibu atakuacha tu. Hakuna ndoa
ya lazima”
“Ataniacha lini wakati mimi nataka niondoke hata sasa hivi?”
“Usiwe na haraka hivyo. Mimi nitakusubiri tu”
“Si unataka kurudi Dar”
“Hata kama nitarudi Dar, sitakaa sana nitakuja tena kwa ajili yako”
“Nataka ukiondoka tuondoke sote. Hata kama sijapewa talaka, huyu
mwanaume nitamuacha tu”
“Basi tutazungumza, si utakuja usiku?’
“Leo sitakuja,tufanye kesho ila nitakupigia simu usiku”
“Sawa”
Nilitegemea Chinga angekata simu lakini simu haikukatwa,
nikamuuliza.
“Mbona hukati simu?”
“Kata wewe” akaniambia.
“Kata wewe bwana!” na mimi nikamwaambia.
Chinga akacheka kisha akakata simu.
Nilipokuwa narudi ndani nikamuona Ibrahim nyuma ya mlango
akipapasa ukuta akielekea upande wa chumbani kwetu. Nikajiuliza ni kitu gani
kilichomleta nyuma ya mlango?. Sikupata jibu. Lakini nilishuku kuwa pengine
alikuwa akisikiliza nilivyokuwa ninaongea na Chinga.
Nikajiambia kama ametusikia atakuwa ameijua siri yangu wakati mimi
sikutaka aujue uhusiano wangu na Chinga.
Ingawa sikuwa na uhakika kwamba alikuwa akitusikiliza au la lakini
nilijiambia kama ametusikia nitajua kwani ni
lazima ataniuliza.
Na nilingoja aniulize ndipo nimueleze wazi kuwa nilikuwa nimemchoka
na nilihitaji kuondoka kwake, hivyo anipe talaka yangu.
Ibrahim akaingia chumbani na mimi nikaingia humo humo ili kama amesikia kitu aniulize. Lakini Ibrahim hakuniuliza
chochote.
Ilipofika saa nne nilitoka bila kumuaga nikaenda sokoni.
Niliporudi niliingia jikoni. Nilikuwa nimenunua samaki,mchele na
vitu vingine. Pesa ya Chinga ilikuwa inafanyakazi.
Nikaanza kupika. Hadi saa saba mchana wali ukawa tayari.
Nikawatengea Ibrahim na mdogo wake kwenye meza na mimi kama
kawaida yangu nilijipakulia kiasi changu nikaenda kukaa uani.
Wakati ninakula nilijiuliza, mbona Ibrahim hakuniuliza kitu wala
hakuonesha kukasirika?.Huenda hakuyasikia mazungumzo yangu na Chinga. Moyo
wangu ukapata faraja kidogo.
Ilipofika mida ya jioni nikamwaambia Ibrahim kuwa ninakwenda kwa Rita
kuzungumza. Si kwamba nilikuwa nimebadilika na kuamua kumpa heshima yake ya
kumuaga kila ninapotaka kutoka, lahasha. Kumuaga huko kulikuwa ni kuzuga
tu kama vile namfanya mjinga. Mbona nikiwa na
safari zangu za maana nilikuwa simuagi!
Nilichukua muda mwingi nikiwa kwa jirani yangu Rita tukizungumza
hili na lile lakini kubwa tuliloliongelea ni kuhusu uhusiano wangu na Chinga.
Kwa vile msimamo wa Rita ulikuwa nisiachane na Ibrahim kwa kuwa
mimi ndiye niliyemsababishia matatizo ya macho, sikumueleza undani wangu kuwa
nilitaka niolewe na Chinga kwa sababu angeupinga uamuzi wangu huo.
ITAENDELEA
No comments:
Post a Comment