Tuesday, January 27, 2015

HADITHI, YALIYONIKUTA TANGA (5)




HADITHI

YALIYONIKUTA TANGA (5)

ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA

“Unafanya kazi gani?” Msichana akaniuliza.

Niliona nisimueleze ukweli kwani watu wengi huwaogopa polisi na makachero.

“Mimi ni afisa ardhi”

“Afisa ardhi unagawa viwanja?”

“Ni moja ya kazi zangu. Sasa naweza kuja kukuona?’

“Kwani unataka nini?”

“Kujuana na wewe”

“Tukishajuana iweje?”

Nikajidai kucheka.

“Mbona unacheka?” Msichana akawahi kuniuliza.

“Unanifurahisha sana. Kwani hupendi tukiwa marafiki?’

“Wewe unapenda kuwa rafiki na mtu ambaye humjui?”

SASA ENDELEA

“Ndiyo sababu nikataka tuonane tujuane”

Baada ya kimya kifupi msichana akaniambia.

“Usiwe na haraka, subiri kwanza”

“Hadi lini?”

“Nitakwambia. Sawa?”

“Inabidi nikubali kwa shingo upande”

“Mwanaume wewe wa ajabu sana!” Msichana akaniambia kisha akakata simu. Sikujua alikuwa na maana gani kuniambia hivyo.

Ikapita karibu wiki nzima bila kuwa na mawasiliano na msichana huyo. Si tu nilikuwa nimetingwa na kazi pia simu ya msichana huyo ilikuwa haipatikani. Ilikuwa imezimwa kabisa. Mpaka nikafikiria kuwa alikuwa amebadili namba.

Nilijaribu kumpigia mara kadhaa. Nilipoona sipati jibu nikaacha kumpigia. Baada ya kupita wiki moja nilikuwa nikichaji simu yangu. Ilikuwa jioni na ndio kwanza nilirudi kutoka kazini. Kwa kawaida ninapochaji simu yangu huwa naizima.

Nilianza kuichaji kutoka saa kumi na mbili jioni hadi saa tatu usiku nilipoiwasha. Simu yangu ilipowaka nikaona meseji iliyotoka kwa yule msichana ikiuliza.

“Utakuwa na nafasi leo?”

Sikujua meseji ile aliituma muda gamin nikaijibu haraka.

“Ninayo nafasi, uko wapi?”

Baada ya kutuma jibu hilo sikupata jibu jingine. Nilipoona muda unazidi kwenda nikaamua kumpigia.

Simu iliita kwa muda mrefu kisha ikapokelewa.

“Hallow…mbona umechelewa kunipigia?” Sauti ya msichana ikauliza.

“Nilikuwa nachaji simu, meseji yako nimeiona sasa hivi”

“Niliituma tangu saa moja, nikaona kimya”

“Kwani hatuwezi kuonana muda huu?”

“Tunaweza kama utaweza kufika huku muda huu”

“Kwanini nisiweze wakati boda boda zipo”

“Sawa, njoo basi”

“Nitakukuta wapi?”

“Njoo hadi hapa Mbuyu Kenda kisha nipigie simu”

Sikuwa nikipafahamu mahali hapo lakini nilijua mwenye bodaboda nitakayemkodi atakuwa anapajua mahali hapo.

“Sawa, ninakuja” nikamwambia.

“Ukifika Mbuyu Kenda utanipigia simu” akarudia kuniambia.

“Sawa”

Msichana akatangulia kukata simu. Nilikuwa nimejilaza kitandani, nikakurupuka na kuvaa shati kisha nikatoka. Wakati naelekea barabarani nilimpigia simu jamaa mmoja mwenye bodaboda niliyekuwa namfahamu.

“Uko wapi?” nikamuuliza mara tu alipopokea simu.

“Niko stendi” akanijibu.

“Nifuate hapa Mabanda ya Papa”

“Sawa, ninakuja”

“Usichelewe”

“Nimeshawasha pikipiki, ninakuja”

Nikakata simu. Nilitembea haraka haraka kutoka zilipokuwa nyumba za polisi hadi eneo hilo la Mabanda ya Papa. Ulikuwa mwendo ulionichukua dakika tatu tu.

Nikasimama pembeni mwa mzunguko wa barabara nne uliokuwa mahali hapo. Mara nikamuona mwenye bodaboda niliyempigia simu, nikampungia mkono. Alipunguza mwendo akaja kusimama karibu yangu.

Nikapanda nyuma yake.

“Twende wapi?” akaniuliza.

“Twende Magomeni”

“Magomeni ipi?”

“Unapafahamu Mbuyu Kenda?”

“Ndipo unapokwenda?”

“Nipeleke hapo hapo”

Nikaondoka na yule mwenye bodaboda. Tuliliacha jiji tukashika barabara ya Majengo. Tulipoiacha Majengo tukaingia Mapinduzi. Barabara ya Mapinduzi ndiyo iliungana na barabara ya Magomeni.

Robo saa baadaye mwenye bodaboda akanisimamisha pembeni mwa mbuyu uliokuwa kiza. Mbuyu huo ulikuwa kando ya barabara.

“Ndio hapa?” nikamuuliza yule kijana huku nikiangaza macho kila upande. Kote kulikuwa kiza. Nyumba chache tu zilizokuwa zinawaka taa ya umeme.

“Ndio hapa”

Nilitaka nitoe simu nimpigie yule msichana nimwambie kuwa nimefika lakini sikutaka yule kijana ajue nilimfuata nani pale, nikashuka kwenye pikipiki.

“Nisubiri” nikamwambia na kwenda kusimama kando.

Nikatoa simu na kumpigia msichana niliyekuwa nimemfuata pale.

“Nimeshafika”  nikamwambia alipopokea simu.

“Upo Mbuyu Kenda?” akaniuliza.

“Ndiyo”

“Subiri” akaniambia.

Je nini kitatokea? Usikose kuendelea na hadithi hii kesho
Zaidi usiache kutembelea blog yangu mtu wangu, www.tangakumekucha.blogspot.com




No comments:

Post a Comment