HADITHI
YALIYONIKUTA TANGA (8)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Nikairudisha ile simu
mfukoni. Wakati nairudisha ilikuwa kama
ninaizima akili yangu kwani hapo hapo sikujielewa tena. Sikujua kama nilipotewa
na fahamu au nilipitiwa na usingizi wa ghafla. Sikuweza kujua.
Nilipozinduka nilijiona
nimechoka, kitu ambacho kilinipa dalili kuwa nililala kwa muda mrefu pale
kwenye kochi.
Nikatazama saa yangu na kuona ilikuwa saa tisa usiku. Nikataharuki. Mwenyeji wangu
hakuwepo. Nilikuwa bado niko peke yangu.
Nikajiuliza Maimuna alikuwa
amekwenda wapi tangu muda ule. Nikanyanyuka na kuanza kumtafuta mwenyeji wangu.
Niliingia ukumbini nikaita “Maimuna!”
Lakini sikupata jibu.
Nikasukuma mlango wa chumba cha kwanza ambao ulikuwa wazi. Nikachungulia ndani.
Chumba kilikuwa kitupu lakini kulikuwa na boksi kubwa lililowekwa nyuma ya
mlango.
Nilichungulia ndani ya lile
boksi nikaona kitu kilichonishitua. Nikaingia mle chumbani na kutazama vizuri.
Ndani ya lile boksi niliona kichwa cha binaadamu, tena kilikuwa kichwa cha
Sajenti Erick!
SASA ENDELEA
Kwa kweli nilipatwa na
mshituko mkubwa. Vile ambavyo nilitoka usingizini nilijihisi kama
nilikuwa kwenye ndoto ya kutisha. Kwa kutoamini macho yangu nilikitazama kile
kichwa tena na tena. Akili yangu ilinithibitishia kuwa sikuwa kwenye ndoto na
nilichokiona ni kichwa cha binaadamu na ni cha Sajenti Erick!
Nikawa najiuliza Sajenti
Erick alichinjwa muda gani na alichinjwa na nani na kwanini kichwa chake kipo
pale? Nikakumbuka kwamba nilipigiwa simu na kachero mwenzangu aliyenieleza
kuhusu kutoonekana kazini kwa Sajenti Erick mchana kutwa wa siku ile.
Kile kichwa kwa jinsi
kilivyoonekana hakikuchinjwa muda mrefu. Jeraha lake lilikuwa
bado bichi na lilikuwa linavuja damu. Macho ya Sajenti Erick yalikuwa wazi
kuonesha kuwa wakati anachinjwa alikuwa ameshituka.
Akili ya kupelelezi ikaanza
kunijia. Nikazungusha macho yangu kwenye kile chumba. Sikuona mahali popote
palipokuwa na damu, hali iliyoonesha kuwa Sajenti Erick hakuchunjwa mle chumbani.
Wakati nayarudisha macho
yangu kwenye lile boksi nikaona magazeti kwenye pembe moja ya kile chumba.
Nikaenda kuyatazama. Yalikuwa magazeti mawili yaliyowekwa pamoja. Juu ya
magazeti hayo kulikuwa na kete tatu ambazo nilishuku zilikuwa kete za kokeni.
Nilizishika na kuzinusa. Kwa
vile nilikuwa na uzoefu na unga huo haramu niligundua harufu yake. Ilikuwa ni
kokeni. Nikaziweka kando. Sasa nilishika yale magazeti. Nilianza kuangalia
mojawapo. Kwenye ukurasa wa mbele kulikuwa na habari ya ajuza (kikongwe)
aliyekamatwa Tanga na kete za madawa ya kulevya.
Picha yake ilikuwa imechapwa.
Nilipoitazama nikagundua ilikuwa ni ya yule mwanamke tuliyemkamata siku ile
mimi na Sajenti Erick. Kumbe habari zake zilichapwa kwenye gazeti. Nikatazama
tarehe ya lile gazeti nikaona ni la siku za nyuma.
Nikashika lile gazeti
jingine. Katika ukurasa wake wa mbele kulikuwa na habari iliyohusu kifo cha
yule kikongwe ambacho kilitokea katika mahabusi ya polisi.
Mpaka muda ule nilikuwa
sijaelewa kitu. Nilikuwa nikijiuliza mengi ambayo hayakuwa na majibu. Wakati
naliweka lile gazeti nikaona kitone cha damu kikidondoka kwenye kiganja changu.
Nikashituka na kutazama juu.
Huko juu niliona kitu cha
kushitusha. Niliuona mwili wa Sajenti Erick usio na kichwa ukiwa umening’inizwa
kwenye miti iliyopaulia nyumba! Lile jeraha la kwenye shingo ndilo
lililotonesha tone la damu lililotua
kwenye kiganja changu.
Mwili ule uliunda picha ya
kutisha sana
hasa kwa vile mtu mwenyewe nilikuwa namfahamu. Ujasiri wa kipolisi niliokuwa
nimebaki nao uliniishia pale pale. Kama
nisingekuwa makini ningekurupuka na kutoka mbio kwani hisia zangu zilishanusa
hali ya hatari.
Nilijua kuwa hata mimi maisha
yangu yalikuwa hatarini. Mahali nilipoingia palikuwa sipo!. Nikainua hatua ili
nitoke katika kile chumba. Baada ya kupiga hatua mbili nilikanyaga mahali
palipotitia! Nikajiona natumbukia chini.
Lilikuwa shimo la urefu wa kama futi nne. Miguu yangu ilipotua chini nikaona kitu
kinanizongazonga kwenye miguu kikinipandia juu. Nikajaribu kukishika. Nikaona
nimeshika kichwa cha nyoka!
“Yesu wangu!” nilishituka na
kukivuta juu. Haikuvutika kwani sehemu yake ya mkia ilikuwa imenizonga kwenye
mguu. Nilitaka kuwania kupanda juu ya lile shimo nitoke lakini nilijiambia nikikiacha kile kichwa
nyoka yule atanigonga.
Nikakipeleka kichwa hicho
chini ya mguu mwingine kisha nikakikanyaga kwa kupiga mguu wangu chini. Kile
kichwa kilipasuka. Ndipo nilipoweza kutoka kwenye lile shimo. Nilikuwa nahema kama niliyekuwa nafukuzwa.
Nilipotoka tu kwenye shimo hilo nilikwenda ukumbini
nikaelekea kwenye mlango wa nje. Nilipoushika ili niufungue nikaona ulifungwa
kwa nje. Mlango haukufunguka!
Nikasikia sauti za watu
waliokuwa wakizungumza huko nje. Sauti ya mwanaume na mwanamke. Zilikuwa
zikisikika kwa mbali lakini zilikuwa zikikaribia kwenye ule mlango. Nikajua ni
watu wanakuja.
Nikatega masikio
kuwasikiliza.
“Sasa mama yuko wapi?”
Ilikuwa sauti ya kiume iliyouliza.
“Mama yuko uani, anachimba
kaburi kabisa” Sauti iliyojibu niliitambua, ilikuwa ni ya yule msichana
aliyenikaribisha mle ndani.
“Na huyo polisi mwingine
aliyewabambikia kesi yuko wapi?” Ile sauti ya kiume ikauliza tena.
“Nilimuacha ukumbini amelala,
sijui kama atakuwa ameamka”
“Sasa acha tumshughulikie na
yeye kama mwenzake”
“Mama yangu, nimekwisha!”
nikajiambia niliposikia maneno hayo. Kumbe tatizo lilikuwa ni ile kesi
tuliyombambikia yule mwanamke.
Sasa akili yangu ilitanzuka.
Nilimkumbuka yule msichana. Alikuwa ndiye yule aliyekuwa na yule mwanamke
kwenye ile nyumba tulipokwenda kuwakamata. Yule msichana alikimbia,
tukamshikilia mama yake peke yake.
Kwa hofu kwamba ningeuawa kama alivyouawa Sajenti Erick, nilikimbilia kwenye mlango
wa uani. Niliukuta mlango upo wazi, nikatoka uani ambako kulikuwa kiza lakini
kulikuwa na mbalamwezi.
Kwenye pembe moja ya ua huo nilimuona
bibi mmoja ameshika shepe akichimba shimo. Nilipomuona tu nikakumbuka yale
maneno ya yule msichana niliyemsikia akisema “Mama yuko uani, anachimba kaburi
kabisa”
Nikajiuliza lilikuwa kaburi
langu au ni la Sajenti Erick? Wakati namtazama yule bibi nikamkumbuka. Alikuwa
ni yule mwanamke tuliyemkamata na kumbambikia kesi ya kumkuta na madawa ya
kulevya.
Jambo ambalo lilinishangaza
ni kuwa mwanamke huyo alikufa akiwa mahabusi lakini muda ule nilimuona akiwa
hai tena akionekana akiwa na nguvu za kutosha.
Kitu ambacho kilikuwa cha ajabu zaidi ni kuwa bibi
huyo alikuwa uchi wa mnyama na mwili wake ulikuwa umejaa manyoya meupe marefu.
Nikaiona miguu yake, ilikuwa na kwato kama
miguu ya punda!
Je nini kitatokea? Usikose kuendelea
na hadithi hii kesho.
Na usisite kutembelea blog hii kila wakati kwa habari nyingi nzuri na za kusisimua, ni tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment