Wednesday, January 28, 2015

SOMA HABARI KUU ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO,TZ

Mkusanyiko wa Stori muhimu zilizopewa Headlines kwenye Magazeti ya leo January 28, 2015

room
NIPASHE
Jeshi la Polisi jana lilitumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), kwa kurusha mabomu, risasi za moto na maji ya kuwasha, na kumkamata Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi wengine wapatao 32.
Nguvu hiyo ya Polisi ilitumika wakati wa kuzuia msafara wa Mwenyekiti huyo kuelekea eneo la Zakhem, Mbagala, kulikokuwa kumeandaliwa na mkutano wa hadhara, kutoa taarifa kwa wafuasi waliokuwa wamekusanyika, kuwa mkutano na maandamano yamezuiliwa na Polisi.
Mkutano huo ambao ungetanguliwa na maadamano kutoka ofisi za wilaya ya Temeke kwenda Zakhem kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 14 ya mauaji ya wafuasi wake zaidi ya 30 waliouawa Januari 27, 2001 na Jeshi la Polisi Zanzibar wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar wa mwaka 2000.
Kutokana na purukushani hizo za jana, polisi wenye silaha na virungu walitembeza kichapo kikali kwa wafuasi waliokaidi amri ya polisi kuwataka watawanyike, huku wakiwashusha waliokuwa kwenye magari.
Baada ya kipigo cha dakika 30, polisi wakiongozwa na S .Zacharia, ambaye mara kwa mara alizungumza na Prof. Lipumba na viongozi wengine kutawanyika bila mafanikio, walimteremsha kwenye gari na kumpakiza kwenye gari ya polisi.
Katika kamatakamata hiyo wafuasi zaidi ya 15 walitembezewa kichapo na kuswekwa kwenye gari tatu za polisi, huku katika gari lililombeba Prof. Lipumba akiwa na wafuasi wengine wawili.
NIPASHE
Matukio ya uporaji silaha yameendelea kuliandama Jeshi la Polisi  nchini baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kuwapora askari wake bunduki mbili aina ya SMG kisha kumjeruhi kwa kumchona kisu mmoja wao.
Tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia jana katika Jiji la Tanga,  pia lilihusisha uporaji wa risasi kutoka kwa walinzi hao wa usalama wa raia na mali zao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, alisema kuwa  tukio hilo lilitokea juzi saa 5:15 usiku katika eneo la barabara ya tano mjini Tanga.
Kamanda Ndaki alisema katika tukio hilo, askari mmoja PC Masoul alichomwa kisu na amelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kwa matibabu.
Alisema askari huyo alipata mkasa huo wakati akiwa na mwenzake PC Mwalimu wakiwa katika doria mjini Tanga na ghafla walivamiwa na watu ambao wanasadikiwa kuwa majambazi kisha kuwapora bunduki hizo.
NIPASHE
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ameanza kukumbana na changamoto za wizara hiyo baada ya kukutana na wasafirishaji wawili wa dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) waliokuwa na kete zaidi 154 aina ya Heroine zenye thamani ya mamilioni ya fedha kwenda nje ya nchi.
Sitta alikutana na wauza ‘unga’ hao ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu Rais Jakaya Kikwete alipofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na kumteua kuwa Waziri wa Uchukuzi akibadilishana na Dk.Harrison Mwakyembe ambaye amehamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Watuhumiwa hao ambao Sitta alikutana nao katika uwanja huo wakiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa uwanja huo ambao wote ni raia wa Tanzania ni wanawake (33), mkazi wa Sinza na wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa wanawake hao alikuwa na hati ya kusafiria namba AB 651920 wakati mwingine alikuwa na hati ya kusafiria namba AB 636250, walikamatwa Januari 23, mwaka huu saa 5:15 usiku wakitaka kusafiri kwa ndege ya shirika la Emirate.
MTANZANIA
Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wameandamana hadi kituo cha Polisi cha Kati, wakidai wapewe taarifa wapi alipopelekwa Mwenyekiti Taifa wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Johnson Minja.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walifunga maduka yao jana na kuandamana wakishinikiza kuachiwa huru kwa Minja, ambaye aliondolewa katika Kituo cha Polisi Kamata bila taarifa rasmi.
Maandamano hayo ya wafanyabiashara, yalikumbana na ulinzi mkali wa askari nje ya jengo la Kituo cha Kati na kuishia nje.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya wafanyabiashara kujaa maeneo ya kituo hicho cha Polisi, Kamanda Siro alithibitisha kupata taarifa ya maandamano hayo na pia kushikiliwa Minja na Jeshi hilo ambapo alisema amepelekwa Dodoma na kamba yuko salama.
Ni kweli Minja amekamatwa lakini tukio lililomfanya akamatwe alilifanya Dodoma, amesafirishwa kupelekwa huko ambako kesi yake iko na kesho atafikishwa mahakamani:- Siro.
Siro alilaani kitendo cha wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufanya maandamano ambayo ni kinyumwe cha sheria.
HABARILEO
Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma itawaweka kiti moto watuhumiwa 9 ambao ni viongozi wanaohusishwa na kashfa ya uchotwaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.
Viongozi hao watawekwa kiti moto kwa uwazi mwanzoni mwa mwezi ujao kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Habari zinaeleza kuwa watakaoitwa ni viongozi wote, wanaowajibika chini ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka ndani ya Tume ya Maadili, zilieleza kuwa kwa sasa hati za kuitwa kwa watuhumiwa hao zinaandaliwa.
Hata hivyo sheria ya maadili ya viongozi wa umma, inawabana viongozi na watumishi wa ngazi ya juu wa umma, wakiwemo wabunge, wakuu wa wilaya, mikoa, majaji na mawaziri na mwanasheria mkuu.
HABARI LEO
Imani za ushirikina, ajali na vitendo vya ukatili dhidi ya binadamu vimesababisha wananchi wa mikoa ya Mbeya kugubikwa na simanzi kutokana na mauaji ya kutisha.
Imeripotiwa kuwa watu watatu wamefariki dunia mkoani hapa katika matukio tofauti yakiwemo mawili ya mauaji ya kinyama.
Miongoni mwa matukio ya mauaji hayo ni pamoja na la mkazi wa kijiji cha Mkutano wilayani Momba, Hamis Simwawa (25) aliyekutwa shambani akiwa ameuawa kwa kukatwa shoka shingoni na kisha kunyofolewa viungo vya mwili ikiwemo ulimi, meno ya chini na jicho la kushoto.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Barakael Masaki alisema mwili wa Hamis ulikutwa Januari 26 mwaka huu majira ya saa mbili asubuhi katika kijiji cha Mkutano kilichopo katika kata ya Nzoka wilayani Momba.
Kaimu Kamanda Masaki alisema kabla ya mauaji kijana huyo aliitwa kwenda kusaidia shughuli za shamba na alipofika shambani ndipo walimuua kwa kumkata na shoka shingoni kabla ya kumnyofoa ulimi, meno ya chini na jicho la kushoto na kupeleka viungo hivyo kusikojulikana.
Alisema tukio hilo linahusishwa na imani za kishirikina ambapo Kawawa Sinkala (31) na Emmanuel Sinkala (15) wakazi wa kijiji cha Mkutano wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.
MWANANCHI
Ni wazo ambalo limekuwa, lakini halizungumzwi bayana, lakini Jukwaa la Katiba lilidiriki kuweka bayana kuwa wagombea wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, wapime afya zao kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alilitoa ushauri huo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana na kusisitiza kuwa wagombea wa nafasi hiyo nyeti na wagombea wenza wapime afya na majibu yao kuwa wazi ili kuepuka gharama zisizo za lazima ya mtu ambaye atashinda uchaguzi na kupewa ukuu wa Serikali.
Kibamba ameweka ajenda mpya kwenye mjadala wa urais wakati nchi ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu na ambao utatoa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano. Uadilifu, usafi, uzalendo na uwezo ndio zimekuwa mada kubwa kwenye mjadala wa urais hadi sasa.
Lakini Kibamba, ambaye alikuwa mmoja wa waangalizi wa uchaguzi Mkuu wa Rais nchini Zambia uliofanyika wiki iliyopita baada ya kufariki kwa Rais Michael Satta, alisema wamepata fundisho baada ya marais wawili wa nchi hiyo kufariki dunia wakiwa Ikulu katika kipindi cha miaka sita.
Suala la viongozi kupima afya hapa nchini limekuwa ni siri sana, lakini kwa mfano huu, hakuna budi viongozi kupima na kubainisha majibu ya afya zao ili kuangalia kama wanaweza kumudu mikikimikiki ya urais bila kuiingiza nchi kwenye gharama ya kuwatibu kila mara tena kwenye hospitali za nje:-Kibamba
MWANANCHI
Hofu kuhusu nafasi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao inazidi kuongezeka baada ya mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kukitabiria chama hicho tawala “kazi kubwa”, akisema hali ya sasa “siyo ile iliyokuwa nayo miaka mitano iliyopita”.
Kagasheki pia alikitahadharisha chama hicho dhidi ya kuzidi kukua kwa nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema iwapo umoja huo utamchagua mgombea makini, CCM itakuwa na kazi ngumu.
Kauli yake inaungana na za vigogo wengine wa CCM waliotahadharisha mwenendo wa chama hicho dhidi ya ongezeko la nguvu ya upinzani, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, ambaye alisema rushwa inakimaliza chama hicho, na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye alisema kuwa chama hicho kisitegemee ushindi wa kishindo.
Akijibu swali la maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao na nafasi ya CCM, Kagasheki alisema: “Ipo kazi, nafasi ya CCM sasa… Jamii imeanza kuwa na maswali mengi kuhusu chama chetu, viongozi wachukue hili kwa umakini, wakifuatilia watajua.”
Mbunge huyo alisema kuwa matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni yametokana na wananchi kuona CCM imeshindwa kuisimamia vizuri Serikali.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia,www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment