Kumekucha blog
Tanga,WAKURUGENZI
na Waganga wakuu wa hospitali za Wilaya Mkoani Tanga, wametakiwa kupita kila
kijiji na kitongoji kutoa elimu ya kujiunga
na mfuko wa bima ya afya ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo iliyojiwekea.
Akifungua kikao cha kujadili mpango
wa mfuko wa Afya ya jamii na kusaini mkataba wa uhamasishaji wa CHF kwa Wilaya
ya Lushoto na Muheza leo, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Salim Mohammed Chima
alisema elimu ya mfuko wa afya ya jamii inahitajika na kuwataka viongozi wenye
dhamana kuacha kujifungia maofisini.
Alisema viongozi wengi wamekuwa
wakishindwa kutekeleza wajibu wao wakiwemo watu wenye dhamana kushindwa kuhamasisha jamii kujiunga na mifuko wa bima
ya afya ya jamii.
“Leo nawafungulia kikao chenu wenyewe
cha kujadili na kuweka mikakati ya jamii kujiunga na mfuko wa afya ya
jamii---baada ya hapa kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake” alisema Chima
na kuongeza
“Tumekuwa tukikemea tabia ya wakuu wa
idara na viongozi wenye dhamana kujifungia maofisini na kushindwa kutekeleza
wajibu wao kwa mujibu wa mikataba ya utumishi wa umma” alisema
Alisema tabia ya viongozi kujifungia
maofisini na kuacha kutekeleza wajibu wao ataikomesha ikiwemo utoro pamoja
na muda wa kuingia na kutoka kazini na hivyo kutoa agizo la kila mmoja kujua
wajibu wake katika kazi.
Awali akizungumza katika kikao hicho,
Mganga mkuu wa Mkoa, Asha Mahita, alipinga vikali ukosefu wa madawa katika
hospitali zake na kuwabebesha mzigo waganga wa hospitali za Wilaya kwa uzembe
wa kuacha kuagizia dawa.
Alisema malalamiko yanayotoka kwa
wananchi juu ya ukosefu wa madawa ni uzembe wa waganga wakuu wa hospitali na
hivyo kutoa wito kwa kila mmoja kuhakikisha kituo chake kinakuwa na dawa za
kutosha ili kuondosha malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Hakuna ukosefu wa madawa hospitalini
na ikotokea ni waganga wakuu wa hospitali kufanya uzembe wa kuacha
kuagizia-----dawa zipo za kutosha na hili nitalishughulikia mimi mwenyewe”
alisema na kuongeza
“Tena natoa wito kwa wananchi popote
katika mkoa huu mgonjwa aendapo hospitali na kuelezwa kuwa hakuna dawa
awasiliane na ofisi yangu au mimi mwenyewe nitalivalia njuga ” alisema Mahita
Kwa kauli hiyo, Mahita aliwataka
waganga wakuu wa hospitali za Wilaya kuhakikisha vituo vyao havipungukiwi na
madawa na kudai kuwa hakuna upungufu huo na yoyote ambaye atafanya uzembe
atamchukulia hatua.
Mwisho
No comments:
Post a Comment