YALIYONIKUTA
TANGA (4)
ILIPOISHIA
TOLEO LILILOPITA
“Ngojeni
gari ije twende kituoni ndipo mtakapojua kosa lenu” Erick aliwambia baada ya
kuhakikishiwa kuwa gari la polisi linatufuata.
Yule binti
alitutoroka pale pale na kupotea. Tukabaki na yule mwanamke.
“Binti yako
ametukimbia lakini tutamtafuta” Erick alimwambia yule mwanamke polisi wenzetu
walipofika.
Tulimtoa
yule mama, tukamwambia afunge mlango wake. Alipofunga mlango wa nyumba yake,
funguo zake nilizichukua mimi. Tukampakia kwenye gari la polisi na kwenda naye
kituoni.
Wakati
mwanamke huyo anahojiwa ndani ya kituo cha polisi, mimi nilitoka nikakodi
bodaboda na kurudi nyumbani kwake. Kile kisanduku cha dhahabu kilikuwa
kimenitoa roho na Erick alikiacha baada ya kuona ilikuwa mali halali ya yule
mwanamke.
Nilifungua
mlango wa nyumba yake kwa kutumia zile funguo ambazo nilikuwa nazo mfukoni.
Nikaingia ndani. Nilikichukua kile kisanduku cha dhahabu nikakifunga na
kitambaa cheupe nilichokikuta mle chumbani kisha nikatoka. Nilipotoka nilikodi
teksi ikanipeleka nyumbani kwangu Msambweni ambako kulikuwa na nyumba za
polisi.
SASA ENDELEA
Nlipofika
nyumbani kwangu, niliingia ndani. Nilikificha kile kisanduku chini ya mvungu wa
kitanda changu kisha nikatoka tena na kurudi na ileteksi kituo cha polisi. Zile
funguo zanyumba ya yule mwanamke nilizikabidhi kwa Sajenti Erick.
“Nilizisahau
mfukoni mwangu” nikamwambia.
Erick
alizichukua nakwenda kuzihifadhi kwenye kabati.
Yule
mwanamke alikuwa amehojiwa na baadaye kupelekwa rumande. Niliambiwa alikuwa
amekanusha kuhusika na zile kete za madawa ya kulevya. Polisi walikuwa katika
pilikapilika za kuandaa mashitaka yake ili kesho yake afikishwe mahakamani.
Kusema kweli
kukamatwa kwa yule mwanamke hakukuwa halali Sajenti Erick alikuwa ameweka mtego
wake apate pesa kwa njia ya kumtisha yule mwanamke lakini mwanamke mwenyewe
hakutishika na akawa tayari ashitakiwe kwa kosa la kukutwa na kete za madawa ya
kulevya ambazo alizikana.
Siku
iliyofuata mwanamke huyo akafikishwa mahakamani. Alisomewa shitaka la kukutwa
na kete tatu za madawa ya kulevya, akakana shitaka hilo. Kesi ikaahirishwa nay
eye akarudishwa rumande kwa kukosa mdhamini.
Niliusifu
sana ujasiri wa Sajenti Erick, kumfungulia kesi mwanamke huyo mzee huku akijua
fika kwamba hakuwa na hatia. Zilikuwa ni chuki za kutopata pesa alizotaka
kutoka kwa mwanamke huyo.
Na hata kama
angebadili mawazo yake, asingeweza kumuachia kwa sababu mtuhumiwa tayari
alishafikishwa kituo cha polisi. Mambo hayoyalitakiwa yamalizikie kule kule
nyumbani kwa yule mama.
Polisi
hawakushughulika tena kumtafuta yule msichana aliyetoroka, wakamng’ang’ani yule
mama. Siku ile ambayo alifikishwa mahakamani siku iliyofuata akakutwa
ameshakufa.
Maiti yake
ilikutwa asubuhi. Ikachukuliwa na kupelekwa hospitali. Sajenti Erick akapata
kazi ya kuwatafuta jamaa zake bila mafanikio. Majirani wa yule mama walimwambia
Erick kwamba hawawajui jamaa zake. Walikuwa wakimuona yeye na yule binti
aliyekuwa naye ambaye alikuwa ametoweka tangu siku alipokamatwa yule mama.
Kesi yake
ikafutwa mahakamani. Na baada ya kutojitokeza kwa jamaa yake yeyote, maiti ya
mwanamke huyo ikazikwa na manispaa. Tukio lile tukalisahau.
Zikapita
siku kadhaa. Kile kisanduku cha dhahabu kilikuwa bado kipo mvunguni mwa kitanda
changu. Sikutaka kuziuza haraka haraka zile dhahabu. Nilikuwa nikisubiri muda
upite na tukio lisahaulike kabisa.
Siku moja
asubuhi wakati natoka nyumbani kwangu naenda kazini simu yangu iliingia meseji.
Nilipoisoma ilisema.
“Sitalisahau
penzi lako”
Namba
iliyotuma meseji hiyo nilikuwa siifahamu. Na mimi nikatuma meseji ya kuuliza.
“Wewe nani?”
Baadaye
likaja jibu likisema.
“Samahani,
nimekosea namba”
Ile namba
nikaizingatia. Jioni nilipotoka kazini nikaipiga. Simu yangu ikapokelewa na
msichana.
“We nani?”
akaniuliza.
“Mimi ni
yule uliyenitumia meseji asubuhi” nikamwambia.
“Ahaa
samahani, nilikosea namba”
“Ulikuwa
unamtumia mpenzi wako?” nikamuuliza.
“Ndiyo”
akanijibu.
“Nilijua
kuwa ulikosea namba lakini nilipenda tu kukufahamu, uko wapi?”
“Mimi?”
“Wewe ndiyo”
“Niko
Magomeni”
Magomeni ni
eneo lilioko pembeni kidogo mwa mji huo. Wakati huo viwanja ndio vilikuwa
vinatolewa na watu kuanza ujenzi wa nyumba.
“Unafnyaje
huko?” nikamuuliza baada ya kukosa la kumwambia.
“Ndiko
ninakoishi”
“Nataka nije
nikuone”
“Kwa ajili
gani?”
“Tujuane tu”
“Kwa lini?”
“Kwa leo”
“Haitakuwa
rahisi”
“Kwanini…”
Alikuwa
ameshakata simu. Nikampigia tena lakini simu yake ikawa haipatikani. Nikaachana
naye.
Jioni ya
siku ya pili yake nikampigia tena. Simu yake ikawa inaita. Iliita kwa muda
mrefu kasha ikapokelewa.
“Hallow!”
Sauti yake laini ikasikika kwenye simu.
“Hujambo?”
nikamuuliza.
“Sijambo”
“Habari ya
tangu jana?”
“Ahaa… wewe
ndio yule jamaa wa jana?”
“Ndiye mimi.
Nimekumiss…”
“Kumbe wewe
uko Tanga?”
ITAENDELEA
KESHO
No comments:
Post a Comment