HADITHI HII INALETWEA KWENU KWA HISANI YA MKOMBOZI SANITARIUM CLINIC MABINGWA WA TIBA ASILI, WAPO CHUDA TANGA, 0654 361333
YALIYONIKUTA TANGA (7)
ILIPOISHIA JUMATATU ILIYOPITA
Nikakata simu na kumfuta yule
kijana wa bodaboda.
“Shilingi ngapi?”
nikamuuliza.
“Ni elfu mbili tu”
Nikatoa noti za shilingi elfu
mbili na kumpa.
“Baadaye nitakupigia uje
unichukue, sawa?”
“Itakuwa saa ngapi?”
“Sijajua lakini haitakuwa saa
nyingi sana”
“Sawa”
Kijana akaondoka na pikipiki
na kuniacha pale pale. Nilisimama kwa dakika kadhaa huku nikitazama kila upande
kwa tamaa ya kumuona yule msichana. Nilipoona muda unazidi kwenda nikampigia.
“Nimekuchelewesha?”
akaniuliza.
“Naona muda unazidi kwenda
sioni mtu”
“Sasa sikiliza nikwambie,
fuata hiyo njia ya miguu iliyoko nyuma ya huo mbuyu uje moja kwa moja. Mbele
yako utakuta mwembe, utakata kushoto…”
SASA ENDELEA
“Si uliniambia utanifuata
hapa?” nikamuuliza.
“Ndiyo lakini kuja huko
nimeshindwa, mwenzko naogopa. Lakini wewe mwanume unaweza kuja tu”
“Kwani wewe uko wapi?”
“Niko huku nilikokuonesha”
Nikatupa macho katika eneo hilo lilioko nyuma ya ule
mbuyu. Niliona pori
tupu.
“Kwani kuna nyumba huko?”
“Ziko nyingi tu”
“Ngoja nije”
“Njoo, nikikuona nitakufuata”
Nikakata simu na kwenda nyuma
ya ule mbuyu. Nikaona njia ya miguu iliyoelekea kwenye pori. Halikuwa pori la kutisha bali lilikuwa la miti ya
mikoroshi na nyasi. Nikaifuata ile njia. Nilikwenda taratibu huku nikiangaza
macho mbele ya lile pori.
Kitu kilichonipa matumaini ya
kuwepo na nyumba ni kwamba nilipishana na watu wawili waliokuwa wakitoka katika
eneo hilo.
Nilikwenda hadi nikauona ule muwembe. Kulikuwa na njia upande wa kulia na
upande wa kushoto wa muwembe huo.
Nikakumbuka msichana
aliniambia nishike njia ya upande wa kushoto. Nikashika njia hiyo. Baada ya
kupiga hatua kadhaa nilianza kuona nyumba moja moja. Nyingine zilikuwa
zimekamilika, nyingine zilikuwa bado.
Msichana akanipigia simu,
nikaipokea.
“Nimeona mtu anakuja, sijui
ni wewe?” akaniuliza.
“Labda ni mimi kwa sababu
niko peke yangu”
“Umevaa tisheti nyekundu?”
“Ndiyo”
“Basi ni wewe, ngoja
nikufuate”
“Kwa hiyo nikusubiri hapa
nilipo au niendelee?”
“Njoo tu na mimi ninakuja.
Tutakutana”
Msichana akakata simu.
Nikaendelea kwenda. Mara nikaona msichana anakuja mbele yangu. Alikuwa amevaa
dera la mauaua. Nikahisi alikuwa ndiye yeye.
Alipofika karibu yangu
nikasimama, akaja akasimama mbele yangu.
“Nafikiri wewe ni mgeni
wangu” akaniambia huku akitabasamu.
“Bahati mbaya hatukuwa
tumeulizana majina. Lakini natumaini ni mgeni wako”
“Sawa. Mimi naitwa Maimuna.
Wewe unaitwa nani?”
“Mimi naitwa Martin”
“Nimefurahi kukufahamu,
karibu nyumbani”
Nikafuatana na yule msichana
kuelekea kule alikotoka.
Ingawa kulikuwa na giza, sura ya yule
msichana haikuwa ngeni machoni kwangu. Nilikumbuka kwamba niliwahi kumuona
mahali fulani pale pale Tanga lakini sikuweza kukumbuka vizuri nilimuona mahali
gani na sikutaka kumuuliza.
“Maimuna unaishi na nani?”
“Naishi na mama yangu”
“Ndiyo mmejenga huku?”
“Ndiyo tulikopata kiwanja”
“Lakini baada ya muda si
mrefu kutakuwa ni mji”
“Karibuni eneo lote
limeshapimwa isipokuwa watu wenyewe hawajaanza kujenga. Wengine wameanza lakini
wanakwenda taratibu”
“Nyinyi mmeshakamilisha
nyumba yenu?”
“Bado kidogo. Lakini tumeamua
kuhamia hivyo hivyo. Si unajua adha ya nyumba za kupanga?”
“Ninaijua. Mmefanya uamuzi
mzuri. Mtakamilisha kidogo kidogo wenyewe mkiwemo ndani”
“Bora tumepiga bati na
tunaweza kukaa, mambo mengine yatafuata. Hatunaharaka”
Tukatokea mbele ya nyumba
moja kama boma lakini lilikuwa limepigwa bati.
Ilikuwa imezungukwa na miti ya mikoroshi.
“Hapa ndio nyumbani” Msichana
akaniambia na kuongeza.
“Karibu ndani”
Alikuwa ametangulia kwenye
mlango akausukuma na kuingia ndani.
“Karibu” akaniambia.
Nikamfuata. Tulitokea kwenye
chumba kama sebule. Hakikuwa kimesakafiwa na
hata kuta za chumba hicho hazikuwa zimepigwa lipu. Juu kulikuwa wazi. Hakukuwa
na dari.
Sebule yenyewe ilikuwa
shaghalabaghala. Kulikuwa na makochi mawili yaliyokuwa yamechakaa na meza moja.
Taa ya fanusi ilikuwa imening’inizwa katikati ya chumba hicho.
“Karibu ukae” msichana
akaniambia.
Nilikaa kwenye kochi mojawapo.
Nikimlinganisha msichana huyo na ile nyumba vilikuwa ni vitu viwili tofauti.
Msichana alikuwa mzuri na mrembo kuliko maelezo lakini nyumba aliyokuwa akiishi
ilikuwa inatisha.
Lakini sikujali. Nilikuwa
nimevutika na yule msichana. Nilijiambia anafaa hata kumuoa.
Msichana aliongeza mwanga wa
ile taa ya fanusi kisha akaniambia.
“Nisubiri kidogo”
Alielekea uani.
Nikamsubiri. Hapo hapo simu
yangu ikaanza kuita. Nikaitoa mfukoni na kuona namba ya kachero mwenzangu
ambaye nyumba zetu zilikuwa jirani.
“Vipi John…?” nikamuuliza
mara tu nilipopokea ile simu.
“Umepata taarifa yoyote
kumhusu Sajenti Erick?” Sauti ya John ikaniuliza.
“Sijapata taarifa yoyote”
“Nimesikia Sajenti hakuripoti
leo kazini na mke wake amekwenda kulalamika kituoni usiku huu kuwa mume wake
hajamuona tangu asubuhi na hajulikani aliko”
“Niko mbali kidogo. Nikirudi
nyumbani tutazungumza”
“Sawa.
Endelea kufuatilia hadithi
hii kesho
Kwa maoni na ushauri piga namba 0655 9029292 au kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment